Mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir, ameahidi kufuata nyayo za waasisi wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, endapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika mkutano wake wa kuonana na watoto yatima wanaolelewa katika nyumba za kulelea watoto zilizopo Kibele na Kitumba, Mkoa wa Kusini Unguja, mgombea huyo alisema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya kampeni zake na pia ni ishara ya kujali makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.
Amesema falsafa na maadili ya Nyerere na Karume ndiyo dira pekee inayoweza kurejesha misingi ya umoja, usawa na maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
“Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walituachia urithi wa heshima, utu, uzalendo na uchapakazi. Mimi nitaendeleza misingi hiyo kwa vitendo, kwa kuhakikisha Zanzibar inakuwa na uchumi imara unaowanufaisha wananchi wote,” alisema Ameir.
Aliongeza kuwa serikali yake itatoa kipaumbele katika sekta za elimu, kilimo, uvuvi, afya na ajira kwa vijana, akisisitiza kuwa hayo ndiyo maeneo yaliyokuwa kiini cha sera za waasisi hao wa taifa.
“Nitahakikisha kila kijana ana nafasi ya kujitengenezea maisha, kila mtoto anapata elimu bora, na kila mwananchi ananufaika na rasilimali za nchi. Hayo ndiyo maono ya Nyerere na Karume na ndiyo njia nitakayoifuata,” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi wa Zanzibar kufanya siasa safi zenye hoja na sera zenye maslahi ya taifa, badala ya siasa za matusi na chuki.
“Siasa safi ndiyo silaha ya maendeleo. Tuachane na siasa za kugawanya watu. Umoja wetu ndiyo nguvu yetu,” alisisitiza Ameir.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED