JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu tuliangalia kwa nini nafasi ya wanawake wakati wa uchaguzi haiishii tu kwenye kuweka alama ya tiki kwenye karatasi ya kura na kutumbukiza karatasi hiyo kwenye boksi la kura. Katika safu yetu leo, tutaangalia kwa nini ni muhimu kwa wanawake kupiga kura kwa hekima. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira
Kwa nini ni muhimu kwa wanawake kupiga kura kwa hekima?
Wote tunafahamu kuwa kupiga kura ni nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko na kusukuma mbele maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa katika taifa lolote. Wanawake, kama nguzo muhimu ya jamii, wana nafasi ya kipekee ya kuchangia mabadiliko hayo kupitia ushiriki wao katika uchaguzi.
Wiki ijayo Watanzania wote, wake kwa waume tutashiriki katika zoezi muhimu na la kihistoria, yaani uchaguzi mkuu. Kwa mara nyingine, tutapata nafasi ya kusema ndiyo au hapana kwa viongozi wanaotaka kushika hatamu za uongozi.
Kwa wanawake wa taifa hili, hii si nafasi ya kawaida. Ni nafasi ya kipekee ya kuandika historia mpya kupitia karatasi zao za kura. Ni fursa ya kutumia sauti zao kujenga mustakabali unaojali utu wao, familia zao na kizazi chao. Ndiyo maana leo, zikiwa zimebaki siku chache kufikia siku ya uchaguzi, ni muhimu kumkumbusha mwanamke juu ya wajibu wake wa kupiga kura si kwa mazoea, bali kwa hekima.
Kabla ya kuendelea, ni vema tukajadili kidogo maana ya kupiga kura kwa hekima. Kwa maneno mepesi, kupiga kura kwa hekima ni kitendo cha kuchambua kwa makini sera, tabia na rekodi za wagombea, kisha kufanya maamuzi yaliyojaa busara, ujasiri na maono wakati wa kupiga kura. Ni kutumia haki hiyo ya kupiga kura kwa uhuru, bila hofu na kwa kuzingatia maslahi yako na ya wengine kama wewe.
Je, kupiga kura kwa hekima kuna faida gani kwa wanawake? Zipo faida nyingi lakini mojawapo ni kwamba kitendo hiki kinawawezesha wanawake kuchagua viongozi wanaoelewa changamoto zao na walio tayari kusimamia sera zinazowasaidia wao na jamii zao.
Kadhalika, kupiga kura kwa hekima kunawawezesha wanawake kuvunja minyororo ya kimfumo na kusema ndiyo kwa mabadiliko yanayowajumuisha kama washiriki kamili katika mchakato wa demokrasia na si kama wapambe tu kwenye siasa. Katika muktadha huu, mwanamke haonekani tu kama mpiga kura wa kawaida, bali kama mleta mabadiliko, mlinzi wa maadili, na mjenzi wa taifa lenye usawa na maendeleo endelevu.
Wote tunafahamu kuwa si kila mgombea anayeomba kura yako ana malengo ya kuwatumikia wale waliomchagua. Je, wanawake watamtambuaje mgombea anayejali maslahi yao? Hili ni swali la msingi sana. Utambuzi wa haraka unaoweza kusaidia ni rekodi za wagombea katika kutetea na kusimamia maslahi ya wanawake, wasichana na jamii kwa ujumla.
Wapo wanasiasa ambao mara zote wamekuwa wakisikika wakizungumzia masuala yanayomgusa mwanamke moja kwa moja, kwa mfano, ukatili wa kijinsia, afya ya uzazi, ajira kwa wanawake, elimu kwa wasichana na mengine.
Lakini wapo wanasiasa wengine ambao wamewahi kusikika wakitoa kauli, kufanya vitendo vya kuwadhalilisha wanawake au kushindwa kukemea ama kuchukua hatua stahili kulinda utu, heshima na haki ya mwanamke.
Ukipima aina hizo mbili za wagombea, utabaini ni yupi kati ya hao anakufaa. Kura yako ina uzito mkubwa, kama mgombea hafai, usikubali kushawishiwa kwa kupewa kitenge, kilo ya mchele au kushinikizwa na ndugu, marafiki ama familia. Piga kura kwa mujibu wa dhamira yako, maarifa yako, ndoto zako na maono yako.
Kupitia kupiga kura utaweza kusema kile ambacho huwezi kukisema kwa maneno ya kawaida. Kumbuka kuwa kama mwanamke, una nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa familia yako, jamii yako, na taifa lako, na hili unaweza kulifanya tu iwapo utapiga kura kwa hekima na si kwa mazoea.
Kwa miaka mingi, wanawake wamekuwa wakihangaika na changamoto zinazotokana na kutokuwepo kwa sera zinazowagusa kwa ukaribu. Ukosefu wa huduma bora za afya ya uzazi, ukatili wa kijinsia unaoachwa bila kushughulikiwa, ukosefu wa mikopo, na vikwazo katika elimu au ajira ni mambo ambayo hayapaswi kuwa kawaida.
Mwanamke anapochagua kiongozi ambaye vipaumbele vyake ni mambo muhimu kwa wanawake kama elimu, afya, huduma za mama na mtoto, usalama, mazingira bora ya biashara ndogo, na ustawi wa jamii, anakuwa ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa.
Kumbuka, kura isiyo ya hekima inaweza kuleta uongozi duni usiowajali wananchi, hali ambayo huathiri zaidi wanawake na watoto. Hekima katika uchaguzi ni msingi wa mabadiliko ya kweli.
Kwa ujumla, kura ni silaha ya mabadiliko. Kwa kutumia kura yako, unaweza kulinda maslahi ya familia yako, afya ya watoto wako, elimu ya mabinti zako, na ustawi wa jamii yako kwa ujumla.
Hata hivyo ili kura yako iweze kuleta tija ni lazima uipige kwa hekima. Usipofanya hivyo, wengine watafanya kwa niaba yako na mara nyingi hawatakuweka kwenye vipaumbele vyao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED