Bussungu aahidi wafungwa kulipwa posho, kufundishwa stadi za maisha Magerezani

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 11:59 AM Oct 21 2025
Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu.

Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu, ameahidi kufanya mageuzi makubwa katika Idara ya Magereza endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, kwa kuhakikisha wafungwa wanapatiwa mafunzo ya stadi za maisha na kulipwa posho kwa kila kazi watakayofanya, ili ziwe mtaji wa kuanzisha maisha mapya baada ya kumaliza vifungo vyao.

Akizungumza leo na wananchi wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, katika mwendelezo wa kampeni zake, Bussungu alisema lengo la serikali yake litakuwa kubadilisha mfumo wa magereza kutoka kuwa taasisi za adhabu pekee hadi kuwa vituo vya urekebishaji na maendeleo ya binadamu.

“Wafungwa wengi wanatoka magerezani bila ujuzi wowote wa kujitegemea, matokeo yake hurudia uhalifu. Serikali yangu itahakikisha kila gereza linakuwa kituo cha mafunzo ya stadi za kazi kama vile ufundi, kilimo, ushonaji, useremala, na kompyuta ili wakitoka waweze kujitegemea na kuacha kuiba,” alisema Bussungu.

Bussungu aliongeza kuwa changamoto kubwa kwa wafungwa wanaomaliza vifungo ni kukosa ajira au shughuli ya kufanya, jambo linalowarudisha kwenye makosa ya awali. Ili kukabiliana na hilo, amesema serikali yake itawawezesha kupata ujuzi na mitaji midogo ya kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.

Aidha, alieleza kuwa mfumo wa sasa wa magereza hauwasaidii wafungwa kurekebisha tabia bali unachangia kuendeleza uhalifu, hivyo ataweka mpango wa kuhakikisha kila mfungwa anapata mafunzo kulingana na uwezo na mahitaji yake.

Ameahidi pia kuwa magereza yataanza kushirikiana na vyuo vya ufundi na taasisi za maendeleo ya vijana katika utoaji wa mafunzo hayo, ili kuongeza ubora na ufanisi.

Bussungu alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, taasisi binafsi, na jamii katika kuwasaidia waliokuwa wafungwa kuanza upya maisha yao:

“Mfungwa si adui wa Taifa, bali ni raia aliyekosea. Tunapaswa kumsaidia ajirekebishe, ajinue kiuchumi, na kuwa raia mwema anayeweza kuchangia maendeleo ya nchi.”