KATIKA mageuzi ya kiafya kwa jamii, hadi sasa sifa iliyoko ni kwamba vijana wadogo wanafika umri wa kupevuka mapema sana, hata kuzua aina ya mijadala kuhusu tafsiri yake.
Jibu la awali kitaalamu sasa liko mezani, kwamba dhana kuu hapo ni “lishe bora imechochea mabadiliko makubwa katika ukuaji wa miili ya watoto na vijana, tofauti na miaka ya nyuma.”
Ndani yake inaanika majibu ya ziada kihistoria, kufanikiwa msingi wa elimu ya afya kwa Watanzania, iliyohubiriwa sana na Rais Julius Nyerere akitumia matamshi; “aina ya chakula ziko tatu (anazitaja) ...lazima tufuate kanuni za afya, mtu ni afya!”
Kurejea matokeo ya kinachojiri kwa vijana sasa, ni kwamba hali inayoonekana zaidi kwa wasichana wanaoanza kupevuka katika umri wastani miaka 10.
Katika elimu na maana ya kinachotokea sasa kwa watoto, kundi la wazazi ambao hawajapata tafsiri yake kwa usahihi, huangukia katika hofu kwa baadhi yao, wakibakiwa na kiulizo cha mabadiliko mapema ya miili kwa watoto wao.
Hapo ndipo wataalamu wa afya, pia maandiko ya taaluma yao kuhusu lishe, zina ufafanuzi kwamba: “Hali hiyo ni ya kawaida kwa watoto wanaopata chakula bora chenye virutubishi vya kutosha.”
Kupiga hatua zaidi ya ufafanuzi, Nipashe iliyoamua baadhi ya wazazi, akiwamo Janeth Samwel, anayesimulia kwamba amejikuta akiangua kilio, baada ya binti yake wa miaka 10 kuvunja ungo.
“Nilihisi kama kuna hatari inamkabili binti yangu, sikuamini kama ni kawaida,” anasimulia mzazi Janeth, anayetamka kwa sauti ya unyonge.
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za kitabibu, lishe duni kwa mtoto, huchelewesha kutolewa homoni muhimu kifaya, mathalan zilizo maarufu ‘estrogen’ kwa wasichana na ‘testosterone’ kwa wavulana.
Hitilafu katika lishe anayopata mwanadamu huyo, inaelezwa na watalamau kwamba ina uhusiano wa moja kwa moja, kuchelewesha kumpevusha kijana, kwa maana ya kubalehe.
Kibaolojia ni kwamba, kuwapo lishe bora, ni tiba ya kwanza kuuwezesha mwili wa kijana huyo kutoa homoni kwa wakati unaofaa, hivyo kuchochea ukuaji wa kawaida kiafya kwa baiolojia ya vijana hao.
DARASA LA KITABUNI
Kitabu cha Mafunzo ya Lishe kwa Ajili ya Watoa Huduma wa Vituo vya Afya, maarufu ‘Kitabu cha Mshiriki (2019)’ kilichotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), inaelezwa namna lishe kuwa mchakato wenye hatua na jinsi mwili unavyokitumia chakula kilicholiwa.
“Hatua hizi ni kuanzia chakula kinavyoliwa, kinavyosagwa, kumeng’enywa, kufyonzwa na kutumika mwilini,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho.
Kitabu hicho kinafafanua kuwa lishe bora inahusush mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi matano, ikiambatana na mazoezi ya mwili misingi inayojenga afya bora na ustawi wa uzazi wa baadaye.
Kwa upande mwingine, inaelezwa kuwa ni hali ya mwili kutopata virutubishi vinavyokidhi mahitaji yake, jambo linaloweza kusababisha kudhoofika kwa kinga ya mwili, kuongezeka kwa magonjwa na kuchelewa kwa ukuaji wa ubongo na mwili kwa ujumla.
Wataalamu wa lishe wanabainisha kuna vyakula vinavyochangia kuimarisha afya ya uzazi na kasi ya ukuaji mwili.
Kuna mifano inayotolewa kusaidia makuzi hayo ni: Mboga za majani kama mchicha, kale na broccoli, zenye viinileshe aina ya ‘folate’ inayosaidia afya ya yai la mwanadamu.
Pia, kuna matundakwa jina la ‘berries’ zenye msaada wa kuzalisha chembe hai za uzazi kwa mwanadamu.
Hali kadhalika, kitaalamu zinatajwa, parachichi, karanga na mbegu chanzo cha viinilishe ‘omega-3 fatty acids’ zinazosaidia kupatikana homoni zinazohitajika.
Pia, kuna mlo; maziwa yenye mafuta kamili, viazi vitamu, maharage, dengu, mafuta ya mizeituni, nafaka nzima na komamanga, vyote vikihangia kuimarisha afya ya uzazi na ukuaji wa vijana.
MTAALAMU LISHE
Ofisa Lishe Mwandamizi, anaitafsiri lishe bora kutoishia kwa afya ya mwili pekee, pia ni nguzo muhimu katika safari ya mtu kukua na kupevuka.
“Watoto wanaokula mlo kamili wenye protini, madini ya chuma, vitamini na mafuta yenye afya hukua haraka na kuanza kubalehe kwa wakati unaotarajiwa,” anabainisha.
Gwarasa anawataja watoto wanaokosa lishe bora au kula vyakula vya aina moja hasa wanga bila ya protini na vitamini, ukuaji wao huchukua hatua taratibu na wanachelewa kupevuka miili yao.
Gwarasa anaeleza kuwa, lishe bora kwa vijana balehe (wenye umri wa miaka 10 hadi 19) ni muhimu, kwani kipindi hicho ndicho cha mabadiliko makubwa hutokea kutoka utotoni kwenda utu uzima.
“Upungufu wa virutubisho kwa vijana wa kike una athari kubwa kiafya, ikiwamo kudhoofika kwa mfumo wa uzazi na kuchelewa kukomaa kwa viungo,” anaongeza.
Kitabu cha TFNC kinaeleza kuwa lishe duni husababisha athari za muda mrefu kama: Udumavu wa kimo, udhaifu wa kinga ya mwili, mtoto kuchelewa kuongea, athari katika ubongo na uwezo mdogo wa uzalishaji katika utu uzima.
Wataalamu pia, wanatahadharisha kuwa lishe hafifu katika ujana, inaongeza hatari ya kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza kama magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu na saratani katika umri utu uzima.
Hapo inaibua rai ya wataalamu, wakiwashauri wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata lishe kamili kila siku, kwa kuwa ndicho chanzo cha ukuaji mzuri kwa mwili yao, pia kinga imara na uwezo wa kupevuka kwa wakati.
Ni dhana inayosonga mbali kiserikali, ikiifanya kuwa sehemu ya elimu rasmi katika mitaala kifataifa, pia katika mustakabali usio rasmi wa kampeni za kitaifa.
Pia, wajibu huo wa kufuata miongozo lishe, iliyomo kwenye sera za kitaifa, mathalan inayohusika na lishe ikitolewa hadi kliniki, hali kadhalika kuwajibisha kisheria jukumu la kuhakikisha mtoto anapata mlo stahiki, kama vile kwenye Sheria ya Mtoto nchini
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED