Kunusurika kukeketwa, kumemnoa na siasa za kupigania haki zake mwanamke

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:29 PM Apr 10 2025
Catherine Ruge
Picha: Mtandao
Catherine Ruge

CATHERINE Ruge ni mwanasiasa na mwanaharakati, mzaliwa wa wilayani Serengeti mkoani Mara, miaka miaka 40 iliyopita.

Anasema nyumbani waliishi maisha ya kawaida, kilimo na ufugaji, akiyathamini maisha ya wazazi wake yaliyomfundisha uhalisia. 

Mwaka 1989 anataja kumpoteza baba yake akiwa na umri miaka sita, mama alibaki nguzo ya familia.

Catherine anatajitambulisha ni mwanamke wa kwanza kijijini kwao kumaliza kidato cha sita, pia kupata shahada ya kwanza, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Anasimulia masomo shahada ya pili akapata katika Chuo cha Uongozi Kusini Mashariki mwa Afrika. 

Pia, Catherine ana cheti cha juu cha uhasibu (CPA -Certified Public Accountant), amesajiliwa na Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Anasema, licha ya kuwa mwanasiasa, wazazi wake wamedumu wakulima na wafugaji.

Historia yake, anatajaa alipoingia CHADEMA, Suzan Lyimo, Mwenyekiti Baraza la Wazee wa chama hicho, na Janeth Mbene, mwana -CCM aliyewahi  kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, ni wanawake anaowataja kumlea kutokana na aina ya siasa za kisomi na weledi walizokuwa wakifanya. Leo anataja alikopitia kumemfanya mwanaharakati.

ALIKOPITIA

Anaisimulia Nipashe alivyonusurika kukeketwa baada kukimbia mpango ulioandaliwa, akitishwa na ushuhuda waliokeketwa wakavuja damu nyingi, kupoteza fahamu, akahofu zamu yake. 

“Mwaka 1994, nikiwa darasa la tano, nilipaswa kukeketwa, wakati huo baba alishafariki. Kipindi hicho ilikuwa ni lazima ukeketwe, nilinusurika kukeketwa na sio kwa kuwa nilijua madhara ya ukeketaji, bali nilikuwa naogopa.

“Nilishuhudia binamu zangu waliokeketwa wakitokwa na damu nyingi lakini mmoja alizimia, nikajua amefariki dunia, baadaye aliamka. Kwa hiyo iliniogopesha sana, nikakimbia,” anasema.

Catherine anasema asichosahau, baada ya kukimbia siku tatu baadaye mganga wa kienyeji aliletwa nyumbani afanya utaalamu wake, akaambiwa:

 “Huyu binti ndio amekaidi kukeketwa na kufuata mila yetu. Mganga alinitamkia maneno ya laana ambayo yalinisononesha.

“Alinitamkia kuwa sitafaulu katika masomo yangu, sitaolewa, sitazaa bali nitatangatanga na sitakuwa mtu yoyote kwenye maisha.

“Laana hiyo ilitolewa mbele ya ndugu zangu na kila mtu akisikia. Hiki ni kitu ambacho sijawaeza kukisahau katika maisha yangu, mpaka leo bado nakumbuka hadi nguo alizokuwa amevaa yule mganga na upande aliokuwa amekaa pale sebuleni kwetu.

“Toka kipindi hicho nimekuwa nikiishi kwa wasiwasi sana nikidhani ile laana itanishika na nilikuwa nikivuka ‘stage’ (hatua) moja kwenye maisha namshukuru Mungu.

“Wakati wa kusubiri matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na cha sita nilikuwa na wasiwasi sana sikuweza kula wala kulala vizuri, nikiwaza nitapata ile laani.

“Lakini nilipata ufaulu wa juu sana na kuchaguliwa shule za vipaji maalum Msalato na Kilakala na baadaye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Baada ya kuolewa, ujauzito wangu wa kwanza uliharibika, nikasema sasa ile laana imenishika, niliogopa sana, lakini Namshukuru Mungu baadaye Mungu alinibariki watoto wawili wa kiume wazuri sana,” anasimulia.

Anataja elimu ndiyo ilimpa mafanikio ya sasa wanasiasa na mwanaharakati huru. Amewahi kuwa balozi wa kupinga masuala ya ukeketaji wasichana, pia, balozi wa hedhi salama.

SAFARI KISIASA, KIJAMII

Kupitia siasa, anataja kuanzisha asasi ya kumkomboa mtoto wa kike kuepuka ukatili, akisema ilimwezesha kufanikisha haki zake.

Hadi sasa anajisifu kuleta mabadiliko katika jamii yake, ikiwamo kujenga bweni la kisasa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana  Ring’wani, walio katika mazingira hatarishi. 

Anataja alianza harakati zake kisiasa mwaka 2010, alipojiunga na CHADEMA mwaka 2013, akaingia katika uongozi, akiteuliwa Katibu wa Rasilimali Fedha Kanda ya Serengeti; mikoa ya Mara, Shinyanga na Simiyu.

Catherine anasimulia mwaka 2015, akagombea ubunge jimbo la Serengeti, hakufanikiwa na mwaka 2016, akagombea Utunza Hazina wa Kanda na kushinda.

Huku akitumikia nafasi hiyo mpaka mwaka 2019, kuanzia mwaka 2017 hadi 2020 alikuwa mbunge wa viti maalum.

Pia, akiwa na dhamana hiyo, akawa Mweka Hazina Taifa wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) na mwaka 2021 akachaguliwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa, nafasi aliyoitumika hadi Januari mwaka huu. 

Huko nyuma harakati zake zilimuinua, anataia mwaka 2016/2017 akashinda tuzo inayoitwa ‘UN-Empowering Women Champions for Change’ ya kuelimisha na kuhamasisha wanawake kujikwamua kiuchumi kwa rasilimali zao.

Catherine anaamini kutumia uwanja wa siasa kumsaidia kuwafikia watu wengi hasa wanawake, pia kushawishi kisheria. 

KASI YAKE BUNGENI

Akitajwa mdau mkubwa bungeni wa mada za demokrasia, mazingira, afya, elimu, na haki za wanawake na wasichana.

Sasa anafurahi kuungwa mkono na ndugu jamaa na marafiki, akimtaja mama kwa kunukuu kauli yake: “Mafanikio yake (Catheerine) si yake peke yake, bali ya jamii nzima.”

“Mama yangu ananipongeza na kunipa ushirikiano katika kila hatua ya maendeleo na mafanikio yangu,” anatamka

KUIVA KISIASA

Anasimulia kupatwa na ushawishi akisaliti chama chake, akifafanu: “Wanawake ambao tumeaminiwa na kupata nafasi za uongozi tuonyeshe mfano, kuwa tunaweza…

“Umechaguliwa mbunge, diwani, fanya vizuri uwape imani wananchi kwamba kumbe hata tukimchagua mwanamke inawezekana….” 

“Pia, serikali iendelee kutoa fursa, kuwepo kwa uwiano kati ya wabunge wanaume na wanawake angalau hata asilimia 50 wawe ni wanawake ili waonyeshe uwezo wao,” anasema Catherine.

Anakisifu chama chake Chadema, kwamba mwanamke akigombea na mwanaume akashika nafasi ya pili au tatu, moja kwa moja anateuliwa, kwenye jimbo.

Catherine anaamini katika uongozi jimbo ni fursa ya kumtathmini aliyeko, mwanamke au mwanaume anayoyafanya, akinena hafurahii kuwakilisha viti maalum:

“…mimi wakati niko bungeni nilikuwa nikitaka kuchangia naambiwa subiri kwanza wabunge wa majimbo wachangie…

“Unaulizwa wewe unataka kuongea nini? Kwa hiyo, viti maalumu sioni kama vinasaidia, japo vimeongeza uwakilishi wa wanawake.

“Serikali iangalie namna bora ya kuongeza uwakilishi kwenye vyombo vya maamuzi, kwani vimekuwa viti vya kudumu kwa baadhi ya watu Fulani.”

Mbunge huyo anaamini ubunge wa viti maalumu ni wa muda mfupi, kuwapa fursa wanawake wengine wajao kujifunza.

Anatoa darasa kuwapo wabunge waliokaa muda mfupi na wakapita katika majimbo na kuwa wabunge, mfano Ester Matiko, Ester Bulaya, Janneth Mbene, Bonna Kalua, na Halima Mdee.

“Mwanamke ameshakuwa mbunge wa viti maalum kwa miaka mitano na umeshamjengea uwezo, kwanini asiende jimboni?

“Mfano chama changu cha Chadema, ukiwa viti maalumu unaambiwa tafuta jimbo la kugombea uishi kwenye kivuli, anza kujenga jimbo ni lazima na kila miezi sita utoe ripoti umefanya nini kwenye hilo jimbo,” anasema.

AWASUKA WAJAO

Catherine anataja kuwajenga na kuwapika wanawake kuwa viongozi katika wilaya ya Serengeti, pia mkoani Dodoma anamtaja Aisha Madoga.

“Niliwapika, nikawajengea uwezo wa kujiamini nikawapa ujuzi, nikawapa mafunzo ya kuwa viongozi bora na waadilifu.,” anasema Catherine, akiongeza kufanikiwa zaidi ni alipoanza harakati kisiasa na kijamii.

Katika orodha anawataja: Hilda Peter, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema, Kanda ya Kati mkoa miatu Singida, Dodoma na Morogoro.

Pia, Rukia Abubakar Mohamed, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Pemba na Chake Chake 

“Nilianza jambo kwa udogo, kwa kuhamasiha kupinga masuala ya ukeketaji katika wilaya ya Serengeti na ndani ya familia.

“Baadaye, nikapata fursa katika majukwaa makubwa sio tu kuzungumzia masuala ya kupinga ukeketaji bali masuala ya wanawake na watoto wa kike. Kwa hiyo kupitia hiki nilienda bungeni na kupaza sauti sana na jambo kubwa lilikuwa ni kupambana kuondoa kodi katika taulo za kike…

“Tulifanikiwa, japokuwa baadae ilirudishwa na mimi ndio nilikuwa katibu wa kikosi kazi hicho,” anasimulia.

SIRI YA MAPAMBANO

Catherine anataja mafanikio mengine ni kampeni ya msichana kurudi shule katika mfumo rasmi, baada ya kupata mimba na ikapitiswa na bunge.

Anatamka kujivunia sana hlio jambo akiamini kuacha alama mpaka sasa, anasema: “Binafsi nimefanikiwa sana katika haya kwa sababu ya kuwa malengo (focus), huwa nikitaka jambo langu lazima linakuwa, mimi ni jeshi la mtu mmoja, hata kama wengine wanapinga mimi nitapigana mpaka tone la mwisho la damu.

“Kingine ni kujiamini na kusimamia kile ninachokiamini na siku zote huwa nakuwa upande wa haki, ukisimama upande wa haki utaungwa tu mkono. Kitu kingine ni kutokata tamaa. 

“Nimepitia mambo magumu sana katika maisha yangu nikiwa mdogo sana, kwa hiyo huwa sioni kitu kigumu kwangu, hata mawimbi yakija, nitakwenda kushoto kulia lakini nitasimama imara,” anasema.

Anasema ndoto yake kubwa haijatimia, akitamani siku moja kuwa mbunge wa jimbo kutumikie jamii likozaliwa. Aligombea meaka 2020, lakini hakufanikiwa.Catherine anaitaja ndio ndoto aliyobaki nayo.

WALIONUFAIKA NAYE

Nchota Makore (70), mama wa mwanasiasa huyo, anajivunia mafanikio ya binti yake na mabadiliko aliyoyafanya wilayani Serengeti, ikiwamo kuwapigania wasichana dhidi ya mila potofu, hata ukeketaji.

 “Ameleta mabadiliko, ameleta maendeleo, amewasaidia wasichana kwa kuwajengea bweni, kwa sasa wanasoma katika mazingira mazuri hawana shida tena.

"Tunajivunia mafanikio yake. Kupambana na ukeketaji ulikuwa ni mchango mkubwa ambao ameufanya, umeendelea kumfanya kuwa hodari na mpigania haki wa kweli. Mimi kama mama, napinga ukeketaji sana, nashirikiana na Catherine mwenyewe," amesema.

Magesa William, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ring’wani wilayani Serengeti mkoani Mara, anasema bweni lililojengwa na aliyekuwa mbunge, Catherine, limekuwa mchango mkubwa na mabadiliko, yakisaidia  watoto wa kike kuzifikia ndoto zao, anaona mabadiliko.

"Bweni hili lina ukubwa wa kuchukua vitanda 48 na lilianza kuchukua wanafunzi kuanzia Januari 2018….” anatamka Mkuu wa Shule na kuongeza vijijini kuna mabinti waliopanga vyumba, nao wanalazimika kuwalinda.

“Tangu kuanzishwa kwa bweni hii, haijawahi kutoa divisheni zero…. Divisheni one ya (pointi) 15 alipata mwanafunzi kutoka bwenini, kwa hiyo bweni hili limekuwa na mchango mkubwa na msaada kwa mabinti hawa,” anasema.

Mwalimu Magesa anasema tangu kuanzishwa kwa bweni hilo wanafunzi 75 kutoka bweni walichaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo. 

Kwa upande wake, Jack Joseph (21) ambaye sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mhitimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Ring’wani mwaka 2021. 

Anasema ndio mwaka walifaulu wasichana wengi kutokana na ushawishi wake Catherine.

WADAU SIASA

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Janeth Mbene, anasema amemfahamu Catherine Ruge, wakati amechaguliwa kushika viti maaluma.

Anamtaja Catherine, kwa kauli: “Ruge ni msichana anayeongea kwa hoja tofauti na wapinzani wengine ambao wanapenda kupinga bila hoja.

“Akitaka kuchangia au kusema jambo bungeni lazima litakuwa na mashiko na lenye maana zaidi. Ni mtu anyeapenda kujifunza, kushirikiana na kusimamia anachokiamini. 

“Mara nyingi alikuwa anakuja kwangu kuniomba ushauri kuhusu mambo mbalimbali. Mimi alinikuta tayari nimetumikia bunge kwa miaka mitano. Lakini niliiona ni ‘potential’ na ndio maana nilikiua nikimuogoza…”

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema, Kanda ya Kati yenye mikoa Singida, Dodoma na Morogoro, anamtaja ni mvuto kwa kinamama.

‘Sikujua kwamba Catherine ana kipawa cha kuinua wanawake , mabinti wadogo kuwa train ili wawe viongozi au wana siasa kakubwa , nilianza kumfahamu tuu kama kiongozi wa Bawacha.

“Nilipoonana naye mara ya kwanza, kulikuwa na semina ya ‘leadership’(uongozi) ya wanafunzi vyuoni ndipo nilipomfahamu, aliponiona nachangia mada alivutiwa na hoja zangu ndipo, aliniita kuniuliza maswali mbalimbali.”

Hapo anataja kumpenda na akaanza kumshirikisha kwenye siasa, akunuia wanawake wengi wawe viongozi, akafanikiwa.

Catherine yuko katika kundi la wabunge G55 wanaopingana na msimamo wa chama hicho kutoshiriki katika Uchaguzu Mkuu ujao.