“KAMA mtu mwenye matumaini na sio aliyekata tamaa, ujumbe wangu ni Afrika inahitaji kutumia rasilimali zake kushughulikia miundombinu ya usafirishaji,” alisema Raila Odinga, Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu Afrika (The High Representative for Infrastructure Development in Africa).
Raila Mhandisi kitaaluma akifanya kazi na Umoja wa Afrika (AU), ni championi wa miundombinu Afrika alitaka kujengwa viunganishi Afrika Mtandao wa Barabara Kuu za Afrika Great North Road na Mtandao wa Reli ya Kasi Trans Africa Railways inayounganisha miji mikuu yote ya bara hili miradi miwili muhimu ya kimiundombinu ya Agenda 2063 ya The Afrika We Want.
Odinga ilianza kazi ya kuimarisha miradi ya miundombinu Tume ya Umoja wa Afrika na Shirika la NEPAD, kwenye Mpango wa Maendeleo ya Miundombinu Afrika - Programme for Infrastructure Development in Africa (PIDA).
Odinga (81), ameondoka duniani na kuacha pengo kubwa ambalo wachambuzi wa uongozi na siasa wanasema haliwezi kuzibwa si tu katika siasa za Kenya, bali Afrika. Mwanamapinduzi huyo akifariki wiki iliyopita Oktoba 15, akiwa India kwa matibabu.
Viongozi, watawala, wanasiasa na wachambuzi wa siasa wanakubaliana kuwa Raila alikuwa zaidi ya mwanasiasa, mtu mwenye sauti ya matumaini, nembo ya mapambano, na alama ya uthubutu wa kweli katika kizazi chake na tegemeo la Afrika.
Kwa miongo kadhaa, Raila alisimama kidete kama mtetezi wa demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria lakini mwenye kutamani Afrika mpya iliyoendelea na inayojisimamia. Katika misingi hii, alikumbatia maumivu, akavumilia mateso na hata kufungwa jela kwa miaka mingi kuliko kiongozi mwingine yeyote wa upinzani katika Kenya huru yote kwa ajili ya taifa alilolipenda kwa dhati.
“Raila hakuwa mwanasiasa wa kawaida. Alijitokeza kama nguzo kuu ya upinzani dhidi ya tawala dhalimu, akichochea mageuzi ambayo hatimaye yalizaa Katiba ya 2010 mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya kisiasa nchini Kenya. Ujasiri wake ulimletea majina mengi ya heshima kutoka kwa wananchi na viongozi wa kimataifa,” asema mchambuzi wa siasa James Obwaka.
Wengi walimwita‘Baba wa Demokrasia ya Kisasa Kenya’, huku wengine wakimwita ‘Tinga’ jina lililoashiria nguvu na msimamo wake usioyumbayumba. Wafuasi wake waaminifu walimwita kwa upendo ‘Jakom’ na ‘Agwambo’ majina ya Kijaluo yanayomaanisha mtu mwenye uwezo wa ajabu au wa kipekee.
Kwa Wakenya, Raila alikuwa mfano wa uthabiti mtu ambaye hakuchoka kudai haki, hata alipokataliwa, kudhulumiwa, au kunyamazishwa. Aliitisha maandamano na kuingia barabarani kuyaongoza na mara kadhaa alikubali kuwa kiongozi wa upinzani kwa heshima bila kushiriki katika mifumo aliyohisi haikuwa ya haki. Katika uhai wake, Raila alifichua kashfa nyingi kubwa zilizotikisa serikali na alisimama kidete kuhoji matumizi ya fedha za umma.
Msimamo wake dhidi ya ufisadi ulimweka kwenye mgongano na watawala, lakini pia ulimfanya kuwa shujaa wa umma. Alijulikana kwa kutoa matamshi makali dhidi ya wizi wa mali ya umma na aliamini kuwa hakuna taifa linaweza kustawi ikiwa viongozi hawawajibiki. Nje ya Kenya, Raila alikuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika. Kama Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu miundombinu, alitembea mataifa mengi kutafuta ushirikiano wa kimaendeleo na kuhimiza uunganishaji wa Afrika kupitia miundombinu ya kisasa.
Katika majukwaa ya kimataifa, sauti yake ilikuwa ya kipekee, ya kiongozi aliyeelewa changamoto za Afrika lakini pia mwenye maono ya kuivusha katika enzi mpya.Kwa sababu hiyo, aliheshimiwa kama ‘Simba wa Afrika’, mtu ambaye alibeba maono ya bara zima kwenye mabega yake. Raila ameacha urithi mkubwa ambao utadumu vizazi vingi: Mfano alipigania uchaguzi huru na wa haki, alitetea haki za jamii zilizopuuzwa, aliongoza juhudi za maridhiano ya kitaifa kupitia handisheki zake na waliokuwa wapinzani wake na aliwaonesha vijana kuwa siasa si lazima iwe ya ubinafsi bali ya huduma kwa umma.
Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, anamtaja Raila kama “mwanasiasa mashuhuri wa Afrika” na “Mwana wa Afrika aliyejawa na maono.”
“Raila Odinga alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya na alikuwa mtetezi thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia maslahi ya wananchi,” alisema Youssouf. “Dhamira yake ya miongo mingi ya kupigania haki, mfumo wa vyama vingi, na mageuzi ya kidemokrasia imeacha alama isiyofutika si tu Kenya, bali kote barani Afrika. Ujasiri wake, uvumilivu, na imani yake katika mazungumzo na taasisi za kidemokrasia uliwavutia viongozi wengi, mimi nikiwa mmoja wao.”
“Akiwa Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika, Raila alifanya kazi kwa bidii kuendeleza ajenda ya kuunganisha bara kimiundombinu na kuimarisha ushirikiano barani, juhudi zilizowezesha misingi ya Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) na mageuzi ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla. Afrika imepoteza mmoja wa wana wake waliokuwa na maono ya kina kiongozi aliyejitolea maisha yake kwa haki, demokrasia na mshikamano,” alisema Youssouf, akiongeza kuwa urithi wake utaishi kwa vizazi vingi vijavyo.
Katika maisha yake, Raila alichukiwa na wengi, lakini aliheshimiwa hata na maadui wake wa kisiasa. Leo, baada ya kuondoka duniani, dunia inakubali kuwa hakika alisimama upande wa haki. Pengo aliloacha Raila haliwezi kupimwa kwa maneno au takwimu. Ni pengo la maono, ujasiri, na sauti isiyoogopa kusema ukweli. Kenya na Afrika zimempoteza mpiganiaji wa haki, shujaa wa demokrasia na kinara wa matumaini,” anasema mchambuzi wa siasa Dk. Isaac Gichuki
Kaka yake Dk. Oburu Odinga, aliyeteuliwa Kaimu Kiongozi wa chama cha ODM cha Raila, alikiri hawezi kujaza pengo aliloacha mdogo wake. Anasema: “Nataka kushukuru chama changu, ODM, kwa kuniteua kuwa kiongozi wa chama. Ingawa viatu vya Raila ni vikubwa mno kunitosha, ninachotaka ni kujitahidi kadri ya uwezo wangu. Nitajitahidi,” Oburu anasema Ijumaa iliyopita wakati wa ibada ya kitaifa ya Raila katika uwanja wa Nyayo.
OBAMA ANAMKUMBUKA
Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama, anaandika ujumbe wa kumwomboleza aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga
baada ya presha kubwa kutoka kwa Wakenya mitandaoni, waliomkosoa kwa kukaa kimya kuhusu kifo cha mtu aliyekuwa na uhusiano wa karibu na familia yake na ambaye alitoka katika eneo linatambulika kama chimbuko la Obama kwenye kaunti ya Siaya.
Kupitia akaunti yake rasmi ya X (zamani Twitter) Jumamosi iliyopita Obama aliandika: “Raila Odinga alikuwa shujaa wa kweli wa demokrasia. Alizaliwa wakati wa uhuru, na aliteseka kwa miongo kadhaa akipigania haki ya kujitawala na uhuru wa watu wa Kenya. Mara kwa mara nilimwona akiweka maslahi ya nchi mbele,” aliandika Obama.
Anamsifu kama kiongozi wa maridhiano aliyeonesha mfano wa msamaha bila kupoteza maadili yake ya msingi.“Kama viongozi wachache sana duniani, alikuwa tayari kuchagua njia ya amani na maridhiano bila kuisaliti misimamo yake. Maisha ya Raila Odinga yalikuwa somo kwa Kenya na bara zima la Afrika, na dunia nzima. Nitamkosa sana,” anasema Rais wa zamani.
Katika hitimisho la ujumbe wake, Obama anatuma rambirambi kwa familia ya Odinga na kwa watu wa Kenya, kwa niaba yake na mkewe, Mama Michelle Obama.Hata hivyo, japo ujumbe huo ulipokewa kwa furaha na shukrani na wengi, unajiri baada ya malalamishi mengi mitandaoni kutoka kwa Wakenya waliotaka Obama aoneshe msimamo mapema, wakimkumbusha uhusiano wa muda mrefu aliokuwa nao na Raila na jamii ya Luo.
Obama na Raila wana historia na urafiki wa karibu wa kifamilia uliodumu kwa miaka mingi. Wote wawili wana asili ya Kaunti ya Siaya, na waliwahi kuonekana pamoja katika hafla kadhaa kabla na baada ya Obama kuwa Rais wa Amerika mwaka 2008. Katika hotuba zake za awali, Obama amewahi kumtaja Raila kama ‘mnara wa matumaini kwa mustakabali wa kidemokrasia wa Afrika.
AU/TAIFA LEO
PICHA
kutoka Madagascar. Ushindi ulikwenda Madagascar. PICHA: MTANDAO
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED