KATIKA toleo la gazeti la Nipashe leo imeripotiwa habari ya mwanaume mmoja kukutwa amekatwa kichwa na kiwiliwili kutelekezwa kando ya barabara itokayo Nyegezi kona-Luchelele karibu na Chuo kikuu cha Mt.Agustono Tanzania (SAUT).
Jeshi la Polisi limeeleza kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kuwakamata watu wawili ambao ni Oscar Emmanuel (20), na Edwin Bujuel (22) wote wakazi wa Mtaa wa Shadi, kata ya Luchelele, wakidaiwa kuhusika na tukio hilo.
Kwamujibu wa taarifa ya polisi maerehemu alitambulika kwa jina la Dickson Madaraka (24), dereva bodaboda ambaye pia ni mkazi wa mtaa wa Shadi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Gidion Msuya amesema baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji ya kijana huyo na kulisaidia Jeshi la Polisi kuonesha mahali walipoficha kichwa chake pamoja na mali nyingine za marehemu.
Amesema mali hizo ni pamoja na pikipiki yenye namba za usajiri MC 715 ENN aina ya TVS rangi vyeusi na simu ya mkononi aina ya INFINIX HOT 10 wanazodaiwa kuzipora kwa marehemu kabla na baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Kamanda Msuya amesema, baada ya mahojiano ya kina imethibitika kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi kwa watuhumiwa kumtuhumu marehemu kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wa Oscar Emmanuel aitwaye Neema Marwa (17).
Pia amesema wakati watuhumiwa wanaonyesha mali za marehemu ndani ya msitu wa Nsumba, lilijitokeza kundi la wananchi waliopata taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia askari Polisi pamoja na watuhumiwa hao.
“Askari walijitahidi kuzuia wananchi wasiwashambulie watuhumiwa huku wakiepusha kutokea kwa madhara makubwa, endapo wangetumia nguvu kubwa ya silaha za moto walizokuwa nazo, kwani kwa watu wengi waliokuwa wamekusanyika na kufuatilia tukio hilo,”amesema Msuya.
Amesema katika purukushani hizo watuhumiwa wote wawili waliuawa na wananchi wenye hasira kali na waliojichukulia sheria mikononi huku askari wawili wakijeruhiwa na kukimbizwa hospitali kwa matibabu.
“Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya kanda Bugando kwa ajili ya kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi. Kichwa cha marehemu Dickson Mdaraka Yusuph pia kimehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya rufani Bugando kwaajili ya uchunguzi na utambuzi,” amesema Msuya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED