Bussungu: Nitanunua ndege za doria kila mkoa kuimarisha Usalama wa Taifa

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 11:47 AM Oct 21 2025

Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu.

Mgombea urais wa Chama cha ADA-TADEA, Georges Bussungu, ameahidi kuiimarisha Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi kwa kununua ndege maalumu za doria katika kila mkoa endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu.

Akizungumza leo na wananchi wa Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, katika mwendelezo wa kampeni zake, Bussungu alisema taifa linakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama ikiwemo ujambazi, usafirishaji wa dawa za kulevya, ujangili, uhalifu wa mipakani na vitendo vya utekaji, hivyo kuna umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa ya anga kudhibiti uhalifu.

“Kila mkoa utapewa ndege maalum ya doria — si ya abiria bali yenye teknolojia ya kisasa ya kufuatilia maeneo kwa haraka. Polisi wetu hawatatembea tena kwa miguu au pikipiki kuwafuata majambazi porini au kufuatilia uhalifu wa usiku,” alisema Bussungu.

Ameongeza kuwa nchi haiwezi kuwa salama iwapo itaendelea kutumia mbinu za zamani za ulinzi, wakati wahalifu wanatumia teknolojia ya kisasa kufanya uhalifu. Kwa sababu hiyo, amesema atafanya mageuzi makubwa ndani ya Jeshi la Polisi kwa kufuta kitengo cha Upelelezi (CID) na kuanzisha kikosi maalumu cha kitaalamu cha upelelezi, kama ilivyo katika baadhi ya nchi zilizoendelea.

Bussungu alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi kubwa, hivyo haiwezi kusubiri wahalifu wachukue hatua ndipo vyombo vya ulinzi viitwe. Amesema ndege hizo zitawawezesha polisi kufuatilia harakati za kihalifu kwa wakati halisi, kudhibiti mipaka, miji na vijiji kwa ufanisi mkubwa.