Wanawake zaidi wajitosa kuwania urais

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:50 PM Aug 11 2025
Miongoni mwa wanawake waliojitosa kuwania urais
Picha: Nipashe Digital
Miongoni mwa wanawake waliojitosa kuwania urais

WANAWAKE zaidi wameendelea kujitokeza kuwania urais na makamu wa rais, ikiwa ni tofauti na miaka mingine tangu kuanza uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.

Hadi sasa wanawake wawili wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa na vyama vyao kuwania urais, huku wanawake sita wakiomba nafasi ya Makamu wa Rais katika vyama 18 vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, mwaka huu.

Hii ni hatua kubwa katika historia ya Tanzania kwa kuwa haikuzoeleka wanawake kushika nafasi za juu kwenye siasa za Tanzania kuanzia ndani ya vyama hadi uongozi wa nchi.

Leo, Agosti 11, 2025, wanawake wawili wa Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Noty Mirambo alichukua fomu ya uteuzi kuwania urais, akiwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji.

Pia chama cha TLP, kimempitisha mgombea mwenza ni Amana Suleiman Mzee, akiongeza idadi ya wanawake wanaowania nafasi za juu.

Agosti 9, mwaka huu, Samia Suluhu Hassan alikuwa wa kwanza kuchukua fomu ya kugombea tena urais kupitia CCM, akifuatiwa na chama cha AAFP ambacho pia kimemteua mwanamke, Chumu Juma Abdalah kuwa mgombea mwenza.

Aidha, wanawake wengine wawili, Chausiku Khatib Mohamed (NLD) na Azza Haji Suleiman (MAKINI) nao walijitokeza kugombea nafasi za juu za uongozi. Hii ni ishara ya wazi kwamba sasa wanawake hawasubiri tena nafasi kuletwa mezani, wanazisaka na kuzichukua kwa ustadi.

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), nacho kimepiga hatua kwa kumpitisha Devotha Minja, Makamu Mwenyekiti wake, kuwa mgombea mwenza wa urais, huku ACT-Wazalendo ikimpitisha Fatma Abdulhabib Ferej kwenye nafasi hiyo hiyo.

Aidha, ACT-Wazalendo pia kilimchagua Dorothy Semu kuwa Kiongozi wa chama na alitia nia ya kuwania urais mwaka huu, lakini alijitoa katikati ya wiki iliyopita kumpisha Luaga Mpina.

Mwanamke wa kwanza kuonesha njia kwa wanawake Tanzania kuwania nafasi ya juu kwa nchi, ni Mwanamke jasiri, Anna Senkoro, mwanamke wa kwanza kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kupitia chama cha PPT Maendeleo.

Katika uchaguzi wa 2015, wanawake wengine wawili waliingia katika kinyang’anyiro cha urais: Anna Mghwira (ACTWazalendo) na Queen Sendiga (ADC). Leo hii, Queen Sendiga ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, baada ya kuwaongoza pia Iringa na Rukwa.