Majambazi wanne wauawa wakikabiliana na Polisi Songwe

By Moses Ng’wat , Nipashe
Published at 06:42 PM Dec 30 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga,
PICHA: MOSES NG'WAT
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga,

Watu wanne wanaodaiwa kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi katika makabiliano na Jeshi la Polisi mkoani Songwe, baada ya kutuhumiwa kuhusika na tukio la kuvamia duka la simu na huduma za kifedha, kisha kumuua mlinzi wake katika eneo la Stand Kuu ya Vwawa, Wilaya ya Mbozi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga, leo Desemba 30, 2025, tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:30 alfajiri ya Desemba 30, 2025, ambapo watuhumiwa hao walivamia duka hilo linalomilikiwa na mfanyabiashara Gabriel Msemwa na kumuua mlinzi wa duka hilo, William Mwampashi (45), kabla ya kuondoka na mali mbalimbali.

Kamanda Senga alisema baada ya tukio hilo kuripotiwa, Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi wa kina kwa kutumia taarifa za kiintelijensia, hatua iliyowezesha kuwabaini na kuanza kuwafuatilia watuhumiwa hao.
 Alieleza kuwa katika operesheni ya ufuatiliaji, askari waliwakamata watuhumiwa hao katika eneo la Ilembo, mjini Vwawa, walikokuwa wamejificha baada ya kutekeleza mauaji na uporaji huo.

“Hata hivyo, wakati askari wakitekeleza jukumu la kuwakamata, watuhumiwa walipambana na polisi kwa kutumia silaha, hali iliyopelekea kutokea kwa majibizano ya risasi,” alisema Kamanda Senga. Aliongeza kuwa, katika majibizano hayo, majambazi wanne walijeruhiwa kwa risasi na baadaye walifariki dunia walipokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi.

Majina ya waliouawa yametajwa kuwa ni Bruce Mwasenga, Eliuta Mapunda, Abdul Chiba na Justine aliyefahamika kwa jina moja. Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikuwa wahalifu sugu waliowahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha, lakini walikuwa wameachiwa baada ya kukata rufaa na kurejea tena katika vitendo vya kihalifu.

Aidha, polisi walisema watuhumiwa hao walihusishwa na matukio mbalimbali ya uhalifu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi. Katika eneo la tukio, askari walifanikiwa kukamata mali mbalimbali zinazodaiwa kuwa ziliibwa katika duka hilo, zikiwamo simu janja 30, simu ndogo 172, mashine moja ya POS ya Benki ya CRDB, bastola moja ya kutengenezwa kienyeji, mbalimbo, bisibisi nne, risasi nne, ganda moja la risasi, pamoja na nondo na makufuli mawili yaliyotumika kuvunja milango.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema linaendelea na msako mkali wa kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaohusishwa na tukio hilo ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.