KUTOSOMANA kwa mifumo na majukumu ya baadhi ya taasisi za serikali kunatajwa kuwa chanzo kikuu cha mafuriko ya mara kwa mara katika eneo la Katubuka, Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambayo yamesababisha vifo, uharibifu wa makazi na kupotea kwa mali za wananchi.
Inaelezwa kuwa iwapo taasisi hizo zingeshirikiana ipasavyo katika kutekeleza utafiti uliokuwa umekwisha kufanyika, maafa hayo yangeweza kuepukika.
Uchunguzi wa Nipashe umebaini kwamba sekta mbalimbali za serikali, zikiwamo Bonde la Ziwa Tanganyika, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), Mipango Miji, na Ardhi, ziliamua kufanya utafiti wa pamoja baada ya madhara kutokea, badala ya kuchukua hatua za tahadhari mapema.
Cha kushangaza, kila taasisi ilikuwa tayari na utafiti wake wa awali ulioonesha hatari hiyo, jambo linalodhihirisha kuwapo pengo kubwa la mawasiliano na ushirikiano kati ya taasisi hizo.
Ofisa mmoja wa Bonde la Ziwa Tanganyika (ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa suala hilo bado liko katika utekelezaji), ameeleza kuwa taasisi zao mara nyingi huombwa taarifa za wingi wa maji baada ya madhara kutokea.
"Tumeshafanya utafiti kwa kushirikiana na taasisi nyingine. Lakini kinachotia wasiwasi ni kwamba matokeo haya yatatumika kutatua tatizo lililokwisha kutokea badala ya kuzuia maafa yajayo. Hii ni hatari," anasema ofisa huyo.
Anasema baadhi ya mamlaka zinapuuza matokeo ya tathmini za awali na kuendelea kutekeleza miradi bila kujali ushauri wa kitaalamu.
"Huwa ninashangaa kwanini hawazingatii utafiti tuliofanya. Labda ni kwa sababu mfadhili anataka mradi ufanyike kwenye eneo husika bila kujali hatari zake. Ni muhimu taasisi zetu kushirikiana kwa dhati,
maana uharibifu unaanzia kwenye uzembe wetu," anaongeza.
Mwezi Aprili 2025, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), James Yonaz, aliitaka NEMC na taasisi nyingine za serikali kuongeza ushirikiano katika kushughulikia changamoto za kimazingira.
Meneja wa NEMC Kanda ya Magharibi, Edga Mgira, anakiri kuwa miradi mingi nchini hufanyiwa tathmini ya mazingira baada ya utekelezaji kuanza, jambo linalochangia madhara kama yaliyotokea Katubuka.
"Katubuka ni eneo oevu, linahifadhi maji. Hivyo, maji yanaporudi kwenye eneo lake la asili husababisha mafuriko. Inaweza kutokea hata baada ya miaka 30.
"Utafiti wetu unaonesha wazi kuwa kabla ya mradi wowote kufanyika, tathmini ya mazingira inapaswa kushirikisha sekta zote husika," anasema Mgira.
Anabainisha zaidi kuwa uvamizi wa binadamu katika eneo la mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji ni kinyume cha sheria. Umeharibu asili ya eneo hilo na hivyo kuchochea mafuriko.
Kanuni za Mipango Miji za mwaka 2018, kifungu cha 89, zinaelekeza halmashauri kushirikiana kupanga matumizi ya ardhi na miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa utekelezaji vifungu hivyo, kikiwamo Kifungu cha 8(1) na 24(1) cha Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007, umekuwa hafifu katika maeneo kama Katubuka.
Vibali vya ujenzi vimetolewa bila kufuata taratibu za kisheria, bila tathmini za mazingira na bila kufanyika kwa ushirikishwaji wananchi kama inavyotakiwa. Matokeo yake, ujenzi holela umefanyika juu ya eneo la bwawa la asili linalokusanya maji ya mvua.
Kanuni hizo pia zinatoa mamlaka kwa sekta ya ardhi kutoa onyo, adhabu au kubomoa majengo yasiyo na vibali, au kutoza faini hadi Sh. 300,000. Lakini katika tukio la Katubuka, hakuna rekodi yoyote inayoonesha adhabu kutolewa kwa wakazi waliojenga kiholela.
HAKUNA ONYO
Wananchi wengi wa Katubuka wanasema hawakuwahi kupewa tahadhari kuhusu hatari za eneo hilo, wala kushirikishwa katika tathmini za mazingira.
Sarafina Kaishozi, mkazi wa Kagashe Road, anasema alipata ramani na kibali cha ujenzi bila kupewa maelekezo yoyote kuhusu vizuizi vya matumizi ya ardhi au hatari za mafuriko katika eneo hilo.
"Ramani yangu ilikuwa safi kabisa, nikadhani eneo ni salama. Sikujua kama ni bwawa la asili," anasema.
Halima Bandua, mkazi wa Katubuka kwa miaka 30, naye anasema hakuwahi kusikia tangazo lolote kuhusu hatari hiyo. "Tuliona watu wanajenga kila siku, tukafikiri ni salama. Serikali ingeonya mapema," anasema.
Ally Shabani anaamini kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa kwa nia ya serikali kujipatia mapato, bila kuzingatia tathmini ya mazingira. "Mifereji iliyochimbwa barabarani haikupangwa vizuri, ikawa inapeleka maji majumbani," anasema.
UTAFITI WA ARU
Utafiti wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wa mwaka 2021 unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 65 ya wakazi wa miji midogo nchini hujenga bila vibali, kutokana na rushwa na kukosa elimu kuhusu sheria za ujenzi.
Tatizo hili, kwa mujibu wa wataalamu, limekuwa sugu kwa sababu baadhi ya viongozi wa kisiasa
wanahofia kupoteza uungwaji mkono endapo watasisitiza utekelezaji mkali wa sheria.
Diwani wa Katubuka, Moshi Mayengo, anakiri kuwa hakukuwa na tathmini ya mazingira kwa wananchi waliouziwa viwanja.
"Wengi waliridhika na vibali kutoka idara ya ardhi tu. Ninashauri wananchi waulize wenyeji kabla ya kununua viwanja, kwani hatari nyingine haziandikwi kwenye karatasi," anasema.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Kisena Mabuba, anasema maafa ya Katubuka yamekuwa funzo kubwa kwa serikali.
"Kuanzia sasa, kabla ya kutekeleza mradi wowote, tutafanya utafiti wa kina ili kuepuka makosa yaliyotokea. Pia tunawahimiza wananchi kutunza mazingira, hasa kwenye maeneo yenye maporomoko," anasema.
*ITAENDELEA KESHO...
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED