Dk.Biteko mgeni rasmi Nishati Bonanza 2025

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:34 PM Jun 27 2025
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Wizara ya Nishati na Taasisi zake litakalofanyika Jumamosi Juni 28, 2025 jijini Dodoma.

Akizungumzia maandalizi ya Bonanza  hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati, Neema Mbuja amesema kuwa, Nishati Bonanza litafanyika kwenye Viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma na kushirikisha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na wadau kutoka Wizara nyingine.

‘’ Nipende kuchukua fursa hii kuzikaribisha taasisi zilizo chini ya  Wizara ya Nishati  kushiriki kikamilifu  bonanza ambalo linaleta fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo baada ya muda wa kazi pamoja na  kufanya mazoezi ili kujenga afya." amesema Mbuja


Ameongeza kuwa, kwa  mwaka huu Nishati Bonanza  linaongozwa na kauli mbiu ya "Michezo kwa Afya bora, Shiriki uchaguzi 2025 ikiwa na lengo pia la kuhamasisha wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 .

Amesema maandalizi yote yameshakamilika na timu zitakazoshiriki michezo mbalimbali zimeshawasili Dodoma kushiriki bonanza hilo litakaloshirikisha watu takribani 1000.

Ametaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni  ni pamoja na Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Mpira wa Kikapu, Kuvuta Kamba, pamoja na  michezo ya jadi kama vile bao na drafti, pia   kufukuza kuku.

Taasisi zitakazoshiriki Bonanza hilo la  Nishati ni pamoja na TANESCO, REA, TPDC, PURA, EWURA, TGDC, ETDCO, TCPM, TANOIL, GASCO, PBPA.

Hili ni Bonanza la pili kufanyika tangu kuasisiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko mwaka jana.