Ushauri wa INEC kuelekea Uchaguzi Mkuu uzingatiwe

Nipashe
Published at 11:27 AM Jul 25 2025
Ushauri wa INEC kuelekea Uchaguzi Mkuu uzingatiwe
Picha:Mtandao
Ushauri wa INEC kuelekea Uchaguzi Mkuu uzingatiwe

WAKATI nchi yetu ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imewataka watendaji wa uchaguzi huo kufanya vikao na viongozi wa vyama vya siasa ili kujadili masuala mbalimbali yakiwamo ya uteuzi wa wagombea.

Uchaguzi Mkuu ni muhimu katika nchi yoyote na ndio dira ya kupata taswira ya taifa katika kuchagua viongozi bora kutokana na jinsi walivyojinadi katika kipindi cha kampeni, dira, mipango mikakati na huduma kwa jamii. Matokeo ya uchaguzi ni kupata serikali imara kutoka kwenye chama kilichoshinda na kukubalika na wananchi, kutokana na Sera, maendeleo ya miradi, na siasa safi zenye kueleza na kuenzi ulinzi, amani wa mshikamano wa taifa.

Katika kufanikisha hayo INEC imeeleza umuhimu wa watendaji kuhusu usimamizi wa shughuli za kila siku za masuala ya uchaguzi kwa kuanza na vikao na vyama vya siasa, utoaji wa fomu za uteuzi na uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na kuhakikisha utoaji wa fomu za uteuzi na uteuzi wenyewe ngazi ya udiwani unafanyika kwa mujibu wa sheria.

Umuhimu wa kuitisha na kuratibu kamati za upangaji wa ratiba za kampeni na kuitisha kamati za maadili na kubaini iwapo kuna changamoto zitajitokeza wakati wa kampeni.

Watendaji hao wanakumbushwa wajibu wao wa kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya vituo na kuratibu na kusimamia vizuri na kwa weledi uchaguzi ngazi za vituo.

INEC inasisitiza kuwa mafunzo watakayotoa watendaji hao yatawawezesha kuratibu na kusimamia uchaguzi ngazi ya kata  na kwa weledi na kwamba jukumu lao ni kutoa mafunzo sahihi, kwa kuonesha kwa vitendo yote wanayotakiwa kuyafanya wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata.

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani (mstaafu), Mbarouk Salim Mbarouk, amewakumbusha watendaji hao wajibu wao wa kubandika mabango, orodha ya majina ya wapiga kura na matangazo au taarifa zinazopaswa kuwafikia wapiga kura kwa kuwa ni takwa la kisheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi.

Mabango, matangazo, orodha ya majina ya wapiga kura na taarifa yoyote inayotakiwa kubandikwa kulingana na kalenda ya utekelezaji wa majukumu ya uchaguzi lazima yabandikwe ili kuepusha malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya sheria na kanuni za uchaguzi.

Watendaji hao wanatakiwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari ili kuwajulisha wananchi na wadau mambo mbalimbali ya uchaguzi.

Watendaji pia wanatakiwa kujiandaa kabla ya kukutana na vyombo vya habari kwa kupima taarifa zao wanazotaka kutoa ili kuepuka kuleta taharuki badala ya utulivu katika eneo wanalotoka.

Watendaji hao wameanza kuandaliwa kwa mafunzo yaliyofanyika kwenye mikoa mbalimbali nchini yakijumuisha waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo.

Tume iliyagawa mafunzo hayo kwenye awamu mbili, awamu hii ilihusisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Mwanza, Mara, Dar es Salaam, Pwani, Rukwa, Katavi, Manyara, Arusha, Songwe na Mbeya.

Awamu ya kwanza ilifanyika mikoa ya Morogoro, Singida, Dodoma, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Mjini Magharibi, Geita, Kagera, Mtwara, Lindi, Tabora, Kigoma, Tanga, Kilimanjaro, Ruvuma, Iringa na Njombe.