JE, ni muda upi una faida zaidi kwenye kuoga? Unakuwa na faida zaidi unapooga asubuhi ukiamka au kabla ya kwenda kulala? Katika dunia ya sasa inayozidi kuwa na watu wenye haiba wanaopenda ulimbwende, urembo, ngozi zilizong’arishwa, vichwa visivyokuwa na mvi hata kama ni mzee mwenye miaka 70, harufu za manukato, kutumia vitakasa mikono ndizo ‘sanitaiza’ bado kuna swali ambalo linawagusa wote , muda bora wa kuoga ni asubuhi au usiku?
Lakini wapo ambao labda hawaogi kila siku wanasema wanapiga ‘pasipoti’ na kubadili nguo muhimu. Hata hivyo wanaweza kujibu swali hili, bila kujali misimamo yao, kikubwa ni chaguo lako lina athari gani za kiafya katika mwili wako?
Angelus Nyirenda, mkazi wa Kibaha mkoa wa Pwani, anasema muda bora wa kuoga ni asubuhi kwa sababu, mosi huondoa taka zilizo kwenye ngozi na kuifungua ili mwili uwe ‘fresh’ na mwili mzima uchangamke. Damu inatembea kikamilifu kwenye ngozi, mwili unaamka na kuweka uwiano sahihi wa joto na baridi. Misuli inasisimuka na ubongo na akili pia huwaza kwa kasi hufanyika kiufanisi.
Anaungwa mkono na Enock Mfuru, anayesema muda mwafaka wa kuoga ni asubuhi kwa vile huupa mwili hali mpya na kuuandaa tayari kwa kazi baada ya siku mpya kuanza. Ni afya zaidi kuoga asubuhi na pia jioni inafaa kuoga lakini pia ni muhimu zaidi unapoamka ili uburudike, uwe mzima, uamshe misuli, mishipa ya damu nay a fahamu pia.
BBC inazungumzia suala hilo, ikisema kuwa kwa wengi wetu, baada ya kuamka asubuhi na matongotongo machoni moja ya mambo ya kwanza tunayofanya ni kukimbilia kuoga.Watetezi wa kuoga asubuhi mara nyingi hubishana kuwa kutumia dakika 10 kujiburudisha chini ya maji ya moto huwasaidia kuamka wakiwa wameburudika na wako tayari kuanza siku. Hata hivyo, wale wanaooga usiku hubishana kuwa kuoga kabla ya kulala huwasaidia kuondoa uchafu wa mchana kabla ya kuingia katika shuka na kulala kwa utulivu.
MAISHA VIMELEA
Kuoga huondoa uchafu, grisi na jasho kwenye ngozi za biandamu. Ikiwa hutaoga kabla ya kulala, mabaki haya hutulia kwenye shuka na foronya zako.
Lakini si hivyo tu. Ngozi yako hujaa vimelea.Ukichunguza kwa karibu ngozi yako, utapata kati ya bakteria 10,000 na 1, 000,000 wanaoishi humo. Wanakula mafuta yaliyofichwa na jasho lako.
Ingawa jasho lenyewe pengine haliwastua wengine lakini lipo na ‘salfa’ inayozalishwa na bakteria kama vile ‘staphylococcus’ lazima hutoa harufu.
‘Salfa’ inachangia harufu ya mwili kwanza hutoka kupitia jasho na pumzi, hasa baada ya kula vyakula vyenye salfa nyingi kama vile vitunguu, vitunguu saumu na tangawizi.
Kwa hivyo, kuoga kabla ya kulala kunaweza kuonekana kama chaguo la usafi zaidi, lakini, kama kawaida, ukweli ni mgumu zaidi kuliko huo."Ukioga usiku, unakwenda kulala ukiwa msafi, lakini bado utatoka jasho usiku kucha," anasema Primrose Freestone, mwanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Leicester nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa Freestone, hata katika hali ya hewa ya baridi, mtu bado hutoka jasho hadi nusu lita kitandani na kuweka seli za ngozi 50,000 kuwa chakula cha wadudu wachafu."Bado utatoka jasho ambalo bakteria kwenye ngozi yako huchukua na kusababisha harufu ya mwili. Kwa hiyo, unapoamka asubuhi baada ya kuoga usiku, bado utasikia harufu kidogo, "Freestone anasema.
Faida za kuoga usiku huonekana tu ikiwa unafua mashuka mara kwa mara. "Pengine ni muhimu zaidi kuosha shuka zako kuliko kuoga usiku," anasema Holly Wilkinson, mhadhiri mkuu katika Uponyaji wa Jeraha na Microbiome katika Chuo Kikuu cha Hull nchini Uingereza.
"Kwa sababu ikiwa unaoga na kuacha shuka kwa muda wa mwezi mmoja, bakteria, uchafu na wadudu wa vumbi watakusanyika."
Hili huleta tatizo, kwani huongeza hatari ya mizio. Inawezekana pia kwamba kulala mara kwa mara na nguo chafu huongeza hatari ya maambukizo ya ngozi, ingawa ushahidi haujathibitishwa.
USINGIZI MNONO
Wapo wanaoamini kuwa kuoga usiku ndiko kulala vizuri usiku. Baadhi ya wafuasi wa kuoga nyakati za usiku wanasema kwamba huwasaidia kulala vizuri, na kuna ushahidi wa kuunga mkono hilo.Kwa mfano, uchanganuzi wa meta uliolinganisha matokeo ya tafiti 13 uligundua kuwa kuoga kwa dakika 10 na maji au kuoga saa moja hadi mbili kabla ya wakati wa kulala kulipunguza sana muda wa kupata usingizi, inasema BBC.
Inawezekana kwamba kuongeza joto la mwili kabla ya kupoa hutoa ishara kwa mwili kujiandaa kwa usingizi, ingawa utafiti zaidi unahitajika ili kuthibitisha hili. Kwa hiyo, pamoja na habari hii yote, tunawezaje kujibu swali la ikiwa ni bora kuoga asubuhi au usiku?
Freestone anapendelea kuoga asubuhi, kwa kuwa hii itaondoa jasho jingi na vijidudu vilivyokusanyika usiku mmoja kitandani, ili kumwezesha kuanza siku akiwa msafi. Inasema BBC.
MAONI MBADALA
Hata hivyo, mtandaoni, wapo wanaotofautiana na Freestone wa BBC, wakisema hakuna wakati "bora zaidi" wa kuoga, kwa kuwa muda unaofaa unategemea mapendekezo ya mtu mwenyewe na kile unachotaka kufikia, kama vile kuhisi umeburudishwa asubuhi au kupumzika jioni.
Kuingia bafuni kwa nyakati zote mbili iwe za asubuhi na jioni zina manufaa, kuoga asubuhi kunaweza kukusaidia kukuamsha na kuosha seli za ngozi usiku kucha, wakati kuingia bafuni jioni zinaweza kukusaidia kupumzika, kuupoza mwili kwa usingizi na kuondoa uchafu na jasho la siku nzima.
Zipo faida za kuoga asubuhi, kwanza inatia nguvu, kukufanya ujisikie umeburudishwa na mwenye nguvu kwa siku mpaka inayoanza.
Ukiingia bafuni asubuhi unasafisha na kuosha seli za ngozi zilizokufa ambazo zimekusanyika kwa usiku mmoja.
JIONI
Utulivu ni jambo la muhimu na kwa kuoga jioni kunaweza kukusaidia kupumzika na kufadhaika kutokana mambo magumu ya mchana kutwa. Hukuza usingizi, kuoga kwa maji ya moto saa moja hadi mbili kabla ya kulala kunaweza kusaidia kupunguza joto la mwili na kukusaidia kulala haraka.
Kuoga jioni kunasafisha uchafu, jasho,vumbi na nta za mchana kutwa lakini hutuliza misuli, maji ya joto yanaweza kusaidia kutuliza maumivu ya viungo na misuli na kupunguza mvutano wa mwili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED