Kupiga kura kwa uelewa, hiari huleta kesho iliyo bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:29 PM Oct 15 2025
Hatima ya maisha bora ya wanawake na watoto imo mikononi mwa uongozi wa umma, unaopatikana kupitia kura inayopigwa kwa kufanya maamuzi sahihi.
Picha: Mtandao
Hatima ya maisha bora ya wanawake na watoto imo mikononi mwa uongozi wa umma, unaopatikana kupitia kura inayopigwa kwa kufanya maamuzi sahihi.

JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu tuliangalia kwa nini mbinu za kusukuma agenda ya usawa wa kijinsia zinatakiwa kuboreshwa ili ziendane na mazingira ya sasa na hatimaye ziweze kuleta mabadiliko chanya na endelevu. Katika safu yetu leo, tutaangalia kwa nini nafasi ya wanawake wakati wa uchaguzi haiishii tu kwenye kuweka alama ya tiki kwenye karatasi ya kura na kutumbukiza karatasi hiyo kwenye boksi la kura. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira

Wanawake wanapopiga kura kwa uelewa na kwa hiari yao, hujenga kesho yao bora 

Katika kampeni nyingi za uchaguzi, mara nyingi wanawake wamekuwa wakihamasishwa kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura lakini pia kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kupiga kura kumchagua kiongozi wanayemtaka. 

Ingawa hakuna ubaya wowote kuelekeza juhudi kubwa katika maeneo hayo, lakini ni muhimu kutambua kwamba nafasi ya wanawake wakati wa uchaguzi, haiishii tu kwenye kuweka alama ya tiki kwenye karatasi ya kura na kutumbukiza karatasi hiyo kwenye sanduku.

Kwa mtazamo wa juu juu, kupiga kura huenda likaonekana kama tendo rahisi. Lakini kwa mwanamke anayejielewa, kura hiyo ina maana kubwa sana, ni zaidi ya alama kwenye karatasi, ni zaidi ya takwimu ya idadi ya kura zilizopigwa; ni sauti yake, msimamo wake, dhamira yake, namna ya kudai haki yake, ni nafasi yake ya kushiriki moja kwa moja katika kuamua hatma ya jamii anamoishi.

Kutokana na hali hiyo, ni muhimu basi, kila jamii ihakikishe kwamba wanawake wanahamasishwa, wanaheshimiwa, na wanashiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa kisiasa, kwa sababu kura yao ni mabadiliko.

Kwa wale wanaodhani umuhimu wa wanawake wakati wa uchaguzi ni kupiga kura tu, wanakosea sana kwani kufanya hivyo ni kuwafananisha na watazamaji wa mchakato wa kisiasa, badala ya kuwaona kama washiriki hai, wenye maono, uwezo na haki ya kuchangia mwelekeo wa taifa lao.

Ingawa kitendo cha kutumbukiza kura kwenye boksi kinaonekana kama rahisi sana lakini matokeo yake yana nguvu kubwa inayoweza kuathiri moja moja maisha ya wana jamii ya kila siku kupitia chaguo walilolifanya. Mambo kama bei za bidhaa, usalama mitaani, haki na uhuru wao na upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii, yote ni matokeo ya kura yao ambapo kama walifanya chaguo la busara huduma hizo zitapatikana na vivyo hivyo watakosa huduma hizo iwapo chagua lao lilikuwa baya. Kwa ufupi, kura yao inaweza kuamua maisha yao yawe bora ama mabaya.

Kupiga kura ni njia nzuri inayowapa nafasi wanawake kupaza sauti kwa namna ya kipekee kuhusu kero zilizoko katika jamii zao. Wakati ambapo njia nyingine za kutoa maoni na kupaza sauti kuhusu kero, zinaweza kuwa ngumu kwa wanawake lakini kupitia kura zao katika sanduku la kura, kila mmoja ana sauti sawa.  

Kwa mfano wananchi wanapokataa kumchagua tena kiongozi aliyeshindwa kutatua shida ya maji katika mtaa wao kipindi alipokuwa madarakani, inamaanisha kuwa wamechoka na kero hiyo na wanataka kiongozi mwingine mwenye mikakati dhabiti ya kuondoa changamoto hiyo. Kitendo cha kumng’oa kupitia kumnyima kura ni ujumbe mzito kwamba kura ina nguvu ya kuamua nani aongoze. 

Wanawake, kwa kutumia nguvu ya kura yao, wana nafasi ya kuchagua viongozi wale tu wanaotambua na watakaoweza kulinda maslahi yao. Sauti yao kupitia kura inaweza kusaidia kuleta mabadiliko katika sheria na sera zinazowaathiri moja kwa moja, kama vile haki ya uzazi, usawa kazini, na uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.

Hata hivyo ni vema tukafahamu kuwa kura ya mwanamke inakuwa ya maana pale anapoamua mwenyewe bila kulazimishwa wala kulaghaiwa kwamba namchagua huyu kwa sababu atatetea maslahi yetu, atasimamia haki na hatasimamia maslahi yake binafsi. Wanapopiga kura kwa uelewa na kwa hiari yao, wanakuwa si wapiga kura tu bali ni viongozi wanaochora ramani ya kesho katika jamii na taifa lao

Kwa maneno mengine unaweza kusema kura ya wanawake ni sauti ya matamanio, matarajio, na msimamo wao katika kujenga jamii yenye usawa, haki, na maendeleo kwa wote. Hivyo basi, kuwahimiza wanawake kupiga kura ni jambo jema, lakini kuwawezesha kuelewa kuwa kura yao ni silaha ya mabadiliko, ndiyo hatua ya kweli ya kuwaweka mstari wa mbele katika siasa na uongozi wa taifa.

Ni vema kufahamu kuwa kitendo cha wanawake kupiga kura hakiwanufaishi wao peke yao bali ni kwa manufaa ya familia zao, jamii zao na taifa lao. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wanawake ndio walezi, walimu wa familia zao, watenda kazi wakubwa katika jamii na maamuzi yao huleta mabadiliko yanayoweza kuathiri kila mtu katika jamii.

Kwa ujumla, kupiga kura ni tendo la nguvu, dhamira, na ushiriki wa kweli katika kuleta maendeleo na usawa. Ni ujumbe wa kisiasa na kijamii unaobeba matumaini na mabadiliko. Kwa msingi huo, wanawake hawapaswi kushiriki uchaguzi kwa lengo la kupiga kura tu, bali wanapaswa kutambua kwamba kila kura yao ni sauti yenye nguvu ya kubadilisha mambo kuwa bora zaidi na yenye ustawi endelevu.