TANZANIA imeibuka kuwa kinara wa kimataifa katika sekta ya korosho, ikiongoza wito wa pamoja wa Afrika wa kusitisha mauzo ya korosho ghafi na kuwekeza kwenye uchakataji wa ndani ili kuongeza thamani. Wito huo wa kimkakati unatarajiwa kuidhinishwa rasmi kama “Azimio la Tanzania” na utakuwa ajenda muhimu ya Mkutano wa Korosho Afrika 2025, unaotarajiwa kufanyika mjini Mtwara mwezi ujao.
Takwimu za Bodi ya Korosho (CBT) za mwaka jana zinaonesha ongezeko kubwa la uzalishaji katika misimu miwili mfululizo mwaka 2023/24 zilipatikana tani 310,000 wakati uliofuata 2024/25 zilikuwa zaidi ya tani 528,000 kiwango cha juu zaidi katika historia ya taifa na Afrika pia.
Zaidi ya kaya takriban 700,000 sawa na Watanzania milioni 2.5 wanategemea zao hili kwa kipato cha moja kwa moja. Tasnia ya korosho sasa inachangia zaidi ya Dola za Marekani milioni 400 kwa mwaka katika mapato ya fedha za kigeni, ikiwa ni mchango muhimu wa pili baada ya tumbaku katika mauzo ya kilimo yanayouzwa nje ya nchi. Ubora wa kipekee wa korosho za Mtwara na Lindi unaipa Tanzania hadhi ya kipekee na takribani asilimia 90 ya korosho hulimwa kiasili, bila mbolea za viwandani, jambo linaloendana na matakwa ya wateja wa kimataifa wanaothamini bidhaa asilia na salama kiafya.
Afrika inazalisha zaidi ya asilimia 55 ya korosho ghafi duniani, lakini inachakata chini ya asilimia 15 ya mazao yake. Hali hii inasababisha hasara kubwa ya mapato. Kilo moja ya korosho ghafi huuzwa takribani Dola 1.20 hadi 1.50, ilhali korosho iliyosindikwa hufikia bei ya hadi Dola 10 hadi 12 katika masoko ya Ulaya, Asia na Amerika Kaskazini kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) ya mwaka 2024.
Nchi kama Vietnam na India wanunuzi wakuu wa korosho za Kiafrika ndizo wanufaika wakuu wa thamani ya uchakataji, wakipata faida mara nyingi zaidi ya wakulima na wachuuzi wa Kiafrika. Ripoti za Benki ya Dunia zinaonesha kwamba iwapo Afrika ingechakata hata nusu ya mazao yake,lingeweza kupata zaidi ya Dola za Marekani bilioni tatu mpaka nne kila mwaka kama mapato ya ziada.
Soko la dunia la korosho linaendelea kukua kwa kasi, likitarajiwa kufikia thamani ya zaidi ya Dola bilioni 15 kufikia mwaka 2030, likichochewa na ongezeko la ulaji wa vitafunwa vyenye protini nyingi na bidhaa mbadala za mazingira.
AZIMIO LA TANZANIA
Wito kwa bara zima, unasikika katika mkutano wa Mtwara, viongozi wa serikali, wakulima, wawekezaji na wadau wa kimataifa wanatarajiwa kujadili na kuidhinisha hatua zifuatazo za kimapinduzi na kikubwa ni kusitisha mauzo ya korosho ghafi kufikia 2027 Afrika nzima kuzuia usafirishaji wa korosho ghafi ili kuchochea ujenzi wa viwanda vya ndani.
Alama za kijiografia na hati miliki ni lazima ziwepo ili kulinda chapa na asili ya korosho kama Korosho za Mtwara ili kuongeza thamani, kuzuia uporaji wa maarifa na kudumisha ubora.
Sekretarieti ya kimataifa ya korosho Afrika inataka kuanzishwa Mtwara kama kitovu cha utafiti, sera na ubunifu na kuufanya mji huu kuwa “Davos ya Korosho.” Lakini pia kuweka Makumbusho na Kituo cha Utafiti wa Korosho ili kuhifadhi urithi wa korosho na kuendeleza teknolojia rafiki kwa tabianchi na mbinu za kilimo endelevu. Jingine ni kuhakikisha uwapo wa Wiki na Siku ya Korosho Afrika Septemba 18 kila mwaka ili kuimarisha uhamasishaji, biashara, ubunifu na mshikamano wa bara zima.
KIUCHUMI/ MAZINGIRA
Sekta ya kuchakata korosho inaakisiwa kutoa mamilioni ya ajira za kijani, hususan kwa wanawake na vijana, na kuchangia zaidi ya Dola bilioni tatu mpaka nne kwa mwaka ikiwa angalau nusu ya korosho za Afrika zitachakatwa nyumbani. Viwanda vya ndani vitapunguza utegemezi wa masoko ya ghafi na kuongeza mapato ya kigeni, huku vikichochea ukuaji wa sekta za usafirishaji, vifungashio na teknolojia.
Mikoko ya mikorosho ni zao linalostahimili ukame, linaongeza uhifadhi wa kaboni na linasaidia kurejesha ardhi iliyoharibika, hivyo kuwa muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Wataalamu wa mazingira wanasema ongezeko la mashamba ya mikorosho linaendana moja kwa moja na mikakati ya Afrika ya kufikia malengo ya net-zero.
Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Tanzania inalenga si tu kuongeza uzalishaji, bali pia kuifanya nchi kuwa kitovu cha uchakataji na biashara ya kimataifa ya korosho.
Serikali imeanzisha sera za kuhamasisha uwekezaji, kutoa mikopo kwa wakulima, na kuboresha miundombinu ya bandari na barabara ili kupunguza gharama za usafirishaji na muhimu pia kampuni binafsi na mashirika ya maendeleo yashirikiane kuanzisha viwanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED