Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Julius Kahabi, amewataka viongozi wa dini wilayani humo kusimama kidete katika kuhubiri amani wakati huu ambapo Taifa linajiandaa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza katika kikao maalum kilichowakutanisha viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wadau wa amani, Kanali Kahabi alisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na utulivu wa nchi.
Aidha, aliwahimiza wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akiwaonya vijana kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
“Ninawakemea vikali baadhi ya vijana wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza matusi na ujumbe usio na maadili dhidi ya viongozi. Hili halikubaliki,” alisema Kanali Kahabi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngara, William Solla, alionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayehusika na vitendo vya kuvuruga amani.
“Kosa la jinai halina ukomo. Watakaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa amani watachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisisitiza Kamanda Solla.
Solla pia aliwataka viongozi wa dini kuhakikisha ujumbe wa kulinda amani wanaoupokea katika kikao hicho unawafikia waumini wao, ili kwa pamoja waendelee kuilinda misingi ya amani nchini.
Naye Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Jasson Bahemu, alisisitiza kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba na siyo chanzo cha migogoro. Aliwataka Watanzania kuungana katika kudumisha amani, upendo, na mshikamano.
“Tuwakatae wote wenye nia ya kuchonganisha na kuvuruga amani ya nchi kwa kuhamasisha maandamano yenye madhara,” alisema Bahemu.
Viongozi wote wa dini waliohudhuria kikao hicho walikubaliana kwa pamoja kuendelea kuilinda amani ya nchi, na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge, na rais.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED