Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeahirisha hadi Januari 28, 2026 kesi ya uhujumu uchumi Na. 000021172/2025 inayomkabili mwanaharakati wa mitandao ya kijamii, Mange Kimambi, baada ya upande wa Mashtaka kueleza kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Shauri hilo liliitwa leo Desemba 4, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Hassan Makube, ambapo upande wa Jamhuri uliomba tarehe nyingine ili kuendelea na taratibu za uchunguzi. Katika hatua hiyo, upande wa utetezi haukuwa na wakili mahakamani, jambo lililomfanya Hakimu Makube kuagiza upande wa Mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika kabla ya tarehe iliyopangwa, ili shauri liweze kuanza kusikilizwa rasmi.
Mange Kimambi anakabiliwa na shtaka la utakatishaji wa fedha kiasi cha Sh138.5 milioni, akidaiwa kuyapata kati ya Machi 1 na 31, 2022 jijini Dar es Salaam kupitia kufanya kazi ya uandishi wa habari bila kibali pamoja na kutumia vitisho. Shtaka hilo limetajwa chini ya kifungu cha 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha (Sura ya 423, 2019), likihusishwa pia na masharti ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Katika siku za karibuni, video iliyosambaa mitandaoni ilimuonesha Mange akidai kupata taarifa za mwenendo wa kesi hiyo na akadai kuwa Serikali inapanga kumrudisha nchini kupitia Sheria ya Uhamisho wa Watuhumiwa kutoka mataifa ya nje (Extradition Act, 2019).
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, naye amethibitisha kuwa ofisi yake inaendelea kuchunguza uwezekano wa kumchukulia hatua Mange kutokana na tuhuma za kuchochea maandamano, na kwamba mikataba ya ushirikiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Marekani ndiyo inayoongoza mchakato huo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED