DC Nyamwese: Hakuna mwananchi atakayebugudhiwa siku ya kupiga kura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:37 AM Oct 20 2025
DC Nyamwese: Hakuna mwananchi atakayebugudhiwa siku ya kupiga kura
Picha: Mpigapicha Wetu
DC Nyamwese: Hakuna mwananchi atakayebugudhiwa siku ya kupiga kura

Halmashauri ya Mji wa Handeni imefanya bonanza kubwa la michezo lililolenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Bonanza hilo limefanyika leo katika Uwanja wa Kigoda, Handeni, na limehusisha wananchi,  watumishi wa umma, viongozi wa dini, viongozi wa kisiasa na taasisi binafsi.

Akizungumza katika bonanza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amewahimiza wananchi wote waliojiandikisha kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.

 “Nawasihi wananchi wote wa Handeni kujitokeza mapema siku ya uchaguzi. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Serikali imeimarisha ulinzi na usalama, hivyo kila mmoja atapiga kura kwa amani na utulivu kama tulivyoshiriki bonanza letu leo, hakuna mwananchi atakayebugudhi," amesema Nyamwese.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Maryam Ukwaju, amesema lengo la Bonanza ni kuhakikisha wananchi wanajitokeza Oktoba 29, 2025 kutimiza haki yao kikatiba.