Angalizo kitaalamu watoto wasishiriki mikutano ya kampeni za kisiasa

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 04:52 PM Oct 21 2025
Watoto wakiwa sehemu ya washiriki wa mikutano ya kampeni ni jambo linalopingwa na wataalamu
Picha: Rahma Suleiman
Watoto wakiwa sehemu ya washiriki wa mikutano ya kampeni ni jambo linalopingwa na wataalamu

WAKATI harakati za kampeni za vyama vya siasa kunadi sera na kutangaza ilani zikielekea ukingoni ili kupiga kura Jumatano ijayo na kuhitimisha Uchaguzi Mkuu 2025, vyombo vinavyosimamia uchaguzi pamoja na taasisi zinazohusika na ustawi wa watoto wakati umefika ziandae sheria ya kuzuia watoto wasishiriki wala kupelekwa kwenye kampeni.

Baadhi ya wazazi, walezi na wanasiasa huwapeleka watoto katika mikutano hiyo, jambo linaloweza kuonekana kama la kawaida, lakini ukweli ni kwamba lina madhara makubwa kwa ustawi wao, malezi pamoja na haki za msingi, ndiyo maana wakati kampeni zinapoishia kuna haja kuandaa sheria za kudhibiti kupeleka watoto kwenye mikutano hiyo kwenye chaguzi ndogo na kubwa.

Mikutano ya kampeni mara nyingi hufanyika kwenye msongamano na mikusanyiko ambayo watoto wanaposhirikishwa hukabiliwa na hatari za kukanyagwa au kujeruhiwa kutokana na vurugu au msongamano na hata kukandamizwa na kukosa pumzi. Mkuu wa kitengo cha elimu ya afya Wizara ya Afya Zanzibar, Bakari Hamad Magarawa, anasema  ni kosa kuwapeleka viwanjani kwenye kampeni kwa  sababu kuna hatari ya watoto kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na kukaa katika maeneo yasiyo salama kiafya.

Anasema watoto ni rahisi kupata changamoto za kiafya na unapowachukua katika mikusanyiko ya watu huenda wakapata magonjwa ya kuambukiza hivyo si vyema kuwashirikisha katika mihemko ya kisiasa. Anaongeza: “Kwenye matukio kama hayo pia kuna hatari ya watoto kukumbana na udhalilishaji unaoweza kuwaathiri kisaikolojia, kihisia na kimwili, ni vyema kuwaelekeza zaidi katika kupata elimu, maarifa na kuwakinga na makundi ambayo yanaweza kuwasababishia athari za kiafya, elimu na ukuaji.”

ATHARI  KISAIKOLOJIA

Mtalamu wa masuala ya saikolojia Asha Khamis, anasema watoto wanaposhuhudia vurugu, matusi, au maneno ya chuki katika kampeni, akili zao changa huathirika na hata kuharibika kwa kupokea mambo ambayo siyo, hali hiyo inaweza kusababisha hofu na msongo wa mawazo na kuiga lugha au mienendo isiyofaa ya kisiasa, pia kupoteza dira ya malezi ya kimaadili kwa kushuhudia mifano mibaya.

Lugha kali, muziki wa kishindo, kelele na maneno ya kuchochea chuki, kejeli na mara nyingi hutawala majukwaa ya kisiasa, hali hiyo inaweza kuwaathiri kisaikolojia watoto ambao wanajifunza misingi ya maadili na heshima. Mikutano ya kampeni mara nyingi hufanyika wakati wa masomo hivyo watoto wanaposhiriki badala ya kuwapo shuleni, hupoteza muda muhimu wa kujifunza wakienda kwenye viwanja vya kampeni.

Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Fatma Mide anasema haipendezi watoto kushirikishwa katika mikutano ya hadhara na watoto wabaki kupata elimu na siasa kuwaachia wanasiasa anashauri zaidi: “Hatua tunazozichukua kuhakikisha watoto hawashiriki katika heka heka za kampeni huzungumza na wanajamii kupitia kamati za shule kuhakikisha kuwa wanasimamia usalama wa watoto,” anasema.

Anasema lazima kila mzazi na mlezi kuwa mlezi kwa watoto wake na wawenzake na kuhakikisha wanawahimiza kusimamia masomo yao ili kuwajengea mustakabali mwema wa baadaye, akifafanua kuwa wizara inafanya jitihada hasa kipindi hiki kuwalinda watoto na kuhakikisha wanapata elimu bora ambayo ndiyo haki yao ya msingi. Aidha, anasema watoto kukatizwa masomo husababisha kushuka kiwango cha ufaulu na kuathiri ndoto zao za baadaye.

HUATHIRI MAKUZI 

Mtaalamu wa masuala ya makuzi kwa watoto, Sharifa Suleiman Majid, anasisitiza jukumu la ulinzi wa watoto akisema si la serikali pekee bali ni wajibu wa kila mmoja kwa sababu wanahitaji uangalizi wa karibu na kulelewa katika mazingira salama ya upendo na yenye fursa za maendeleo hivyo si vyema watoto kuwashirkisha katika mikutano ya kampeni ambapo kunaweza kumsababishia madhara ikiwamo ya kiakili au ya kisaikolojia au kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji.

Sharifa anafafanua kuwa wanahitaji mapenzi na uangalizi ili kuwajenga akili na kuwa na taifa bora linalojenga utu na upendo, mtoto anapopata malezi ya pamoja yenye upendo unamjengea mazingira bora ya badaye ili wawe baba au mama bora miaka ijayo, pamoja na hayo wanahitaji ulinzi ili kuwakinga na majanga mbalimbali vikiwamo vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na ukatili na kuitaka jamii kujifunza ya kwamba mtoto anahitaji ulinzi muda wote ili kuwakinga na mambo maovu ambayo yanaweza kukatisha uhai wao, utu  na ndoto zao.

Baadhi ya wanasiasa huwatumia watoto kama chombo cha kutafuta kura kwa kuwavalisha sare za vyama vya siasa, kuwashika mikononi au kuwapandisha katika majukwaa ya kisiasa lakini watetezi wa haki za watoto wanasema hiyo ni aina ya unyonyaji wa watoto na ni kinyume na haki zao zilizowekwa na mikataba ya kimataifa pamoja na sheria za kitaifa za ulinzi wa mtoto.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Onesmo Olengurumwa, anasema watoto wanapohusishwa katika kampeni, huanza kuingia katika migawanyiko ya kisiasa mapema na kuongeza: “Hili linaweza kupandikiza chuki, ubaguzi na mtazamo finyu katika akili zao, jambo ambalo si sahihi kwa malezi ya kizazi chenye mshikamano wa kijamii.”

Aidha jamii, wazazi, walezi na viongozi wa kisiasa wana wajibu wa kuhakikisha kuwa haki za watoto zinalindwa na kwamba hawatumiki kama nyenzo katika mapambano ya kisiasa. Kuwashirikisha watoto katika mikutano ya kampeni za uchaguzi ni kinyume na maslahi yao bora na watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya mazingira hatarishi na kupatiwa nafasi ya kukua katika mazingira salama, yenye elimu bora na malezi ya kimaadili.

NINI KIFANYIKE

Dk.Mzuri Issa Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA)  Zanzibar, anasema kuwadhibiti watoto wasijihusishe katika mikutano ya kampeni ni njia ya kulinda haki zao za msingi kama zilivyoainishwa na Mkataba wa Haki za Mtoto wa Umoja wa Mataifa (CRC) na sheria za kitaifa. Anasema hatua hiyo inalinda usalama, afya, utu na maendeleo yao na pia inalenga kuhakikisha kwamba watoto hawageuzwi kuwa nyenzo za kisiasa bali wanalelewa katika mazingira salama na yenye kuzingatia maslahi yao.

Kwa ujumla wadau na wanashauri wanasisitiza elimu kwa wazazi na walezi, jamii kuhusu madhara ya kuwaingiza watoto katika mikusanyiko ya kisiasa na wajibu wao wa kuhakikisha watoto wanabaki salama nyumbani au maeneo salama.Kanuni na Sera za Uchaguzi, Tume za Uchaguzi Bara na Zanzibar na vyama vya siasa vinapaswa kuweka miongozo na sheria zinazokataza waziwazi ushiriki wa watoto kwenye mikutano ya kampeni.

Ushirikishwaji wa vyombo vya habari ili viwe mstari wa mbele kuelimisha jamii na kuonyesha mfano bora kwa kuepuka kurusha picha zinazohusisha watoto kama nyenzo za kisiasa, ni jambo linalohitaji kufanyiwa kazi.

Yote yaende pamoja na kuwapa ulinzi kisheria ambalo ni jukumu la vyombo vya ulinzi kusimamia na kuchukua hatua kwa vyama au watu wanaoingiza watoto katika siasa kwa manufaa binafsi bila kusahau kuandaa programu mbadala, wakati wa kampeni, wadau wa elimu na jamii wanaweza kuandaa shughuli mbadala za kielimu na kijamii zitakazowashirikisha watoto, ili wasione hamasa ya kwenda kwenye mikutano hiyo.