RAIS Samia Suluhu Hassan, tangu alipoingia madarakani mwaka 2021 kutoka kwa mrithi wake Hayati John Magufuli, alikuja na kaulimbiu yake ya ‘Kazi Iendelee’ ikiashiria kuwa yale yote yaliyokuwa yanafanywa na mtangulizi wake na hayajakamilika, yeye anayaendeleza.
Katika kipindi chake cha miaka minne madarakani, tumeona kaulimbiu hiyo ikitekelezwa kwa kasi kutokana na miradi mingi ambayo ilianzishwa na ikiwa bado haijakamilika, Rais Samia anaendelea kuikamilisha na mingine akiikamilisha.
Mfano mzuri ni Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambao Rais Samia ameukuta haujakamilika, lakini alipoingia madarakani ameukamilisha na sasa unafanya kazi.
Lile tatizo la mgawo wa umeme sasa limebaki kuwa historia, ingawa kila kwenye maendeleo kuna changamoto zake, lakini umeme wa uhakika sasa unapatikana na hata kuwa na mipango ya kuuza nchi za jirani.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambao pia ulikuwa haujakamilika kwa asilimia kubwa, sasa umeanza kutoa huduma kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma.
Wasafiri wengi sasa wameamua kukimbilai usafiri wa SGR kwa kuwa ni wa uhakika na unatumia saa chache kufika safarizao.
Kwa sasa wafanyakazi wanaweza kulala Dar es Salaam, lakini wakawahi kufika ofisini Dodoma bila wengine kujua hakulala Dodoma.
Haya ni mafanikio makubwa na hata mataifa mengine ya jirani yanaonekana kufurahishwa na maendeleo yanayofanyika Tanzania.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, umetoa taswira nzuri kwa Tanzania hasa kwa wageni wanaoingia nchini kutokana na kujengwa kisasa na kuwa vifaa vya kisasa vinavyorahisisha wageni kufanya uhakiki wa taarifa zao kwa wepesi.
Miundombinu ya barabara inaendelea kuboreshwa kuanzia barabara za juu hadi za mwendokasi. Kazi hii imekuwa ikiendelea nchi nzima na matokeo yanaonekana.
Barabara zimeleta maendeleo makubwa kwa kuwa katika kila eneo lenye miundombinu ya barabara nzuri kumefunguliwa shughuli mbalimbali za biashara yakiwamo maduka makubwa ya bidhaa.
Pia, barabara zimesaidia kupunguza msongamano uliokuwa ukiwakwamisha watu wengi kupoteza saa nyingi barabarani, badala ya muda huo kutumika kufanyakazi.
Katika kipindi chake cha miaka minne, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kutumia nishati safi ambayo lengo lake ni kumwondoa Mtanzania katika matumizi ya kuni na mkaa ambao umeleta uharibifu mkubwa wa mazingira.
Juhudi za Rais Samia zimeleta mafanikio kutokana na Watanzania wengi hivi sasa kuhamia kwenye nishati safi ya gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, hasa kwenye kupikia.
Hivi sasa katika maeneo mengi yenye migahawa, mama lishe na taasisi kubwa, wameamua kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye gesi na kuwaepusha kuvuta hewa chafu ambayo huwasababishia kupata magonjwa.
Kwa upande wa mashirika ya umma, Rais Samia amefanya mageuzi makubwa ya kuyafanya mashirika hayo kujiendesha yenyewe badala ya kutegemea rudhuku kutoka serikalini.
Kutokana na kujiendesha yenyewe, hivi sasa yanaweza kutoa gawio kwa serikali.
Mazingira mazuri ya uwekezaji pia, yamewavutia wageni wengi kuja kuwekeza Tanzania hali inayoifanya nchi kukua kiuchumi na kutoa ajira kwa Watanzania.
Sekta ya afya ni kati zilizopiga hatua kubwa nchini Tanzania kwa kupata watalaam mabingwa na vifaa vya kisasa na kusaidia wagonjwa wengi wanaokwenda kutibia nchi za nje sasa kutibiwa hapa hapa nchini na kuipunguzia serikali mzigo wa gharama za kutibia wagonjwa nje ya nchi.
Waswahili wanasema mnyonge mpeni haki yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED