Wananchi wa Tegeta A leo wamepata faraja kubwa baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha polisi kipya kilichojengwa kwa jitihada na nguvu zao wenyewe.
Kituo hicho, ambacho kimekuwa ndoto ya muda mrefu ya jamii, sasa kipo tayari kutoa huduma muhimu za ulinzi na usalama karibu na wananchi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, amesema: “Kuna maeneo mengine wananchi wanachoma vituo vya polisi, lakini hapa Tegeta A mmechagua kujenga. Hii ni hatua ya kizalendo na ya kuigwa. Nawapongeza kwa mshikamano wenu na moyo wa kujitolea kwa ajili ya usalama wa jamii.”
Akizungumza katika uzinduzi huo, wananchi mbalimbali wameeleza kuwa kituo hicho kitapunguza changamoto za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za polisi, na pia kitasaidia kupunguza vitendo vya uhalifu.
"Tunamshukuru sana Mkuu wetu wa Wilaya kwa kuja kushirikiana nasi katika siku hii muhimu. Lakini zaidi tunawashukuru wananchi wote waliotoa michango yao ya hali na mali hadi kufanikisha ujenzi wa kituo hiki," alisema mmoja wa viongozi wa mtaa huo.
Kwa upande wao, viongozi wa kijamii wametoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika kudumisha amani na usalama wa eneo la Tegeta.
Akihitimisha hotuba yake, Mkuu wa Wilaya Msando alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusogeza huduma za kijamii na kiusalama karibu na wananchi, na kwamba Tegeta A imekuwa mfano halisi wa ushirikiano wa Serikali na wananchi katika kufanikisha maendeleo.
Kuzinduliwa kwa kituo hiki kunatajwa kuwa ni ushahidi wa mshikamano wa wananchi na mfano wa kuigwa katika maeneo mengine nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED