RAIS wa Uganda Yoweri Museveni anatarajiwa kuandaa mkutano wa maalum wa mawaziri kujadili kuhusu hali ya usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Henry Okello, mkutano huo, utakaofanyika Desemba 21, mwaka huu katika Ikulu ya Entebbe, kilomita 40 kusini mwa Kampala, mji mkuu wa Uganda, unalenga kutuliza mapigano yanayoongezeka mashariki mwa DRC.
Waziri Okello alielezea kwamba mkutano huo unakamilisha makubaliano yaliyofikiwa Washington, Nairobi, na Luanda, pamoja na mipango ya Qatar ya kukomesha miongo kadhaa ya migogoro katika eneo hilo.
“Rais Museveni anatimiza tu mipango iliyochukuliwa Nairobi, Luanda, na kisha Washington, na hapa tuliko. Juhudi zinazofanywa na kila nchi, au na viongozi wao, zinalenga kushughulikia mapengo yoyote ambayo yanaweza kuonekana katika mchakato huu.
“Baada ya makubaliano ya Washington, mgogoro uliongezeka tena. Kwa uzoefu wangu katika eneo hilo, hali nchini DRC inaeleweka vyema na wahusika wa kikanda. Uganda na Rais Museveni wako katika nafasi nzuri zaidi. Tunajua historia ya mgogoro huu na maendeleo yake,” Okello amesema.
Ameongeza kwa kubainisha kwamba eneo hilo liko katika nafasi nzuri zaidi ya kupata suluhisho la matatizo ya nchini DRC.
Mapigano mashariki mwa DRC yameongezeka, huku kundi la M23 likisonga mbele hadi ngome mpya licha ya kusainiwa, mnamo Desemba 4, mwaka huu kwa makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani kati ya DRC na Rwanda.
Siku ya Jumatano, M23 ilianza kujiondoa kutoka katika mji wa Uvira, mji wa kimkakati mashariki mwa DRC, siku chache tu baada ya kuuteka.
Kundi hilo la waasi lilisema kwamba kujiondoa huku kulifanyika kwa ombi la wapatanishi wa Marekani na ilikuwa hatua ya kujenga imani ili kuunga mkono mchakato wa amani unaoendelea
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED