Samia aahidi ujenzi barabara, ‘flyover’ Dar kupunguza msongamano

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:58 PM Oct 21 2025
news
Picha CCM
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ametaja mikakati yake ya kuimarisha miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam ikiwemo kukamilisha ujenzi wa barabara pamoja na kuanzisha miradi mipya kama ujenzi wa ‘Flyover’ katika barabara za makutano ili kuondoa msongamano.

Dk. Samia aleyaahidi hayo leo Oktoba 21, 2025 mkoani Dar es Salaam akiwa kwenye mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Dk. Samia amesema katika miaka mitano ijayo, serikali atakayoiunda ikiwa atapewa ridhaa itajenga barabara za juu (Flyover) kwenye makutano ya barabara za Mwenge, Morocco, Magomeni, Ali Hassan Mwinyi na United Nation.

Amesema lengo la kumalizia ujenzi wa barabara  na kuweka barabara za juu ni ili kuongeza ufanisi na kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii mkoani Dar es Salaam.

“Pia tutashughulikia maeneo yenye kukabiliwa na changamoto ya mafuriko Jijini Dar es Salaam ikiwemo Mto Mbezi, Mto China na Mto Gide. Mradi wa uendelezaji wa Dar es salaam (Dar es Salaam Metropolitan Development Project – DMDP) awamu ya pili utaondoa changamoto hizo,” amesema Dk. Samia.

Amesema katika utekelezaji wake watajenga na kukamilisha pia mifereji ya maji ya mvua katika maeneo ya Tandale, Magomeni na Makumbusho ili kuondoa adha ya mafuriko katika maeneo hayo ya Kinondoni jijini humo.

1
Aidha, Dk. Samia amesema ndani ya miaka mitano ijayo ikiwa atapewa ridhaa ya kuunda serikali, atakamilisha ujenzi wa barabara ya Kimara- Mavurunza- Bunyokwa- Kinyerezi, yenye urefu wa Kilomita saba, barabara muhimu kwa maendeleo ya majimbo matatu ya Segerea, Kibamba na Ubungo.

Kadhalika, ameahidi kutekeleza miradi mipya katika wilaya hiyo ikiwemo upanuzi wa barabara ya Mwai Kibaki sehemu ya Kilomita tisa kutoka Morocco hadi Kawe na barabara ya Garden (Garden road).

Barabara nyingine ni ya Tegeta - Bagamoyo yenye jumla ya urefu wa Kilomita 57 na kukamilisha barabara ya Kibamba - Mloganzila, sehemu ya Mloganzila mpaka Mloganzila Citizen yenye urefu wa Kilomita nane.