KAMPENI za Uchaguzi Mkuu zinaingia kwenye hatua ya mwisho zikizidi kufurahisha na kujawa na matumaini mapya kwa Watanzania, huku mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akiibuka kama kiongozi mwenye dira na uhalisia wa maendeleo yanayogusa maisha ya watu, kutokana na yaliyofanyika.
Ziara yake katika mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Simiyu imeacha alama kubwa kwa wananchi, wengi wakieleza kuwa “ameahidi kwa kutenda.”
Katika mikutano yake, Dk. Samia ametoa ahadi zaidi ya 50 zinazolenga sekta kuu za uchumi, kijamii na miundombinu, ikiwamo afya, elimu, nishati, biashara, kilimo, ajira, na usafirishaji, ambazo tayari zimeanza kuzaa matokeo yanayoonekana.Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni kuboreshwa kwa Hospitali ya Rufani ya Kagera.
Dk. Samia anasema serikali imeongeza huduma za kibingwa, hatua iliyopunguza safari za wagonjwa kwenda Bugando au Muhimbili.
“Idadi ya wagonjwa waliotibiwa imeongezeka kutoka 128,305 mwaka 2021 hadi 478,002 mwaka 2025. Hili ni ongezeko la zaidi ya watu 349,000 waliopata huduma hapa nyumbani,” anasema Rais Samia, akiahidi pia kuzindua bima ya afya kwa wote ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa tena, ili kila Mtanzania awe na uhakika wa matibabu bila kikwazo cha kiuchumi, jambo lililopokelewa kwa makofi na vigelegele vingi.
Katika sekta ya elimu, Dk. Samia anaahidi kuendelea na ujenzi wa shule mpya, mabweni na vyuo vya ufundi. Tayari mkoa wa Kagera una shule tatu za amali, shule ya sayansi kwa wasichana na vyuo vitano vya VETA vilivyojengwa katika kipindi cha miaka mitano.
Serikali pia imeendelea kutunisha Mfuko wa Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ili vijana wengi zaidi wapate fursa ya kujiendeleza kielimu. “Tunataka elimu iwe nguzo ya ajira. Vijana wasome, wabobee katika fani na wawe sehemu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda,” anasema.
Akiwa Bukoba, Dk. Samia anatangaza ujenzi wa soko la kisasa la machinga complex lenye thamani ya Sh. bilioni 10. Lengo ni kuimarisha mazingira ya biashara, kuongeza ajira na mapato ya halmashauri.Vilevile, serikali itaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hatua iliyothibitishwa kuwa imeongeza miradi midogo na ajira mpya.
Sambamba na hilo, anasisitiza pia ahadi yake ya Sh. bilioni 200 kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali, ili kukuza uchumi wao.
“Tutaongeza fursa, lakini pia tutahakikisha mikopo inatumika vizuri kwa miradi yenye tija,” anaeleza na kutaja ahadi kubwa katika sekta ya nishati ni kuhakikisha kama kuna kitongoji ambacho hakijapata umeme kinapata huduma hiyo ndani ya miaka miwili ijayo.
Kagera ina miradi minne mikubwa ya kuzalisha umeme wa maji yenye jumla ya megawati 221.8, ikiwamo Rusumo, Ngara na mradi mpya wa kuzalisha megawati 40 unaoandaliwa na serikali pia inaendelea kusambaza nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti na kulinda afya za wananchi.
Mgombea wa CCM anasema serikali imejipanga kuibadili sekta ya kilimo kuwa kilimo biashara, kwa kuongeza tija na kipato cha mkulima, kupitia mpango wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT), vijana, wavuvi na wafugaji watapewa mitaji na vifaa vya kisasa.
“Tunataka kilimo kiwe ajira, si kazi ya mazoea. Vijana wetu watatumia teknolojia, mbegu bora na masoko ya uhakika,” anaahidi kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao, hasa vya kahawa na samaki, ambavyo vitaendelea kujengwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kwingineko nchini, ili kuongeza ajira na mapato ya ndani.
Rais Samia anabainisha kuwa serikali inaendelea kuboresha bandari za uvuvi, vituo vya kuhifadhia samaki na viwanda vya kuchakata nyama. Anataja chanjo za mifugo zimeendelea kutolewa kwa wingi, huku machinjio yanaboreshwa kufikia viwango vya kimataifa ili kuongeza mauzo ya nyama nje.
Uboreshaji wa Bandari ya Kemondo na ya Bukoba ni sehemu ya mikakati yake ya kukuza biashara kati ya Tanzania, Uganda na Rwanda. Na hapa anaahidi “Tumeongeza usalama wa mizigo na abiria, tumekarabati gati mbili na kujenga jengo jipya la abiria lenye uwezo wa kuchukua watu 700.”
Anabainisha kuwa meli ya kisasa MV Mwanza, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 400, itakuwa chachu ya biashara na utalii katika Ziwa Victoria.Katika hotuba zake, Rais Samia anasisitiza umoja na amani kama msingi wa maendeleo.
Katika kampeni hizi anaishukuru idara za ulinzi na usalama kwa kuhakikisha mikutano yote ya kampeni imefanyika kwa utulivu. Miongoni mwa matukio makubwa katika mikutano hiyo ni kurejea kwa viongozi wa upinzani ndani ya CCM miongoni ni Mwenyekiti mstaafu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekia Wenje, ambaye katika mkutano unaofanyika Chato, mkoani Geita, anasema amerudi CCM kwa sababu “mbele kuna mwanga.”
“Mheshimiwa Samia ametenda, kila tunakopita tunasikia mabilioni ya miradi ya kijamii. Hii ndiyo Tanzania mpya tunayoiamini,” anasema Wenje.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, anamtambulisha Rais Samia kama kiongozi wa matendo, si maneno, akiahidi ametenda, ahadi zake zinapimika na kazi zake zinaonekana, anasema kwenye moja ya mikutano ya mgombea urais Kanda ya Ziwa.
Ziara ya Rais Samia katika Kanda ya Ziwa imeonyesha mwelekeo wa Tanzania mpya yenye matumaini, kutokana na kauli ya baadhi ya wananchi wakizungumzia mabadiliko makubwa waliyoyaona katika sekta za afya, elimu, maji, umeme na ajira.
“Tunaona matokeo, si propaganda. Hii ni serikali inayotenda, si ya maneno,” anasema Neema Byabato, mkazi wa Bukoba mjini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED