KAMPENI za Uchaguzi Mkuu ziko ukingoni, vyama vinavyoshiriki vimesikika kwenye mikutano ya hadhara,Watanzania wamewaona, wamewasikiliza na sasa ni kazi kwao kuingia kwenye sanduku la kura na kufanya maamuzi sahihi Jumatano ijayo Oktoba 29.
Miongoni mwa waliosikika na kuonekana ni Haji Ambari Khamisi mgombea wa urais kupitia chama cha NCCR-Mageuzi, ambaye anasema chama chao kina mipango lukuki iliyomo ndani ya Ilani ya2025/30 na watakapoingia ikulu wataanza mchakato wa kupata mwafaka wa kitaifa na katiba mpya.
NCCR-Mageuzi ikipata ridhaa kuingia Ikulu kinaipatia Tanzania maridhiano kwa kuanzisha mchakato wa kufikia mwafaka wa kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya nchi na wananchi Khamisi akiahidi kuwa watausimamia kwa nguvu zote.
Mchakato utahusisha wanasiasa, makundi mbalimbali ndani ya jamii, wakiwamo wataalam wa utatuzi wa migogoro, asasi za kiraia, vijana, wanawake, walemavu na wote wanaopenda maendeleo, kwani lengo ni kutaka kujenga nchi kwa pamoja," anasema Khamisi.
Anasema mwafaka wa kitaifa utawezesha kupata tume huru ya uchaguzi na pia kuondokana na mfumo wa chama dola na kwamba ili kufikia lengo hilo, Watanzania hawana budi kuafikiana na kwamba licha ya tofauti zetu za kiitikadi, yapo masuala ambayo chama chochote kitakachoshika madaraka lazima kiyaheshimu, kwa kuwa ni ya taifa letu.
Anafafanua kuwa mwafaka wa kitaifa utajumuisha makubaliano katika mambo ya msingi yenye maslahi ya taifa na watu wake hasa kwa kuweka mbele Utanzania badala ya kusimamia itikadi tofauti za vyama.
Katika mwendelezo huo, anasema serikali ya NCCR-Mageuzi itahamasisha mwafaka juu ya misingi mikuu ya utaifa ambayo itapendekezwa na kukubalika na jamii kwa ujumla bila kujali chochote.
"Tunataka kufanya hivyo, kwa sababu mwafaka wa kitaifa utasaidia kupanua wigo wa fikra zetu kuhusu maadili ya viongozi na wananchi. Hivi sasa mjadala kuhusu maadili ya taifa unajali na kuelekeza nguvu kwenye ufisadi, lakini hoja hii ni pana kuliko ufisadi," Khamisi anasema.
Aidha, katika ilani yao wanasisitiza kuwa ni lazima kwa pamoja kama Watanzania kuzungumzia malezi ya taifa, misingi na sababu ya malezi hayo, uzalendo na masuala muhimu yakiwamo mmomonyoko wa maadili.
KATIBA MPYA
Mbali na hilo, katika ilani yao mgombea Khamisi anataja katiba mpya na kuahidi kuwa iwapo atashinda, serikali yake itarejesha na kukamilisha mchakato wa kupata katiba hiyo kupitia bunge la katiba lenye kujumuisha makundi yote ya kijamii kadri atakavyoshauriana na viongozi wenzake ili kuwaletea Watanzania kile wanachokitaka na kukililia kwa miaka mingi.
"Mchakato wa kupata katiba mpya ulitekelezwa kwa sehemu kubwa na muhimu, lakini ukakwama, ni wazi kwamba katiba mpya ni takwa la Watanzania wengi, hivyo tutaendeleza mchakato iwapo hakutakuwa na dalili za kupatikana kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 20230," anasema.
Anafafanua kuwa katiba ya nchi ndiyo sheria kuu ya nchi, sera za serikali na sheria za nchi lazima zitokane na kufungamana na katiba ya nchi, na kwamba kama taifa lina katiba mbaya isiyolinda haki za wananchi, sheria na mfumo wa utoaji haki utakuwa mbaya na usiotenda haki.
Mgombea huyo anasema kuwa hilo la mchakato wa katiba mpya, litafanyika baada ya kuwa na mwafaka wa kitaifa ambao anaueleza kuwa ndiyo msingi wa kuwaweka watu pamoja kama taifa.
Anafafanua kuwa mchakato wa kurejesha katiba mpya utakwenda sambamba na maboresho kadhaa yaliyogawanyika maeneo 10 muhimu kwa lengo la kuifanya iwe manufaa kwa watu wote.
YAKUBORESHWA
Mgombea urais Khamisi anataja maeneo ya muhimu watakayosimamia katika uongozi wao kuwa ni kupata katiba mpya na kuboresha sheria za nchi.
Kukubaliana kitaifa kuwa kuvunja na kukiuka katiba ni kosa la jinai.
"Eneo la muhimu pia litakaloangaliwa ni kuongeza wigo wa uhuru na haki za msingi za binadamu katika katiba, jingine ni kuwa na tume huru ya uchaguzi, tutahakikisha suala la kugatua madaraka kutoka serikali kuu kwenda mamlaka za serikali za mitaa linazingatiwa," anasema.
Eneo jingine ni kumpunguzia rais madaraka yake, ikiwamo kujaza au kufanya uteuzi wa baadhi ya nafasi za uongozi serikalini asiwateue.
Jingine ni kuwapa wananchi mamlaka ya kuwa ndiyo wamiliki na watawala wa taifa lao katika shughuli zote zinazohusu maslahi yao na taifa lao kwa ujumla na hivyo.
"Katika uongozi wetu tutaweka sheria na taratibu za kuwawezesha wananchi kudhibiti na kuwajibisha dola na vyombo vyake ili viwatumikie badala ya wao kuwa watumwa wa kuvitumikia," anasema.
Mgombea huyo anaongeza kuwa wanataka kuhifadhi kikatiba haki za binadamu ambazo hazijahifadhiwa na katiba ya nchi kama vile haki za mgombea binafsi, za elimu, afya, kupata habari na haki ya kujifungua salama bila kufa mama wala mtoto.
"Eneo jingine muhimu ni kusimamia pia umuhimu wa kuitambua sekta ya habari kikatiba ili kuimarisha demokrasia, uhuru na haki za vyombo vya habari," anasema.
Kulipa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania nguvu kama chombo cha kutetea maslahi ya wananchi na umma, kuwa na maamuzi ya mwisho katika utungaji wa sheria, kuridhia mikataba na kuwa na mamlaka ya kupitisha na kuthibitisha au kutopitisha ama kutothibitisha uteuzi wa viongozi wa serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED