HADHI ya Ligi Kuu Tanzania Bara iko hatarini. Misimu miwili iliyopita kulikuwa na malalamiko ya ratiba ya ligi kupanguliwa mara kwa mara. Wahusika wakajirekebisha na kupunguza malalamiko.
Msimu huu wa ligi hiyo umekuwa na malalamiko yanayojumuisha mdhamini mmoja kwa zaidi ya timu moja, madai ya kuwapo upendeleo katika uchezeshaji wa marefa na baadhi ya timu kupanga kutuhumiwa kupanga matokeo.
Kukiwa na madai hayo mazito dhidi ya ligi hiyo inayotajwa kushika nafasi ya sita katika orodha ya ubora wa ligi barani Afrika, kuna hili la mwishoni mwa wiki -- mechi ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba kuahirishwa Jumamosi iliyopita saa chache kabla ya muda wachezaji kuingia uwanjani.
Mvutano uliosababisha kadhia hiyo iliyotafsiriwa na wataalam kuwa imesababisha madhara makubwa kiuchumi na kimichezo, ulitokana na madai ya timu ya Simba kunyimwa haki ya kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa siku moja kabla ya mechi hiyo.
Kwa mujibu wa Kanuni za Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), timu ngeni inaponyimwa nafasi ya kufanya mazoezi kwenye uwanja ambako mechi imepangwa kuchezwa, mechi itachezwa lakini timu mwenyeji itatozwa faini ya hadi Dola 5,000 kwa kuminya haki hiyo.
Tofauti na maelekezo hayo ya CAF ambayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni mwanachama wake, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikaamua kuahirisha mechi ya Yanga dhidi ya Simba, jambo ambalo uongozi wa klabu ya Yanga umelipiga vikali, hata kutoa taarifa kwa umma kwamba hautacheza tena mechi dhidi ya Simba kwa msimu.
Ni msimamo ambao unaiweka mechi yenyewe njiapanda. Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaelekeza timu inayosusia mchezo ipokwe pointi na ihesabike imepoteza mchezo husika kwa alama tatu na magoli matatu. TPLB iliyotoa uamuzi wa kuahirisha mechi kinyume cha kanuni, itawapoka Yanga pointi tatu kwa kususia mechi ijayo?
Kama hali hii itaendelea, itasababisha kuvurugika kwa ligi na itakuwa vigumu kwa mashabiki na wadau wa soka nchini kuendelea kuwa na imani na mfumo wa uendeshaji wa ligi yenyewe.
Ili kulinda hadhi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba sheria na kanuni zinaheshimiwa, na kwamba haki za timu zote zinazingatiwa kwa usawa na haki. Uongozi wa TFF na TPLB unapaswa kuchukua hatua za haraka ili kuzuia uharibifu zaidi wa hadhi ya ligi.
Ni muhimu pia watendaji waliohusika, hata kusababisha sintofahamu hii, wawajibike kwa maslahi ya umma kwa kujiuzulu nyadhifa zao. Ligi hii ina udhamini wa mabilioni kutoka kwa wawekezaji waliojitosa kusaidia ligi yenyewe na timu shiriki. Hakuna mwekezaji makini atakeyendelea kuwekeza fedha katika ligi inayozungumzwa kwa ubaya.
Benki, tena ya biashara, ndiyo mdhamini mkuu wa ligi. Kampuni ya habari iliyonunua haki za matangazo imelalamika kupata hasara kubwa kutokana na kuahirishwa kwa mechi hiyo.
Mashabiki wa soka waliotoka ndani na nje ya nchi kwenda Dar es Salaam kushuhudia mechi ya watani na wajasiriamali wa vyakula na vinywaji pia wamesikika kwa nyakati tofauti wakilalama kupata hasara kutokana na kuahirishwa kwa mechi hiyo.
Hali hii ikiendelea, kuna hatari mashabiki wasijitokeze viwanjani kwa kuwa hata wakikata tiketi, hawana uhakika wa kuchezwa kwa mechi za ligi hii.
Ili Ligi Kuu Tanzania Bara iendelee kuwa na hadhi na kuvutia, ni muhimu kwa wadau wote wa soka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, kushirikiana kwa dhati na kuhakikisha kuwa haki za timu, wadhamini na mashabiki zinaheshimiwa. Hii itasaidia kufuta malalamiko na kuimarisha nafasi ya ligi hii kama moja ya bora barani Afrika.
Shime, hatua zichukuliwe kulinda hadhi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kushuka.
Nipashe tutamatishe kwa hili, makandokando hayo yanayojitokeza, leo hii nafasi ya ligi hiyo imeporomoka kwa ngazi moja kutoka ya tano hadi ya sita barani.Hiyo ni tahadhari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED