Ngeleuya: Mwigulu hana hisa Esther Luxury Coach

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:55 PM Dec 27 2025
MFANYABIASHARA na mwekezaji wa mabasi ya Kampuni ya Esther Luxury Coach, Joseph Ngeleuya
PICHA: GODFREY MUSHI
MFANYABIASHARA na mwekezaji wa mabasi ya Kampuni ya Esther Luxury Coach, Joseph Ngeleuya

MFANYABIASHARA na mwekezaji wa mabasi ya Kampuni ya Esther Luxury Coach, Joseph Ngeleuya, 'amemkana' Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, akitaka asihusishwe na umiliki wa mabasi hayo.

Ngeleuya, akizungumzia sakata hilo leo (Disemba 27,2025) katika Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, amesema Esther Luxury Coach, ni mali yake na familia yake, na wala isihusishwe na kiongozi yeyote wa kisiasa, au mtu mwingine yeyote, nje ya familia yake.

"Nimewaita hapa leo kwa lengo la kutoa ufafanuzi wa kina na wa ukweli kuhusu taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kwa ujumla, zinazohusu kampuni yangu ya usafirishaji inayojulikana kama ESTHER LUXURY COACH.

...Hivi karibuni, kampuni yangu imehusishwa kimakosa na baadhi ya viongozi wakuu wa kisiasa hapa nchini, ikiwemo madai kuwa inamilikiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba. Kutokana na tetesi hizo zisizo na ukweli, kampuni yangu imepata madhara makubwa wakati wa machafuko yaliyojitokeza baada ya uchaguzi, ambapo waandamanaji walivamia kampuni yetu, kuchoma mabasi sita na kuharibu mali nyingine nyingi.

Zaidi amefafanua: "Napenda kuwajulisha waandishi wa habari na Watanzania wote kwamba Esther Luxury Coach ni mali yangu na ya familia yangu, bila kuhusishwa na kiongozı yeyote wa kisiasa au mtu mwingine yeyote nje ya familia yangu."

Mfanyabiashara huyo, amesema kampuni hiyo ina hisa za watu wawili pekee, ambao ni yeye na mkewe, Neema Peter Thomas. "Jina la Esther tuliamua kulitumia kwa heshima ya mtoto wetu wa kwanza, Esther Joseph Ngeleuya.Huo ndio uhalisia wa kampuni yetu.

...Kwa masikitiko makubwa, tunawasihi Watanzania waache kufanya maamuzi ya kuharibu mali za watu kwa misingi ya tetesi na majungu. Hasara tuliyoipata ni kubwa sana na haiwezi kuelezeka kwa urahisi."

Kuhusu hasara iliyopatikana, Ngeleuya, amesema maandamano ya Genz ya Oktoba 29 mwaka huu, yamemuumiza kiuchumi, baada ya kupata hasara ya Sh. bilioni 2.1 kutokana na mabasi sita kuteketezwa kwa moto.