WATU saba kati ya kumi wanaojihusisha na biashara ya ununuzi na uuzaji katika mtandao ya kijamii kwa siku hukumbana na utapeli wa kuibiwa huku ukiacha maumivu makubwa kwa baadhi huku wengine wakijikuta kuathirika kisaikolojia.
Jukwaa la biashara mtandaoni la Go7eight katika utafiti yake iliyoifanya mwakahuu umebaini ongezeko la utapeli huo huku maelfu ya Watanzania kupoteza fedha na kuathirika kisaikolojia na kupelekea msongo wa mawazo huku hali hizo zikileta migogoro hata kwa familia.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa jukwaa la Go7eight, Jackline Malavanu amesema kufuatia hali kwa watanzania jukwaa hilo linakuja na kampeni ya uhamasishaji umma ijulikanayo kama SEMA UPONE inayolenga kuwahamasisha waathirika kujitokeza na kuzungumza ili kuwalinda wengine wasiingie katika mitego hiyo.
Amesema kampeni hiyo imelenga kuwapa sauti waathirika ambao mara nyingi huchagua kunyamaza baada ya kukutana na kadhia ya kudhulumiwa kampeni hiyo itasaidia kuwaponya wengine. Aidha amebainisha utafiti huo pia unaonyesha kuwa visa vinane kati ya kumi vya utapeli unaotokea kupitia mitandao ya kijamii umebaini udhibiti wa mifumo ya ulinzi kwa watumiaji wa mitandao bado ni mdogo haijaimarika ipasavyo.
“Watu wengi wanaopata matatizo ya utapeli mtandaoni huogopa kuzungumza kwa kuhofia kudharauliwa au kulaumiwa. Wengine hupitia msongo wa mawazo na kuamua kubaki kimya,” alisema. Ameongeza kuwa kampeni ya Sema Upone inalenga kukusanya simulizi halisi kutoka kwa waathirika, ili kuelimisha umma, kuongeza tahadhari na kuzuia wengine kuangukia katika mitego hiyo.
Kupitia kampeni hiyo, wananchi wanahimizwa kushiriki uzoefu wao kwa njia ya maandishi mafupi, sauti au video, wakieleza jinsi walivyotapeliwa na majukwaa yaliyotumika. Hatua hiyo inakuja wakati matumizi ya mitandao ya kijamii katika biashara yakiongezeka, hasa misimu wa sikukuu, ambapo Watanzania wengi hutegemea mitandao hiyo kununua bidhaa na huduma mbalimbali.
Kwa mujibu wa utafiti huo utapeli mara nyingi huanza kwa matangazo ya bidhaa kwa bei ndogo isiyo ya kawaida wateja huombwa kulipa fedha zote awali au sehemu ya fedha hiyo kabla ya kupokea bidhaa, kisha muuzaji hutoweka baada ya malipo kufanyika.
Amefafanua Vijana wengi huathirika kutokana na kuamini sana, kukosa taarifa sahihi na kuvutiwa na bei nafuu zisizo halisi na kuweka wazi hali hiyo endapo itaendelea bila kudhibitiwa inaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi nchini.
Kupitia kampeni ya Sema Upone, waandaaji wanawahimiza wananchi kuzungumza wazi, kushirikiana taarifa na kusaidia kujenga mazingira salama ya biashara mtandaoni haitakiwi kunyamaza ili kuwalinda wengine ili kukuza soko salama la kidijitali.
Aidha Malavanu amejitolea mfano yeye mwenyewe aliwahi kupoteza kiasi cha Sh.660,000/ alipokuwa akinunua simu ya mkononi mtandaoni wakati wa masomo yake ya chuoni. “Niliambiwa nitume fedha mapema ili mzigo usafirishwe. Baadaye nikaombwa hela nyingine kwa madai ya ushuru. Baadaye nikaona namba ya ufuatiliaji ilikuwa ya uongo,” alisema.
Miongoni mwa waathirika wengine ni Mussa mfanyabiashara wa mitindo ya nguo mtandaoni, alisema aliwahi kupoteza Sh.250,000/ baada ya kuamini tangazo la duka la mitindo lililokuwa mtandaoni. “Nilivutiwa na bei nafuu na mauzo ya haraka, baada ya kulipa tu bidhaa sikuwahi kuzipata. Hii ilisababisha hasira na hofu ya kuendelea na biashara mtandaoni,” alisema.
Kwa upande wa waathirika wa kike, Neema Mbaga mwanafunzi wa Shule ya Sekondari alieleza jinsi alivyopoteza Sh.120,000/ baada ya kuamini tangazo la komputa ndogo ya masomo mtandaoni. “Nilidhani napata ofa nzuri kwa ajili ya masomo yangu, lakini niliambulia hasara kubwa na kuathirika kisaikolojia. Nilihisi kudanganywa na kuogopa kununua mtandaoni tena,” alisema.
Wengine ni Hassan mfanyabiashara wa bidhaa za kilimo, ambaye alikumbana na utapeli wa Sh400,000 kutoka kwa mteja mtandaoni aliyedai kulipa kabla ya kupokea bidhaa. “Nilijikuta nikipoteza fedha na kuogopa kuendelea na biashara mtandaoni,” alisema. Pia Amina mfanyabiashara mdogo, alieleza jinsi alivyopoteza kiasi cha Sh200,000 baada ya kutapeliwa kwa bidhaa za mitindo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED