Kufungiwa Uwanja wa Mkapa meneja anaweza kuwa tatizo

Nipashe
Published at 08:39 AM Mar 17 2025
Uwanja wa Mkapa.
Picha: Mtandao
Uwanja wa Mkapa.

WIKI iliyopita Watanzania walipata habari ya kushtusha baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kutangaza kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

CAF ilidai inaufungia uwanja huo kwa kutoridhishwa na eneo la kuchezea 'pitch.'

Habari hiyo ilileta sintofahamu, kwani moja ya timu ambayo ingeathirika moja kwa moja ni Simba, ambayo inatarajia kucheza mchezo wao wa marudiano wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry, unaotarajiwa kuchezwa Aprili 9, mwaka huu, uwanjani hapo.

Kwa maana hiyo italazimika kusaka uwanja mwingine, ndani ama nje ya nchi kwa ajili ya mchezo huo.

Kwa bahati nzuri, haraka sana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akalazimika kupoza 'presha' ya mashabiki na wadau wa soka nchini.

Kwanza akakiri kupokea tangazo hilo la kufungiwa uwanja huo, lakini akasema ukaguzi wa CAF ulifanyika kama wiki mbili zilizopita na ulifanyika baada ya mechi ya Simba na Azam, ambapo kabla ya hapo walikuwa wameshaufunga kupisha ukarabati.

Alisema mechi kama hizo huwa na mashabiki wengi na mambo mengi ya kiusalama, hivyo Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), liliwaomba litumie uwanja huo, ambapo kutokana na presha na ugumu wa mchezo wenyewe uwanja ukachimbika kidogo.

Akasema wakati wanacheza mchezo huo, wakaguzi wa CAF walikuwapo na waliwaeleza kuwa wahakikishe wanarekebisha na wakataka kuona mashine za kurekebishia sehemu ya kuchezea.

Hata hivyo, akasema hawakuweza kuwaonesha kwa kuwa mashine hizo zilikuwa njiani zinatoka kwa mtengenezaji nchini China.

Msigwa akasema mashine hizo ziliingia nchini baada ya siku tano tangu walipotaka kuziona na kutumika kufanya ukarabati wa uwanja huo.

Akamalizia kwa kusema tayari kwa sasa uwanja uko vizuri, na kuwataka TFF kuwaita CAF warejee tena kuukagua kwani kwa sasa uko vizuri.

Tunampongeza Msigwa na Serikali kwa ujumla, kwa kuwahi kutoa ufafanuzi na kutaka wakaguzi wa CAF waitwe haraka kuja kukagua. Uharaka huu unaweza kusababisha mechi ya Simba dhidi ya Al Masry kuchezwa kwenye uwanja huo, pamoja na Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ambayo ina michezo mbalimbali ya kimataifa, ikiwamo wa kusaka tiketi ya kufuzu Kocha la Dunia 2026 nchini Morocco.

Hata hivyo, tumekuwa na mashaka na manejimenti ya sasa ya uwanja huo kama iko makini na kazi yake, au kuna uzembe mahali.

Kwanza tunajiuliza, inakuwaje uwanja huo ambao hautumiki kucheza mechi za Ligi Kuu kwa sasa unaharibika baada ya mchezo mmoja tu kati ya Simba na Azam? Kuna mahali hakuko sawa. Nadhani meneja wa uwanja huo anapaswa kujiuliza na kujibu maswali haya.

Tunakumbuka misimu kadhaa nyuma, Uwanja wa Benjamin Mkapa, ulikuwa unatumika kwa mechi nyingi za Ligi Kuu, lakini bado ulionekana uko vizuri tu na kuendelea kuwavutia CAF kwa kutumika kwa michezo za kimataifa.

Simba na Yanga zilikuwa zinautumia kwa mechi zao zote za Ligi Kuu kama uwanja wao wa nyumbani. Bado kuna timu kutoka nje nazo zilikuja kuomba kuutumia kwa mechi zao za michuano mbalimbali, iwe ya klabu au za timu za taifa, lakini bado uliendelea kuwa bora sehemu ya kuchezea.

CAF wakaendelea kuukubali kutumika kwa Simba na Yanga kucheza mechi zao za kimataifa, Taifa Stars pia, na hata nchi jirani nazo zilikuwa zinakuja kuutumia pia. Na wakati huo hakukuwa na hata hizo mashine.

Iweje leo ambapo Simba na Yanga zinatumia Uwanja wa KMC Complex, uwanja unakaa muda mrefu bila kutumika, halafu uonekane hauko vizuri kwa kuchezwa mechi moja tu. Je kungekuwa na mlolongo wa mechi za ligi kama zamani ingekuwaje? Hapa tunaona kuna tatizo na linapaswa kumilikwa mapema kwa mustakabali mzuri wa kuulinda uwanja huo ambao umekuwa msaada mkubwa kwa timu za ndani na hata za nje kwa kuiingizia nchi mapato.