Daraja la Uzi kuchochea hamasa ya maendeleo Zanzibar

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:50 PM Oct 21 2025
Daraja la Uzi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Daraja la Uzi.

Muonekano wa daraja linalounganisha Kisiwa cha Uzi na maeneo mengine ya Unguja unaendelea kuvutia wengi, huku kazi za ujenzi zikisonga mbele kwa kasi kubwa. Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 2.5 linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Mradi huo unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), na unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutalii kwa wakazi wa kisiwa hicho kilichopo Mkoa wa Kusini Unguja.

Kupitia daraja hilo, wakazi wa Uzi wataunganishwa kwa urahisi na maeneo mengine ya Unguja, jambo litakalorahisisha usafiri wa bidhaa, huduma na watu.

Aidha, daraja hilo linatarajiwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea eneo hilo kutokana na mandhari yake ya kipekee na urithi wa kitamaduni wa wenyeji wa Uzi, ambao ni kivutio cha kipekee visiwani Zanzibar.

Kukamilika kwa mradi huo kutakuwa hatua muhimu ya kihistoria kwa Zanzibar, ikiashiria dhamira ya serikali kuboresha miundombinu na kuleta maendeleo jumuishi na endelevu kwa wananchi wake.