Uongozi wa Klabu ya Yanga umethibitisha kuwa mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers hautakuwa na kiingilio, na hivyo mashabiki wote wataingia bure kushuhudia pambano hilo litakalochezwa Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Msemaji wa Klabu hiyo, Ally Kamwe, amesema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya Kamati ya Utendaji kupitia maombi ya wanachama na viongozi wa matawi waliopendekeza mechi hiyo iwe bure ili kila mwanachama apate fursa ya kuishangilia timu yao.
“Uongozi umepitia hoja na maombi ya wanachama wetu, na umepitisha kwamba maeneo yote yatakuwa bure isipokuwa majukwaa ya VIP A na B ambayo yatakaliwa na watu maalum,” amesema Kamwe.
Amesema hoja hiyo imelenga kujaza uwanja, kuipa nguvu timu yao na kuhakikisha wanafanikiwa kufika hatua ya makundi.
Katika hatua nyingine, Kamwe amesema mchakato wa kumpata kocha mpya unaendelea vizuri, na ndani ya siku tatu zijazo kocha huyo atakuwa amewasili nchini.
“Mchakato wa kumpata kocha mpya unaendelea vizuri. Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, ndani ya siku tatu zijazo atakuwa amepatikana,” amesema.
Kwa sasa, timu itaendelea kuongozwa na Kocha Msaidizi Patrick Mabedi, ambaye amewahi kupata mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi.
Amesema pia mchezaji Clement Mzize ameimarika kiafya kwa asilimia 100 na ana nafasi kubwa ya kuwamo kwenye kikosi kitakachocheza Jumamosi.
Kamwe ameongeza kuwa maandalizi yanaendelea vizuri huku kikosi kikiweka nguvu kuhakikisha kinapata matokeo mazuri na kufanikiwa kutinga hatua ya makundi.
Aidha, amethibitisha kuwa wapinzani wao, Silver Strikers, watawasili nchini Alhamisi majira ya saa mbili usiku kwa ajili ya mchezo huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED