Dk. Mwinyi awaahidi Kusini Unguja skimu za umwagiliaji, pembejeo bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:36 PM Oct 14 2025
Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya kuinua sekta ya kilimo kwa kujenga skimu mpya za umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa zana za kisasa, na kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ili kudhibiti bei ya mchele nchini.

Akizungumza na wakulima wa mpunga, mwani na wavuvi katika uwanja wa Marumbi, wilaya ya Kati, mkoa wa Kusini Unguja, Dk. Mwinyi amesema serikali inatambua changamoto zinazowakabili wakulima wa mpunga, ikiwemo uhaba wa zana za kilimo na pembejeo, na kwamba hatua madhubuti zimeanza kuchukuliwa ili kuboresha sekta hiyo.

“Serikali inaendelea kuhakikisha tunapanua skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mpunga. Tunajua tunahitaji zana za kisasa, na ahadi yetu ni kuleta matrekta makubwa, ‘powertillers’, pamoja na mashine za kuvunia. Vifaa hivyo vitasaidia kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji,” amesema Dk. Mwinyi.

Ameongeza kuwa serikali itaendelea kusambaza pembejeo muhimu kama mbolea, mbegu bora na viuatilifu kwa wakati pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa wakulima, ili kuhakikisha Tanzania inapunguza uagizaji wa mchele kutoka nje ya nchi.

Kuhusu bei za mchele, Dk. Mwinyi amesema serikali imeshapanga kujenga maghala ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi na kununua mpunga kutoka kwa wakulima wa ndani, hatua itakayosaidia kudhibiti mfumuko wa bei mara baada ya kipindi cha mavuno.