JUZI, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitia saini makubaliano ya ukusanyaji wa taka za plastiki na Kampuni ya 𝗚𝗔𝗜𝗔 𝗖𝗟𝗜M𝗔𝗧𝗘 ya Uturuki, mradi ambao unatarajiwa kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa vijana. Makubaliano hayo yalitiwa Saini jana baina ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, na Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Gediz Kaya, jijini Dar es Salaam.
Ushirikiano huo ni wa kupongezwa kwa kuwa utakuwa na manufaa makubwa kwa mazingira. Taka za plastiki kwa muda mrefu zimekuwa zikizagaa kwenye maeneo mbalimbali nchini na kusababisha madhara makubwa kwa viumbe hai wa majini na wa nchi kavu.
Mbali na athari mbaya kwa viumbe hai, pia taka za plastiki zimekuwa na madhara makubwa ya kiafya kwa binadamu zinapoingia mwilini. Kwa hiyo mpango huu ni habari njema kwa nchi na wapenda mazingira kwa ujumla kwa kuwa utasababisha mazingira kuwa safi na salama kwa viumbe.
Kwa muda mrefu, taka hizi hazikusanywi ipasavyo hali ambayo imechangia kuharibu mazingira na kuhatarisha maisha ya watu na viumbe hai. Inaelezwa kuwa kwenye mradi huo hata taka za nyavu ambazo mara nyingi huwa hazikusanywi na kuteketezwa, zitakuwa zinakusanywa na kuteketezwa.
Hali hiyo itasaidia kuokoa uhai wa mito na maziwa nchini kwa kuwa nyavu hizo zinapochakaa na kufikia mwisho wa matumizi, zimekuwa zikiishia kutelekezwa kwenye mito na maziwa.
Kwa ujumla, mradi huu umekuja wakati mwafaka na utaibua fursa ya kiuchumi kwa vijana ambao watakusanya taka za plastiki na kwenda kuziuza kwenye vituo vitakavyoanzishwa. Ni wakati mwafaka Watanzania tuone taka kama fursa ya kiuchumi kwa vijana kuchangamkia mradi huo utakapoanza ili kuondokana na umaskini.
Kama alivyosema Dk. Semesi wakati wa kutia Saini makubaliano hayo, anatarajia vijana wengi watanufaika na ukusanyaji wa taka za plastiki. Kwa hiyo ni matumaini ya baraza kuwa kupitia makubaliano hayo, mazingira yatatunzwa kwani taka zote za plastiki zitakusanywa na kurejelezwa kuwa bidhaa mbalimbali.
Uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya bahari unatajwa kuwa na athari kwa viumbe hai waishio chini ya maji kutokana na baadhi ya taka ikiwemo plastiki kuwa na madhara ya moja kwa moja kwa viumbe hao.
Umoja wa Mataifa umekuwa ukizitaka nchi wanachama kuhakikisha wanadhibiti taka hizo katika mataifa yao ili kuokoa maisha ya viumbe hai waishio chini ya maji pamoja na mfumo wa Ikolojia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), zaidi ya tani milioni 400 za plastiki huzalishwa kila mwaka kote duniani, nusu ya taka hizo hutumika tu mara moja, kati ya hizo, chini ya asilimia 10 ya plastiki huchakatwa, na kila mwaka takriban tani kati ya milioni 19 na milioni 23 huelekea kwenye Maziwa, Mito na Bahari.
Uchafuzi huo wa mazingira ni mwiba mkali kwa viumbe hai waishio chini ya maji kutokana na taka ngumu kama plastiki kutiririshwa baharini, mitoni na maeneo ya ziwani hivyo kuendelea kuhatarisha maisha ya samaki ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka.
Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) katika ripoti yake ya mwaka 2022 ilieleza kuwa idadi ya uchafu wa plastiki inayoingia kwenye mifumo ya ekolojia ya majini imeongezeka kwa miaka ya hivi karibuni na inakadiriwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka wa 2030.
Ripoti ya UNEP ya mwaka 2021 inaonesha kwamba plastiki huchangia asilimia 85 ya takataka za baharini na inaonya kuwa kufikia mwaka wa 2040, kiwango cha uchafu wa plastiki katika maeneo ya baharini kitaongezeka karibu mara tatu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED