Uvutaji shisha washtua, sheria sasa kufumuliwa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 01:38 PM Jul 29 2025
Shisha
Picha: Mtandao
Shisha

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeanza mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya tumbaku na shisha nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wa afya ya umma na kudhibiti mmomonyoko wa maadili, hasa kwa vijana.

Uvutaji shisha washtua, 

sheria sasa kufumuliwa

 

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA


Akizungumza na TBC Redio Jamii juzi, Katibu Mtendaji wa LRCT, George Mandepo, alisema tume imeona umuhimu wa kupitia upya sheria hizo ili kuendana na mabadiliko ya kijamii na kuzuia madhara ya kiafya na kijamii yanayosababishwa na matumizi holela ya shisha na tumbaku.

"Vijana wengi wanavutwa na matumizi ya shisha, licha ya athari zake kiafya na kiuchumi. Hali hii inachochea kupungua kwa tija kazini na kuchangia kuenea kwa tabia zisizofaa," alisema Mandepo.

Mbali na hilo, Mandepo alieleza kuwa tume imeanza mchakato wa kupitia sheria zinazogusa michezo ya kubahatisha, kwa lengo la kulinda maadili ya watoto na vijana. 

Alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakitoroka masomo ili kushiriki katika michezo hiyo inayopatikana kwenye vibanda vya kamari, hali inayohatarisha mustakabali wao wa kielimu na kimaadili.

"Hili ni suala la haki za mtoto na linaangukia katika haki jinai na madai, hivyo tume inalipa kipaumbele kwa ajili ya kuweka ulinzi zaidi wa kisheria kwa watoto wetu," alisema.

Katika hatua nyingine, Mandepo alisema LRCT inaandaa mpango maalum wa kupitia sheria zinazohusiana na ardhi kutokana na kuongezeka kwa migogoro ya ardhi nchini. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwaka ujao.

Christina Binal, Mkuu wa Sehemu ya Mapitio ya Sheria LRCT, alisema tume imefanikiwa kupitia sheria kadhaa kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikiwamo Sheria ya Kampuni kwa lengo la kubaini upungufu unaokwamisha ufanisi wa biashara.

Alisema Sheria ya Majina ya Biashara imepitiwa kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa rahisi na thabiti.

Sheria ya Takwimu (Sura ya 351) imepitiwa kwa lengo la kuweka mfumo mmoja wa ukusanyaji takwimu serikalini kwa ufanisi zaidi.

Sheria ya Usuluhishi (Sura ya 15) imepitiwa kwa lengo la kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani kwa njia mbadala ya utatuzi wa migogoro.

Sheria ya Migogoro ya Mikopo ya Benki pia imepitiwa ili kurahisisha utatuzi wa migogoro hiyo bila kuathiri ukuaji wa uchumi.

"Sheria hizo zikipitiwa kikamilifu zitasaidia kuvutia wawekezaji, kurahisisha biashara na kuleta tija kiuchumi kwa taifa na kwa wananchi mmoja mmoja," aliongeza Binal.

Aidha, tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia kampeni ya 'Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, inayofanyika kwa njia ya vipeperushi, majarida, vipindi vya redio na televisheni. Mpaka sasa, zaidi ya wananchi milioni tano wamefikiwa na elimu hiyo.

Kwa upande wa haki za ndoa, Saada Bushiri, Mkuu wa Sehemu ya Udhibiti Ubora LRCT, alisema Sheria ya Ndoa iko wazi kuhusu mgawanyo wa mali ambapo kila mwanandoa, mwanamke au mwanaume, ana haki kupata sehemu ya mali aliyochangia wakati wa ndoa.

"Mama wa nyumbani si wa kupuuzwa. Amechangia kazi za nyumbani zinazomwezesha mwenza wake kutafuta kipato, hivyo anastahili kushirikishwa kwenye mgawanyo wa mali," alisema Bushiri.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea na jukumu lake la kuhakikisha sheria za nchi zinakuwa rafiki kwa wananchi, zinaboresha mazingira ya kiuchumi, kijamii na kitaasisi, sambamba na kulinda haki za msingi za binadamu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977).

---