Kila la heri Taifa Stars

Nipashe
Published at 11:24 AM Mar 24 2025
Kila la heri Taifa Stars
Picha: TFF
Kila la heri Taifa Stars

TIMU ya Tanzania, Taifa Stars, keshokutwa Jumatano itashuka dimbani kucheza dhidi ya Morocco kwenye mchezo wa Kundi E wa kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2026.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Honneur uliopo Manispaa ya d’Oujda nchini Morocco ambao unatumiwa na klabu ya Mouloudia.

Morocco inaongoza kundi hilo la E ikiwa na pointi 9 baada mechi 3 ikifuatiwa na Niger yenye pointi 6, Tanzania ikiwa ya 3 kwa kukusanya pointi 6, Zambia ikishika nafasi ya 4 kwa pointi 3 baada ya michezo 4 na Congo ipo nafasi ya 5 na haina pointi.

Pointi hizo ilizopata kwa kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Niger, Novemba 18, mwaka juzi, na ikashinda tena ugenini dhidi ya Zambia, Juni 11 mwaka jana.

Ilipoteza mchezo mmoja nyumbani, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikifungwa mabao 2-0 dhidi ya Morocco, uliopigwa, Novemba 21, mwaka juzi.

Katika kundi hili, Morocco ndiyo inayoongoza ikishinda michezo yake yote mitatu, ikivuna pointi tisa, ambapo inahitaji tena pointi zingine tatu dhidi ya Stars ili ifikishe 12.

Michuano ya Kombe la Dunia la mwaka 2026 itafanyika kati ya Juni 11 na Julai 19, mwaka 2026 zikiandaliwa kwa pamoja kwa nchi tatu za Marekani, Canada na Mexico.

Stars itashuka kwenye mchezo huo bila ya nahodha wake, Mbwana Samatta anayechezea Klabu ya PAOK ya nchini Ugiriki kutokanana na kuwa majeruhi.

Stars inahitaji ushindi ili kufikisha tisa na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele kuwania tiketi hiyo.

Mchezo huo ni muhimu sana kwa Stars hasa kutokana na msimamo wa kundi hilo la E na hivyo kwa namna yoyote inatakiwa kuhakikisha inaibuka na ushindi ili kijiweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kwa mashindano hayo makubwa zaidi duniani.

Licha ya ubora wa kikosi cha Morocco ambacho kilifika nusu fainali ya kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar, lakini Stars ina uwezo wa kuifunga iwapo wachezaji wake watajituma ipasavyo uwanjani.

Wachezaji wote wanatakiwa kutumia vizuri maelekezo ya kocha na benchi zima la ufunndi linaloongozwa na Hemed Morocco ili kuhahakikisha ushindi unapatikana kwenye mchezo huo.

Tunasema ushindi ni lazima kwa sababu pointi tatu zitainyanyua Stars kutoka nafasi yake ya tatu iliyopo sasa na kujivuta kwenye eneo la kufuzu kwa michuano ya kombe la Dunia.

Tuna imani na kocha Morocco pamoja na wachezaji wote walioitwa kwa ajili nya kuiwakilisha nchi, hivyo tunawatakiwa kila la kheri na wanatakiwa kupambana vya kutosha ili kuweza kuibuka na pointi zote tatu.

Tunajua kwamba kucheza kwenye uwanja wa ugenini ni ngumu kwa timu yoyote, lakini kujiamini na kujituma ndio silaha pekee ya kuhakikisha Stars inapata ushindi kwenye mchezo huo.

Wachezaji wanapaswa kujua kwamba, wanapoichezea timu ya taifa maana yake wanaipeperusha bendera ya nchi na pia wao wanajiweka kwenye nafasi nzuri ya kujitangaza kimataifa pale wanapoonesha kiwango bora uwajani.

Wachezaji waliobahatika kuiitwa kwenye kikosi cha Stars wana kila sababu ya kuipiganinia bendera ya nchini na kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo muhimu.

Nipashe tukiwa kama wadau wakubwa wa michezo hapa nchini, tunaitakia kila la kheri Taifa Stars kuelekea mchezo huo na tuna imani kubwa kwamba wachezaji watapambana vya kutosha na kuibuka na ushindi.

Rai yetu ni kwamba, wachezaji wanatakiwa kutumia mbinu zote walizopewa na benchi la ufundi pamoja na vipaji walivyojaliwa ili kujihakikishia ushindi kwenye mchezo huo.

Kila la kheri Taifa Stars.