Askofu Mkuu wa Kanisa Aglikana Tanzania Dk. Maimbo Mndolwa, ameeleza namna ambavyo aliyekuwa Spika mstaafu wa bunge Hayati Job Ndugai, alivyotumia kipawa chake alichopewa na Mungu cha ushauri kumsaidia kuvuka kwenye magumu aliyopitia wakati fulani.
Amesema hayo leo Agosti 11,2025 wakati akihubiri kwenye ibada ya kuombea mwili wa Hayati Ndugai iliyofanyika kwenye Kanisa Aglikana Tanzania la Mtakatifu Michael Dinar ya Kongwa.
Askofu Dk. Mndolwa amesema Mungu alimjalia Hayati Ndugai vipawa vingi ambavyo naye alivitumia kwa ajili ya kusaidia wengine na hakuwa mbinafsi.
Amesema wanajua kuwa Mungu alimjalia kipawa cha ulimi ulio mnono ulimi uliosafi kauli zake wakati mwingi akisimama zisizo na shaka, na wakati mwingine akizisema ukimtazama usoni unajua hapa inasikika sauti fulani.
“Siyo wote wanapewa hiyo, amekitumia vema kipawa hicho akiwa katika mamlaka ameitumia vema hata alipostaafu hata alipo endelea na ubunge na mimi nakumbuka nikiwa katika changamoto ngumu katika maeneo fulani nilimwita yeye na tuliongozana mara kadhaa.
“Na mara ya mwisho tulipoongozana katika safari moja kulikuwa na magumu kabisa lakini kwa kutumia ndimi yake karama aliyopewa na Mungu ilisaidia kutuliza jazba ya pale tulipokuwa na hatimaye kazi ya Mungu ikaenda,”amesema Askofu Dk. Mndolwa
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED