Waziri wa zamani wa Masuala ya Uchumi na Usalama wa Taifa nchini Japan, Sanae Takaichi, ameandika historia baada ya kushinda kura ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke kuwahi kutokea nchini humo.
Takaichi, mwenye umri wa miaka 64, ambaye ni kiongozi wa Chama cha Liberal Democratic Party (LDP), alipata ushindi katika uchaguzi uliofanyika mapema leo, Oktoba 21, 2025, ikiwa ni jaribio lake la tatu kuwania nafasi hiyo ya juu serikalini.
Kura hiyo ilipigwa na wabunge wa Bunge la Japan, na si kura ya wananchi wote, kama ilivyo utaratibu wa kikatiba wa nchi hiyo.
Baada ya ushindi huo, macho ya dunia sasa yameelekezwa kwake, wengi wakisubiri kuona jinsi atakavyokabiliana na changamoto kuu zinazolikabili taifa hilo — zikiwemo uchumi dhaifu, uhusiano tete na Marekani siku chache kabla ya ziara ya Rais Donald Trump, na mivutano ya ndani ya chama tawala (LDP) iliyosababishwa na kashfa na migogoro ya kisiasa.
Takaichi, anayejulikana kwa upendo wake kwa muziki wa ngoma nzito na pikipiki aina ya Kawasaki, alizaliwa na kukulia katika eneo la Nara, karibu na jiji la Osaka.
Akitoka katika kundi la kisiasa lililokuwa likimuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe, ambaye aliuawa mwaka 2022, Takaichi amekuwa mrithi wa sera za kihafidhina za Abe. Kama mtangulizi wake, ameonyesha wazi dhamira ya kurekebisha katiba ya Japan inayopinga matumizi ya kijeshi, na amewahi kutembelea madhabahu yenye utata ya vita, inayohusisha majina ya wale waliopatikana na hatia ya uhalifu wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia — jambo linalozua mashaka na hasira kutoka China na Korea Kusini, washirika muhimu wa kibiashara wa Japan.
Kwa ushindi huu, Sanae Takaichi anaingia katika historia kama ishara mpya ya mabadiliko ya kijinsia katika siasa za Japan, huku akibeba matumaini na changamoto za kizazi kipya cha viongozi wa Asia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED