RIPOTI za kimataifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na shirika linalohusika na masuala ya Ukimwi (UNAIDS) zinaonesha malaria, kifua kikuu (TB) na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), bado ni mzigo mkubwa unaozitesa nchi nyingi duniani, ikiwamo Tanzania.
Taarifa ya mwaka 2024 iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti na Kupambana na VVU (TACAIDS), inaonesha Tanzania inakadiriwa kuwa na takribani watu 60,000 wanaopata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka, wanawake wakiongoza, ikilinganishwa na wanaume.
Takwimu za taifa zinaonesha kwamba nchini, takribani watu 1,548,000 wanaishi na VVU, huku asilimia 78 wakitajwa kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo.
Katika jitihada za kudhibiti ugonjwa huo, Tanzania imeweka malengo yaitwayo ‘95-95-95’ ya UNAIDS ikimaanisha kwamba asimilia 95 ya wananchi wanapaswa kujua hali zao, huku asilimia 95 watumie dawa husika na kiwango hicho asilimia 95 wasiweze kuambukiza.
Kwenye kiwango cha kimataifa, ripoti zinaonesha kwamba mzigo mkubwa wa VVU uko barani Afrika na hususani nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
KIFUA KIKUU KILIVYO
Ripoti ya asasi ya kimataifa iitwayo Global Tuberculosis Report 2023, inakadiria kuwa dunia nzima inapata kesi milioni 10.8 za kifua kikuu, Afrika ikitajwa kuwa na mzigo mkubwa wa ugonjwa huo, ikikadiriwa kuwa na asilimia 23 ya mikasa mipya za TB duniani na asilimia 31 ya vifo vyake ngazi hiyo ya dunia.
Kihistoria, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zenye mzigo wa juu wa maambukizi ya ya kifua kikuu, hali kadhalika VVU.
Hata hivyo, sasa kuna mageuzi kwa ripoti za kitaifa, zikionesha Tanzania imepiga hatua nzuri maambukizi yakipungua kutoka watu 306 kati ya watu 100,000 mwaka 2015, hadi watu 183 kati ya 100,000 kwa mwaka 2023, pakimaanisha.
Vifo vya TB nchini pia vimeripotiwa kupungua kwa asilimia 68 kwa maana ya kutoka vifo 58,000 mwaka 2015, hadi vifo 18,400 mwaka huo 2023.
Kiwango cha mafanikio ya matibabu, kwa kesi zilizotambuliwa mwaka 2023 nacho kinatajwa kuwa
asilimia 96, ambacho ni juu ya malengo ya kitaifa na ile ya WHO.
ILIVYO MALARIA
Ripoti ya Malaria mwaka jana (World Malaria Report 2024), inaonesha kuwa mwaka 2023 kulikuwapo mikasa milioni 263 za ugonjwa huo, ikiwa ni ongezeko kutoka milioni moja mwaka juzi.
Hivyo ni vifo vinavyotokana na malaria yanayokadiriwa kuwa 597,000 mwaka 2023. Kwa Kanda ya WHO Afrika, Tanzania kunatajwa kuwa na mzigo mkubwa kwa asilimia 94 ya mikasa ya malaria duniani na asilimia 95 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Changamoto inayotajwa kukwamisha vita dhidi ya malaria, hali ya upinzani wa dawa, upinzani wa viuatilifu vya mbu (insecticide resistance) na usambazaji hafifu wa kinga na matibabu katika baadhi ya maeneo.
Kwa Tanzania, ripoti ya WHO ya mwaka 2023/2024 inakadiria kuwa katika mwaka 2021 kulikuwapo mikasa milioni nane za malaria pamoja na vifo 25,787, huku maambukizi yakikadiriwa kuua watu 126 katika watu 1,000.
Hali hiyo imeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizoorodheshwa katika mzigo mkubwa, hata kuwekwa katika kinachoitwa na WHO katika malaria kuwa ni “High Burden to High Impact” (HBHI) ya WHO kwa malaria.
Kwa mujibu wa WHO mwaka 2023, Tanzania imechangia asilimia 4.3 ya vifo vya malaria dunini.
Hata hivyo, kukirejewa ripoti hizo kuna hatua kupigwa, Tanzania ikishuhudia kupungua kwa maambukizi ya TB na mafanikio ya matibabu yakiboreshwa. Shida inaonekana bado katika afya ya umma katika ubia wa magonjwa matatu (HIV, TB, malaria).
Aidha, shida ya kuwapo bajeti inayotegemea wafadhili wa nje katika kukabiliana na magonjwa, inatajwa kuwa kikwazo kinachotajwa kukwamisha nchi nyingi za kiafrika, Tanzania ikiwamo.
Ili kuiwezesha Tanzania kupambana na watafiti wamebaini mbinu nne za kupata mapato kwa ajili ya bajeti ya afya kwa magonjwa hayo na mengineyo, ili kulina afya ya jamii.
Wanasema ufadhili wa ndani, unachangia takribani asilimia 42.8 ya jumla ya matumizi ya sasa ya afya, hali inayosababisha sehemu kubwa ya huduma muhimu kubaki katika hatari kutokana na kutegemea misaada isiyotabirika ya wafadhili nje ya bajeti.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Francis Ngadaya wa Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health Institute), kwa ushirikiano na watafiti wenzake kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na kitengo chake cha utafiti.
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakichambua maoni kutoka kwa watunga sera 76 na watoa huduma za afya nchini.
Wanasayansi hao wametoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kushuka kwa kasi kwa huduma za kitabibu katika programu kuu za taifa zinazopambana na malaria, VVU/UKIMWI na TB.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa katika toleo la Septemba 29 la jarida la BMJ Public Health lenye makao yake jijini London, Uingereza wakisema nchi kama Tanzania zinapaswa kupata suluhisho endelevu la ufadhili wa ndani kwa programu hizo, wakipendekeza mikakati ya kuziba pengo kifedha linaloongezeka.
Hapo wanaonya kwamba bila kuchukua hatua za haraka, mafanikio yaliyopatikana kwa muda mrefu katika kupambana na magonjwa hayo matatu makuu, yanaweza kudorora au kurudi nyuma.
Watafiti hao wanasisitiza kwamba, mbali na kutafuta vyanzo vipya vya mapato, kuna haja kubwa ya mageuzi ya ndani, ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya rasilimali zilizopo.
Mojawapo ya mapendekezo yao muhimu ni kuanzishwa kwa mpango wa bima ya afya kwa wote, ambao Serikali ya Awamu ya Sita nchini imeanza mikakati ya kuisuka, kwa kupanua wigo wa walengwa na kuongeza mapato thabiti na yanayotabirika.
Pia, wanapendekeza kutoza kodi katika bidhaa na huduma fulani, hususan zile zinazoitwa za ‘dhambi’, zinazolenga bidhaa kama vile tumbaku, vileo au vinywaji vyenye sukari nyingi, ili fedha zake zielekezwa katika huduma za afya.
Watafiti hao pia wanapendekeza, kuanzishwa mifuko maalumu ya magonjwa, mfano Mfuko wa TB (TB Trust Fund), kwa ajili ya kuhakikisha ufadhili wa muda mrefu na unaolengwa moja kwa moja kwenye magonjwa husika.
Kadhalika, wanapendekeza kupunguza makundi yanayopata huduma za afya, bila ya malipo, kwa kuondoa misamaha ya jumla na kuelekeza huduma za bure kwa makundi katika mazingira magumu zaidi.
HALI HALISI NYUMBANI
Ni utafiti unaobainisha kwa miaka mingi Tanzania kama nchi nyingine nyingi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, imekuwa ikitegemea kwa kiwango kikubwa misaada kutoka kwa washirika wa kimataifa.
Hapo kunatajwa mifano ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kudhibiti UKIMWI (PEPFAR) na Mfuko wa Dunia (Global Fund) chini ya Benki ya Dunia (World Bank Group) — utegemezi ulioathiriwa na changamoto za dunia, ikiwamo janga la magonjwa ya UVIKO-19, ambayo katika dalili za kutokuwa endelevu tena.
Aidha, wanasisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa kuongeza uwazi katika usimamizi na matumizi ya fedha za afya, sambamba na mamlaka ya kifedha katika ngazi za chini.
Wanapendekeza kutenga asilimia maalumu ya mapato ya halmashauri kwa huduma za afya na kutoa mamlaka zaidi kwa vituo vya afya kufanya maamuzi ya kifedha.
Pia, kuna pendekezo la kupunguza gharama na kuwekeza zaidi katika kinga na utambuzi wa mapema, kupunguza upotevu wa rasilimali hospitalini na kuboresha upatikanaji dawa kupitia uzalishaji wa ndani.
Hapo kunatolewa mifano ya nchi nyinginezo kama Kenya, kumeanzisha Mfuko wa VVU (HIV Trust Fund), unaotumia kati ya asilimia 0.5 na moja ya mapato ya serikali, huku matogfa kama Namibia na Malawi, zikitumia mbinu mseto zinazojumuisha michango ya sekta binafsi na ushuru wa safari za ndege.
Mtafiti Ndagaya, anautaja unaweza kutumika kama mifumo endelevu ya ufadhili, akinena: “Bila mawasiliano ya wazi na mifumo imara ya uwazi, juhudi hizi zinaweza kudhoofishwa na upinzani wa umma au matumizi mabaya ya fedha,”.
Ni aina ya uafiti uliolenga kuwapa watunga sera na viongozi wa sekta ya afya taarifa za kisayansi zitakazowasaidia kutengeneza sera jumuishi zinazokuza ufadhili endelevu wa afya, ili taifa liweze kulinda afya na ustawi wa wananchi wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED