MSAFARA wa Yanga 'umesoteshwa' kwa saa nne kwenye Uwanja wa Ndege baada ya kuwasili nchini Algeria kwa ajili ya kucheza mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji MC Alger itakayofanyika kesho jijini Algiers.
Mechi hiyo ya Kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Juillet 5 kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Kikosi cha Yanga kiliwasili salama nchini humo lakini kililazimika kutumia zaidi ya saa nne kwenye uwanja wa ndege ili kukamilisha taratibu za uhamiaji na kusubiri mizigo yao na kuanza safari ya kuelekea hotelini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Alex Ngai, alisema kwa kile walichokikuta na kukipata uwanjani, ni ishara mechi ya mpira wa miguu dhidi ya wapinzani wao imeanza rasmi nje ya uwanja.
Ngai alisema walishangazwa kuona ucheleweshaji wa kukamilisha taratibu za uhamiaji na kusababisha kutumia muda mrefu wakiwa uwanjani hapo.
"Kiukweli mechi imeanza rasmi, tumefika saa sita usiku, lakini hadi kutoka hapa uwanja wa ndege tumetumia kama saa nne, tumetumia saa mbili kwenye masuala ya uhamiaji, mawili mengine kusubiria mizigo yetu, lakini tunashukuru mwisho wa yote mizigo mingi imepatikana, bado michache ambayo meneja anaendelea kuifuatilia nina imani ataipata.
Nadhani sasa mechi ya mpira wa miguu iliyotuleta hapa Algiers imeanza rasmi nje ya uwanja, hatukutarajia, lakini tulijipanga kwa sababu mechi hizi za Kiafrika zina matatizo sana, wala hii haitatutoa mchezoni, tuna viongozi na wachezaji ambao ni wazoefu katika michezo kama hii ya kimataifa," alisema Ngai.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema walitumia saa saba kutoka Dubai hadi Algiers, kabla ya kukutana na saa nne nyingine uwanja wa ndege.
Kamwe alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri na changamoto hiyo waliyokutana nayo ni ya kawaida na haiwaondoi kwenye malengo ya kusaka ushindi hapo kesho.
"Hebu angalia hapo, tumetumia zaidi ya saa 10, kutoka Dubai hadi hapa, yote kwa yote tumekuja katika mapambano, baada ya kuanza vibaya kwa kufungwa, mchezo huu wa pili hatutaki kupoteza, tumekuja kwa ajili ya kulinda heshima ya klabu yetu ya Yanga," alisema Kamwe.
Kuhusu hali ya baridi, Kamwe alisema waliamua kwenda mapema nchini huko ili kuzoea hali hiyo.
"Daktari wetu alisema kama tutatumia zaidi ya saa 48, itatusaidia kuzoea hali ya hewa, na hichi ndio tulichokifanya kuhakikisha tunakuja (Algeria), mapema," aliongeza ofisa huyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sead Ramovic, jana aliwafanyisha wachezaji wake mazoezi ya kuweka miili sawa baada ya safari ndefu.
"Mazoezi haya ya leo (jana), ni ya kuweka miili ya wachezaji sawa, tutakuwa tunafanya majira ya saa 2:00 usiku kwa saa za hapa kwa sababu ni muda ambao mechi yetu itachezwa, sababu nyingine ni kuzoea hali ya hewa maana baridi huku ni kali sana," alisema kocha huyo.
Yanga ilianza hatua hiyo ya makundi kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Al Hilal Omdurman ya Sudan, mechi iliyochezwa Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati MC Alger ililazimisha suluhu ya ugenini dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).
Al Hilal ndio kinara wa Kundi A, ikifuatiwa na MC Alger, TP Mazembe na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanaburuza mkia.
Wawakilishi wengine wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Simba nao wako Algeria na kesho watashuka dimbani kuwavaa wenyeji, CS Constantine, katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED