Kampuni ya Meta imeanza kuondoa akaunti za vijana walio chini ya umri wa miaka 16 kutoka kwenye mitandao yake ya kijamii nchini Australia, ikiwa ni hatua ya maandalizi kuelekea marufuku mpya iliyotangazwa na Serikali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa sheria hiyo, watoto walio chini ya umri wa miaka 16 hawataruhusiwa kuwa na akaunti katika majukwaa kama TikTok, Facebook, YouTube na Instagram.
Meta, ambayo ni kampuni mama ya Facebook na Instagram, ilitangaza mwezi uliopita kuwa imeanza kuwafahamisha watumiaji wenye umri wa kati ya miaka 13 na 15 kwamba akaunti zao zitaanza kufungwa kuanzia Desemba 4, 2025. Hatua hiyo itaathiri takriban watumiaji 150,000 wa Facebook na zaidi ya akaunti 350,000 za Instagram nchini humo.
Mitandao kama Threads, ambayo inafanya kazi kwa mtindo unaofanana na X (zamani Twitter), inapatikana kupitia akaunti ya Instagram, ambayo pia itahusika katika utekelezaji wa sheria hiyo.
Australia inakuwa taifa la kwanza duniani kutekeleza marufuku ya aina hii kwenye mitandao ya kijamii. Kuanzia Desemba 10, kampuni zote zinazotoa huduma hizo zitakabiliwa na adhabu ya faini hadi A$49.5 milioni (sawa na takriban US$33 milioni au £25 milioni) endapo zitashindwa kuchukua “hatua zinazofaa” kuhakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 16 hawafungui akaunti.
Hatua hii imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Australia kulinda usalama wa watoto mtandaoni na kupunguza madhara ya kiafya na kijamii yanayoweza kusababishwa na matumizi ya mitandao ya kijamii katika umri mdogo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED