Uongozi wa Klabu ya Simba SC umethibitisha kuwa kikosi chao kipo tayari kwa pambano la marudiano dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika utakaochezwa Oktoba 26, mwaka huu, majira ya saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mashabiki wataruhusiwa kuhudhuria.
Akizungumza leo Makao Makuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema baada ya kurejea kutoka Eswatini, wachezaji walipewa mapumziko mafupi kabla ya kurejea mazoezini leo (Jumatano) kuanza maandalizi rasmi kwa mchezo huo muhimu.
“Baada ya kuwasili kutoka Eswatini tuliwapa mapumziko mafupi wachezaji wetu, na leo tunaanza mazoezi rasmi kujiandaa na mchezo huo ambao hatuwezi kuubeza hata kidogo,” amesema Ally.
Ahmed Ally ameongeza kuwa Kocha Msaidizi Selemani Matola atarejea kwenye benchi la ufundi baada ya kumaliza adhabu yake, huku Alassane Kanté akitarajiwa kuungana na wenzake baada ya kupona majeraha.
Kuhusu mlinda mlango Moussa Camara, ambaye hakushiriki mchezo wa kwanza, Ahmed amesema tayari amerejea kutoka Guinea na anasubiri kufanyiwa vipimo na madaktari wa timu ili kubaini aina ya matibabu anayohitaji.
“Camara amerudi na madaktari watafanya vipimo kujua hali yake. Kwa upande wa Mohamed Bajaber, yeye ameshaanza mazoezi muda mrefu, ni uamuzi wa Meneja Mkuu kuona kama ataingizwa kwenye kikosi,” amesema.
Aidha, Ahmed Ally amekemea vikali tabia za mashabiki wanaoingia uwanjani na kuwasha baruti au moto wenye moshi, akisema kitendo hicho kiliisababishia Simba kucheza mchezo uliopita bila mashabiki, jambo lililoathiri morali ya timu.
“Hatutasita kuchukua hatua kali. Wengine si mashabiki wa Simba bali wanakuja makusudi kufanya vitendo vinavyoharibu taswira ya klabu,” amesisitiza.
Akitaja viingilio vya mchezo huo, Ahmed amesema:
Ameongeza kuwa tiketi zimeanza kuuzwa jana, akiwataka mashabiki kununua mapema ili kuepuka usumbufu siku ya mchezo.
Pia amebainisha kuwa mchezo huo utatumika kumtambulisha rasmi Meneja Mkuu mpya wa klabu, Dimiter Pantev, chini ya kauli mbiu “Hatujaridhika, Tunataka Zaidi.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED