SHAHIDI wa sita upande wa Jamhuri, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Wilson Nchimbi, amedai mshtakiwa Maliki Jafari Maliki alikutwa amejificha uvunguni mwa kitanda wakati wa upekuzi uliofanyika nyumbani kwake Tandika, Temeke.
Tukio hilo lilielezwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, mbele ya Jaji Godfrey Isaya, ambapo ASP Nchimbi alitoa ushahidi wake kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ellen Masululi.
ASP Nchimbi alidai kuwa Machi 22, 2022, akiwa katika ofisi za Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, alipokea maagizo kutoka kwa Mkuu wake wa Kitengo akielekezwa kumkamata Maliki Jafari Maliki, anayedaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Baada ya kuandaa nyaraka muhimu, ikiwamo hati ya upekuzi, hati ya ukamataji mali na fomu ya onyo, ASP Nchimbi aliambatana na askari wenzake kuelekea nyumbani kwa Maliki. Walipofika walipokewa na mke wa Maliki, Dalinga Salumu, ambaye alidai kuwa mumewe hakuwa nyumbani.
"Tulijitambulisha na kumweleza nia ya kupekua nyumba. Baada ya kumpata shahidi huru, Tabu Hassan, tuliingia chumbani kwa Maliki na mkewe tukaanza upekuzi," alidai ASP Nchimbi.
Alidai walipokuwa wanaanza upekuzi, walimkuta Maliki amejificha uvunguni mwa kitanda. Walimwamuru ajitokeze ndipo wakaendelea na upekuzi, ingawa hawakukuta dawa za kulevya.
Badala yake walikuta vitambulisho mbalimbali, simu tatu, hati ya kusafiria na kadi ya chanjo ya homa ya manjano.
Shahidi huyo alidai kuwa katika mahojiano ya awali aliyofanya na Maliki, mshtakiwa alikiri kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, akitaja kuwa anashirikiana na washtakiwa wenzake, Iddi Nassoro na Mwinyi Mgazija Mwinyi.
ASP Nchimbi aliwasilisha mahakamani hati ya upekuzi na hati ya ukamataji mali kama vielelezo, ambavyo vilikubaliwa na kupokewa rasmi na mahakama.
Katika kesi hiyo, washtakiwa ni Maliki Jafari Maliki, Iddi Nassoro, Ally Jafari na Mwinyi Mgazija, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 1.02.
Washtakiwa wote wanajitetea kupitia mawakili wao, Nehemiah Nkoko, Habibu Kassim na Wilson Ogunde. Shauri hilo linaendelea kusikilizwa mahakamani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED