TUNAPOSHEREHEKEA Siku ya Mwalimu Nyerere mwaka huu, tunarejea kumkumbuka kiongozi aliyeishi kwa maadili ya utumishi, uadilifu na kujitolea kwa ajili ya maendeleo ya watu wake na bara la Afrika kwa ujumla, hoja ikizama mbali hadi dunia.
Kwa Mwalimu Julius Nyerere, uongozi ulikuwa jukumu la kutembea pamoja na wananchi, kuwainua kwa pamoja na kutanguliza maslahi ya wengi kuliko yale binafsi.
Katika wakati uliopo ambao sekta ya afya barani Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi, ni muhimu kuenzi maono na uongozi wa Mwalimu Nyerere, kwa kujifunza kutoka kwake.
Jicho kuu hususan leo, linazama katika kukuza uongozi wa utumishi kwa viongozi wetu wa kikanda, ili kuhakikisha mustakabali bora wa afya kwa bara letu.
NYERERE VS KUASISIWA ECSA-HC
Miaka 51 iliyopita, yaani mwaka 1974, Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC) ilianzishwa chini ya uratibu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Lengo lake kuu lilikuwa ni kuunganisha nguvu za pamoja kutoka mataifa jirani ili kukabiliana na changamoto za kiafya kwa mshikamano.
Mwalimu Nyerere alikuwa mmoja wa waanzilishi wa taasisi hiyo, akiamini kuwa hakuna taifa la Afrika linalopaswa kupambana pekee dhidi ya milipuko ya magonjwa, uhaba wa rasilimali, au changamoto za sera.
Ifikapo mwaka 1980, nchi wanachama zilichukua rasmi umiliki wa ECSA-HC kupitia mkataba wa makubaliano uliotiwa saini na mawaziri wa afya.
Leo hii ECSA-HC inajumuisha mataifa tisa: Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Eswatini, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe. Huku ikitoa msaada wa kiufundi kwa zaidi ya nchi 16 nyingine barani Afrika.
CHANGAMOTO ZA LEO
Mosi, kuna uwekezaji mdogo na utegemezi wa wafadhili. Licha ya afya kuwa nguzo ya ustawi wa jamii, mataifa mengi ya Afrika bado hayawekezi vya kutosha.
Kwa mfano, Tanzania inatumia takribani asilimia 5.1 ya bajeti yake kitaifa kwa afya, huku Zimbabwe ikiwa karibu asilimia 5.2. Mataifa mengi bado yanategemea misaada ya wafadhili kwa zaidi ya asilimia 30 hadi 40 ya bajeti zao zake kiafya. (Ripoti ya Human Rights Watch, 2024)
Pili, kuna utegemezi mkubwa wa bidhaa kutoka nje wastani wa asilimia 70 hadi 90 ya bidhaa za afya Afrika huagizwa kutoka nje, zikiwamo dawa, vifaa tiba, chanjo na vipimo.
Afrika huzalisha chini ya asilimia 30 ya dawa zake na chini ya asilimia 10 ya vifaa tiba. Kwa chanjo, uzalishaji wa ndani ni chini ya asilimia moja, hali inayoifanya Afrika kuwa katika hatari ya kipekee wakati wa migogoro ya kimataifa ya usambazaji wake.
Utafiti nchini Tanzania unaonesha, dawa zinazozalishwa nchini huwa na bei nafuu (MPR 0.69) ikilinganisha na zilizoagizwa (MPR 1.34), lakini upatikanaji wake ni mdogo, hasa katika sekta binafsi.
Nchini Ethiopia, dawa za kuagiza zilionekana kuwa nafuu zaidi katika baadhi ya vipimo, lakini bado zilikosa uhakika wa upatikanaji wake.
Hiyo inaonesha kuwa uzalishaji wa ndani hauwezi kufanikiwa, bila ya kuwa na mifumo bora ya udhibiti, usambazaji, ubora na sera thabiti.
FUNZO LA COVID-19
Kuwapo janga la maradhi COVID-19, lilifichua kwa kina udhaifu wa Afrika kutokana na kutegemea nje. Marufuku ya usafirishaji, ushindani kimataifa wa malighafi na kuchelewesha usambazaji, vilisababisha uhaba wa barakoa, PPE, oksijeni, vipimo na chanjo.
Ni hali iliyosababisha vifo vya kutisha na kusambaratika kwa huduma za afya.
UNUNUZI UNAOIJENGA AFRIKA
Mifumo ya ufadhili wa afya duniani, inaelekea katika mabadiliko makubwa. Benki za maendeleo, wahisani na mashirika ya kimataifa sasa yanataka Afrika ijitegemee zaidi kupitia uzalishaji wa ndani.
Hilo linahimizwa kufikia minyororo ya usambazaji kikanda na kujenga ‘uhuru wa kiafya’ (health sovereignty). Umoja wa Afrika (AU) kupitia dira yake mpya ya afya (New Public Health Order) inasisitiza kujitegemea kwa bara kwa njia ya uwekezaji wa ndani kwenye dawa, vipimo na teknolojia.
Katika mazingira hayo mapya, inaifanya Afrika kuwa ouia mzalishaji, si mtumiaji wa bidhaa pekee. Kauli mbiu ya “Nunua Afrika, Jenga Afrika” lazima itafsiriwe kwa vitendo.
MIKAKATI 7 YA MABADILIKO
Moja, ni ununuzi wa pamoja na vituo vya uzalishaji vya kikanda. Nchi wanachama wa ECSA-HC zinaweza kuanzisha mifumo ya pamoja ya manunuzi ya dawa na vifaa, ili kupata bei nafuu na kiasi kikubwa cha uzalishaji kwa viwanda vya ndani.
Vituo vya uzalishaji vikanda, kwa mfano Tanzania, Kenya n, Uganda, vinaweza kusaidia kuzalisha API, vifaa tiba, na vipimo vya uchunguzi.
Pili, inagusa ulinganifu wa sheria, ubora na viwango; Uzalishaji wa ndani lazima usimamie viwango vya kimataifa. ECSA-HC inaweza kusaidia kuimarisha mamlaka za udhibiti za kitaifa, kuoanisha mifumo ya sheria na kuiunga mkono chombo chao kiitwacho Africa Medicines Agency (AMA).
Tatu, kuna Uwekezaji na motisha kwa sekta binafsi: hapo, serikali ziandae mazingira refiki ya uwekezaji kama misamaha ya kodi, maeneo maalum ya visanda vya afya, na ushirikiano na sekta binafsi.
Shirika la UNCTAD linaonesha kuwa sera kama hizi ni muhimu kuvutia mitaji ya uzalishaji wa ndani.
Nne, ni kuimarisha mifumo ya afya na minyororo ya usambazaji: Uzalishaji pekee hautoshi, bali ni lazima kuwapo upatikanaji malighafi, mifumo bora ya usambazaji, ufuatiliaji wa kidijitali, vifaa vya kuhifadhi na uwezo wa kutunza vifaa. ECSA-HC inaweza kusaidia kwa msaada wa kiufundi na mafunzo.
Tano, ni katika ufadhili wa pamoja wa kikanda wa afya: Azma ni kupunguza utegemezi wa wafadhili, ECSA-HC kuweza kuchochea uundaji bima za afya kikanda, mifuko ya mshikamano na kodi za mpakani kwa bidhaa za afya.
Tano, ni kwa maandalizi ya pamoja dhidi ya majanga: Kuwapo akiba ya vifaa vya dharura kama PPE, oksijeni, na vipimo. Kituo cha dharura cha kikanda (Emergency Operations Centre) na miongozo ya msaada wa haraka vitasaidia usimamizi wa janga lolote litakalojitokeza.
Saba, inarejea uongozi na utumishi bora, mfano wake Mwalimu Nyerere: Ili hayo yote yafanikishwe, kunahitajika viongozi wa afya wanaoishi maadili yake.
Hao ni wanaosikiliza, kushirikiana na kuweka mbele huduma. Viongozi wa ECSA-HC wanapaswa kulazimishwa kuwa wajenzi wa madaraja kati ya serikali, sekta binafsi, taasisi za elimu na jamii.
MWELEKEO MPYA AFRIKA
Siku ya Mwalimu Nyerere, ina umuhimu wa kufanyiwa kumbukumbu, pia wito wa kuchukulia baadhi ya hatua. Ni wakati wa kuacha mifumo ya utegemezi na kujenga uwezo wa ndani. ECSA-HC, kama nguzo ya afya kwa zaidi ya miaka 50, inapaswa sasa kuwa kinara wa mageuzi ya kina.
Afrika haina budi kuachana na utegemezi wa kuagiza na kuwa wazalishaji. Hiyo itahitaji mipango ya pamoja, uongozi wa maono, na utashi wa kisiasa unaozingatia utu na huduma kama ilivyokuwa hulka ya Mwalimu Nyerere.
Inatajwa Afrika yenye afya bora, ni Afrika inayojitegemea. Pia, inatajwa kuwa Afrika inayojitegemea hujengwa kwa mshikamano, uzalishaji wa ndani na uongozi wa kiutumishi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED