SERIKALI imeanza mchakato wa kutengeneza mfuko wa ndani wa kuyawezesha mashirika yasiyo ya kiserikali kujiendesha, ili kuepukana na utegemezi wa ufadhili kutoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa Agosti 10, 2025 mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Tanzania, Mwantumu Mahiza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Azaki za Kiraia uliondaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRDC).
Mahiza amefafanua kuwa serikali imeshaelekeza juhudi za kuanzisha kutengeneza mfuko huo na uko mbioni kuanza, ili kuinua mashirika hayo na kwamba awali waliweka matarajio hadi ingefika mwezi Desemba, mwaka huu, ungekuwa umeanza lakini utachelewa kutokana na uchaguzi mkuu.
Amesema mfuko huo utakapoanza utasaidia mashirika kujiendesha ndani na utawezesha kupunguza baadhi ya masharti wanayopewa na wafadhili kutoka nje ya nchi ambayo baadhi ya hayo hayapendezi na kwenda kinyume na mila na desturi za kitanzania.
"Kwa pamoja tukishirikiana tutaweza kufika mbali na kuleta matokeo makubwa na kudumisha mila na desturi zetu kwa mustakabali wa taifa letu" amefafanua Mahiza.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema jukwaa hilo la pamoja la mkutano mkuu wa mwaka uliowakutanisha AZAKI za Kiraia 300 utaweza kujadili mambo muhimu kutoka na maazimio ya pamoja.
"Kuna baadhi ya mashirika hayapo tena mengine yamepunguza kutoa huduma kutokana na mtikisiko huo wa ufadhili kwahiyo changamoto ni kubwa," amefafanua
Mratibu wa THRDC Kanda Magharibi pia Mkurugenzi wa Shirika la Nguruko, Samwel Msokolo, amesema mkutano huo wa mwaka uliowakutanisha watetezi, umetuleta kwa pamoja utatuwezesha kuongeza ujuzi wa kufanya uchechemuzi katika kutengeneza na kurekebisha baadhi ya sheria hususani haki za binadamu na mabadiliko ya sera.
“Utatuwezesha kutoka na makubaliano ya pamoja kwa kipindi kinachofuata na kuongeza uwezo wa kukabiliana na majukumu mbalimbali ya utetezi wa haki za binadamu.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED