Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema maendeleo makubwa yanayoendelea katika Kampasi ya Mloganzila ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ni matokeo ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kupanua wigo wa elimu ya juu na huduma za afya kwa kujenga miundombinu mipya nje ya kampasi za zamani.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Prof. Mkenda amesema mradi unaotekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)—mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia—unalenga kujenga uwezo wa taasisi za elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wabobezi, kuimarisha tafiti na kuchochea maendeleo ya sekta ya afya na uchumi kwa ujumla.
Amesema Rais Samia alitoa maelekezo mahsusi kuwa fedha za miradi mikubwa ya elimu ya juu zisitumike tu katika kampasi zilizopo, bali zitumike kufungua maeneo mapya na kujenga vituo vya umahiri vitakavyohudumia Watanzania wengi zaidi.
“Ninajivunia sana maendeleo ya mradi huu wa HEET kwa sababu maelekezo tuliyopewa yanaonekana kwa vitendo. Kampasi zinajengwa Kagera, Rukwa, Zanzibar, Kigoma, Tabora, Mwanza, Shinyanga, Lindi na maeneo mengine. Kasi ya ujenzi tunayoyaona hapa Mloganzila yanafanana na yanayoendelea sehemu nyingine nchini,” amesema Prof. Mkenda.
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuifanya Mloganzila kuwa mji wa kitaaluma wa tiba (Academic Medical City) na kituo kikubwa cha umahiri wa mafunzo, tafiti na huduma za afya katika ukanda wa Afrika Mashariki, hususan katika magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, magonjwa ya damu, magonjwa ya kuambukiza pamoja na tafiti za kisayansi za hali ya juu.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Apollinary Kamuhabwa, amesema utekelezaji wa Mradi wa HEET katika Kampasi ya Mloganzila unagharimu Dola za Kimarekani milioni 45.5.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, dola milioni 30 zinaelekezwa moja kwa moja katika Kampasi ya Mloganzila, huku dola milioni 15 zikitumika katika maeneo mengine ya mradi huo. Alisema ujenzi unaoendelea unahusisha mabweni ya wanafunzi wa mwaka wa mwisho, majengo ya maabara za kisasa zipatazo 20, jengo la mafunzo ya anatomia kwa kutumia miili ya binadamu, maktaba, jengo la utawala, kumbi za mihadhara pamoja na miundombinu ya makazi kwa wanafunzi na watumishi.
“Ujenzi ulianza mwezi Desemba 2024 na kwa sasa majengo mengi yamefikia zaidi ya asilimia 50 ya utekelezaji, mengine yakifika hadi asilimia 70. Tunatarajia ujenzi huu kukamilika ifikapo Juni 2026,” amesema Prof. Kamuhabwa.
Ameongeza kuwa Kampasi ya Mloganzila, yenye ukubwa wa takribani hekta 3,800, tayari ina Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, na mwaka ujao ujenzi wa Hospitali ya Magonjwa ya Damu utaanza baada ya Serikali tayari kutenga fedha kwa ajili ya mradi huo.
Prof. Kamuhabwa amesema kukamilika kwa awamu ya kwanza ya miundombinu hiyo katikati ya mwaka ujao kutaiwezesha MUHAS kuongeza ubora wa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya kwanza na uzamili, pamoja na kuanzisha programu mpya adimu ambazo wataalamu wake ni wachache nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Uwekezaji huu mkubwa kupitia Mradi wa HEET utaiwezesha MUHAS kuongeza weledi wa wataalamu wa afya tunaowazalisha, kuimarisha tafiti na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya afya na elimu ya juu nchini,” amesema.
Ametoa shukrani kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika, akisema mradi huo ni hatua ya kihistoria katika kujenga mfumo imara wa elimu ya afya na huduma za tiba bora kwa Watanzania.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED