KATIKA toleo letu la jana, tulikuwa na habari kuhusu marafiki Frida Chale (88) na Martha Jeremia (97) waliokutana mwaka huu baada ya kupotezana mwaka 1958, yaani miaka 67 iliyopita.
Mbali na kuangazia maisha ya urafiki wao na baada ya kupotezana kwa kipindi kirefu hicho, wawili hao walizungumzia baadhi ya mambo yanayotikisa jamii hivi sasa.
Hayo ni pamoja na ndoa nyingi kuvunjika, mauaji baina ya wanandoa, ukatili wa kijinsia na vijana wa kiume kutopenda kazi, hata kukimbilia kulelewa na kinamama wenye kipato, ambao wana umri sawa na mama zao, maarufu 'mashangazi'.
Bibi Frida aliyeanza kazi mwaka 1957 katika wilaya ya Arumeru mkoani Arusha akiwa Ofisa Maendeleo ya Jamii na baadaye kutumikia mashirika ya kimataifa, UNICEF na FAO katika nchi mbalimbali anasema kwa sasa kuna tatizo kubwa la malezi na kuporomoka kwa maadili miongoni mwa vijana, taasisi 'ndoa' ikiwa ni mwathirika mkuu wa kadhia hiyo.
Mtaalam huyo wa kimataifa wa masuala ya lishe na maendeleo ya jamii anasema kuwa kwa sasa ni vigumu kukutana na ndoa iliyodumu miaka 20 kutokana na wanandoa kukosa uvumilivu, utandawazi na kukosekana kwa hofu ya Mungu.
Kwa mujibu wa bibi huyo, hivi sasa ni kawaida kusikia mke amemuua mumewe, mume kaua mkewe, watoto kuua wazazi, baba kuwanajisi watoto wake, binti kuwapiga wakwe zake.
Ni kadhaa ambazo Nipashe tunaungana na bibi huyo kwamba ni mambo yaliyoshika kasi. Athari yake ni kuendelea kuweka visasi na chuki, hata kuchangia ongezeko la watoto wa mitaani na kukosekana kwa lishe bora katika familia, hivyo watoto kupata udumavu na kushindwa kufikiri vyema.
Bibi Frida ana lingine la ziada. Kwa mtazamo wake uzazi umekuwa mgumu. Vijana wa kiume wamekuwa wavivu, wamedumaa, hawawezi kufikiri na kujiongeza. Wengi wanapenda fedha za haraka na kusababisha matatizo ya kutoana kafara na kukata tamaa.
Katika hili, mtaalam huyo wa maendeleo ya jamii anashauri serikali ihakikisha vijana wa kiume wanajitambua na kupata ajira. Iwe ni lazima kwenda nyumba ya ibada. Chini ya mabalozi na viongozi wa kimila, iwe ni lazima kwa kila kijana wa kiume kuoa au wa kike kuolewa ili kuponya taifa dhidi ya kuporomoka kwa maadili.
Katika kulinda heshima ya ndoa, Nipashe tunaunga mkono hoja ya bibi huyo kwamba wazazi wasiingilie ndoa za watoto wao. Wabaki kuwa washauri tu na kuwaelekeza namna bora ya kuishi na serikali iendelee kuwekeza katika elimu ya kujitegemea ili vijana waachane na dhana ya kutegemea kuajiriwa tu.
Huyo ni Bibi Frida. Kikongwe mwenzake Martha (97), anasisitiza hoja ya kumcha Mungu, kusamehe na kuwapenda watu wengine. Kwa mtazamo wa Martha, kama alivyokuwa katika ndoa yake, mke akikosea, apige magoti mbele ya mumewe kisha mumewe amwombee kwa Mungu hekima na maisha marefu. Siyo kutukanwa na kupigwa!
Ni mtazamo ambao Nipashe si tu tunaupokea, bali pia tunaunga mkono hoja yake, tukiamini utasaidia kutatua matatizo yanayoandaa taasisi 'ndoa' na kuwapo matukio mengi ya mauaji miongoni mwa wanandoa huku serikali ikiripoti idadi kubwa ya ndoa zinazovunjika nchini.
Vikongwe hawa wanatoa hoja zinazohitaji kutekelezwa ili kuleta mabadiliko katika jamii. Maadili yanaathiri kila sehemu ya maisha ya watanzania — kutoka kwa familia hadi katika jamii pana. Ni wakati wa kupokea na kutekeleza mawazo haya ili kujenga jamii yenye maadili, inayoheshimu ndoa, na inayothamini haki za binadamu. Kunahitajika mabadiliko ya haraka!
Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na jamii ambayo inajivunia utamaduni wa kuenzi ndoa, familia na uhusiano wa kijamii. Maadili mazuri yatakuwa chachu ya maendeleo endelevu. Vijana watakuwa na mwelekeo mzuri na familia zitaendelea kuwa nguzo muhimu katika jamii.
Maadili ni msingi wa amani, upendo na ushirikiano. Ni mambo muhimu katika kujenga taifa lenye ustawi. Vikongwe hawa wana hoja kuntu. Zifanyiwe kazi!
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED