WAFANYAKAZI nchini Kenya watalazimika kulipa hadi KSh 2,160 (Sh 41,413) kwa mwezi kwenye Hazina ya kitaifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanzia Februari 2026, kutokana na ongezeko la kiwango cha michango ya lazima ya pensheni. Hii itazidisha mzigo wa kifedha kwa familia huku gharama za maisha zikiongezeka.
Mjadala wa makato ya serikali ili kugharamia uchumi wa nchi ulianza kujipenyeza tangu wakenya kulazimika kulipa asilimia tatu ya mshahara wao ili kuhudumia hazina mpya ya Maendeleo ya Makazi.
Serikali ya Kenya imesisitiza kuwa malipo hayo sio kodi bali ni hakiba ingawa makato hayo yatalindwa na sheria na kutolewa kwenye mishahara ya wafanyakazi.
Inaelezwa kuwa makato hayajaishia hapo, mshahara wa walioajiriwa pia umepungua zaidi kutokana na nyongeza ya ada kwa mfuko wa huduma ya afya ya jamii yaani (SHIF).
WATAKAOTOZWA ZAIDI
Kulingana na mfumo mpya, wafanyakazi wanaopata mshahara wa zaidi ya KSh 100,000 (Sh milioni 1.9) kwa mwezi watalipa KSh 6,480 (Sh 124,239) kila mwezi, kutoka kiwango cha sasa cha KSh 4,320 (Sh 82,826). Na kwamba wale wanaopata chini ya KSh 100,000 michango yao itapanda hadi KSh 6,000 kutoka KSh 4,320.
Hata hivyo, wafanyakazi wenye mapato ya chini ya KSh 50,000 (Sh 958,635) kwa mwezi hawataathirika na ongezeko hilo, na wataendelea kulipa kati ya KSh 1,500 hadi 2,100 kulingana na kipato chao.
Inaelezwa kuwa ongezeko hilo linafuata mageuzi ya hivi karibuni kwenye NSSF, ambayo yamegawanya mchango wa pensheni wa lazima wa asilimia 12 kwa usawa kati ya mwajiri na mfanyakazi.
Mwaka jana, NSSF pia iliongeza kiwango cha juu cha michango, ambako safu ya kwanza iliongezeka hadi KSh 960 (Sh 18,405) kwa mwezi, na safu ya pili kwa wale wanaopata mshahara wa zaidi ya KSh 70,000 (Sh milioni 1.3) ilipanda hadi KSh 8,400 (Sh 161,051).
Ongezeko la hivi karibuni linatarajiwa kuongeza shinikizo kwa wafanyakazi ambao tayari wanakabiliana na kupungua kwa uwezo wa kununua, kutokana na mfumuko wa bei, kodi kubwa na makato mengine ya lazima.
Mageuzi ya NSSF yanalenga kuongeza akiba za kustaafu na kuboresha usalama wa pensheni kwa muda mrefu, lakini wakosoaji wanasema kuwa muda wa ongezeko hilo unaweza kuongeza matatizo ya kifedha kwa wafanyakazi wasio na kandarasi ya kudumu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED