VITA YA TEKNOLOJIA DUNIANI; Ndivyo China ‘inavyoitoboa’ macho Marekani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:39 PM Oct 15 2025
Rais wa China Xi Jinping,
Picha: Mtandao
Rais wa China Xi Jinping,

MAREKANI iliona ni mpango bora wa kibiashara kampuni zake kama Apple kuwekeza mitaji China na kuzalisha kwa kigezo cha unafuu wa gharama na nguvukazi, hivyo kupata faida kubwa zaidi.

Lakini, pengine bila kujua, kampuni za Marekani zilipeleka kwa washindani wao wa baadaye nguvu na ujuzi wa teknolojia itakayoishi daima baada ya kuwapa ujuzi wa kuzalisha simu za mkononi, magari ya umeme na bidhaa nyingi za kielektroniki, China imeendeleza uwezo wake wa viwanda, kiteknolojia na rasilimali watu ambao ni vigumu kwa nchi nyingine kushindana nayo leo.

Wakati kampuni za Marekani zilitumia China kuzalisha kwa sababu ya unafuu, China ikibamba fursa hiyo kuimarisha maendeleo yake kiteknolojia. Kyle Chan, mtafiti wa Chuo Kikuu cha Princeton, anasema China ilifanya juhudi makini kuvutia na kutumia kampuni kama Apple kuboresha uchumi kikamilifu.

"Haikuwa rahisi kusema, 'sawa, njoo uzalishe hapa na utajirike, kila mtu atafurahi.' Hapana. Ni kama kusema, 'lazima uchangie kitu katika maendeleo ya China.Na sio Apple tu, bali pia Volkswagen, Bosch, Intel, SK Hynix, na Samsung," Chan anaeleza, akisema wataalamu wanakubaliana kuwa China ni kituo kikubwa chenye nguvu ya teknolojia duniani.

Siku za Marekani kuwa nchi pekee yenye uwezo wa kuzalisha teknolojia inayobadilisha historia ya binadamu zimekwisha, na sasa kuna ushindani mkali katika kila sekta.

"Sasa si mbio za farasi mmoja," Han Shen Lin, mkurugenzi wa China wa kampuni ya ushauri ya Marekani The Asia Group, anaiambia BBC.

ILIVYOANZA

Katika kitabu chake Apple in China: The Capture of the World's Greatest Company, Patrick McGee anasema, kwa mujibu wa mahojiano ya zaidi ya wafanyakazi 200 wa zamani wa Apple, uamuzi wa Apple kuzalisha zaidi ya asilimia 90 ya bidhaa zake China haukuwa tu kwa sababu ya faida, bali pia fursa ya ujuzi.

"Utajiri wa Apple na uwezo wake wa kiutengenezaji uliwasaidia Wachina kufundishwa, kusimamia na kupewa stadi ambazo Beijing sasa inatumia kama silaha dhidi ya Magharibi," anasema McGee, mwandishi wa zamani wa Silicon Valley wa Financial Times.

Silicon Valley  ni eneo la Kaskazini mwa California eneo la San Francisco Bay ambalo ni maarufu kwa tasnia yake ya teknolojia ya juu.

Profesa Chan anaeleza kuwa, kadri muda ulivyopita, wasambazaji wa kigeni waliokuwa sehemu ya mnyororo wa uzalishaji wa simu za iPhone na vifaa vingine vya Apple walianza kukosa nafasi ambazo zilichukuliwa  na wasambazaji wa China.

"Kuanzia  glasi, lensi,kioo au skrini na aina za kamera."

Uchambuzi wa mwaka 2024 wa gazeti la Japan Nikkei Asia, asilimia 87 ya wasambazaji wa Apple wana viwanda China na zaidi ya nusu wanakaa China au Hong Kong, ingawa Apple imejaribu kusambaza uzalishaji wake nchi nyingine, bado inategemea sana wazalishaji na wafanyakazi wa China wanaolipwa kati ya dola 1 na 2 kwa saa.

McGee anadai kuwa, kama China ingependa, serikali ingeweza kusitisha uzalishaji wa Apple mara moja.

Zaidi ya kuwa mzalishaji mkuu wa Apple, China pia imejifunza kuzalisha simu zake, magari ya umeme na mifumo ya akili unde  (AI) yenye umahiri sawa na ya Marekani, wakati wataalamu na uwekezaji wa mamilioni kutoka Apple na kampuni nyingine za magharibi vilihamishia ujuzi muhimu kwenda China, na kuisaidia kuibuka kwa kampuni kubwa kama Huawei, Xiaomi na BYD.

Leoingawa Marekani bado ipo mbele, China ina kampuni zake kubwa za kushindana na Marekani hata kama inaongoza katika teknolojia kuu, lakini China inakwenda kwa kasi kupata ujuzi katika uvumbuzi na uwezo wake wa kuzalisha sana,anaeleza  Han Shen Lin, lakini Kyle Chan anaongeza : "China imeanza kuipita Marekani katika baadhi ya maeneo na lililo kubwa ni mwendo wake wa kasi."

MAPAMBANO  AI

Sekta moja inayoonyesha ushindani mkali kati ya Marekani na China ni akili unde, ingawa China imewekeza sana katika AI kwa miongo kadhaa, Marekani ilionekana mbele na mfumo wa GPT-3, mfano wa lugha wa mapinduzi uliozinduliwa na OpenAI mwaka 2020, lakini, ghafla, DeepSeek, chatbot ya China iliyo karibu na ChatGPT, iliibuka Januari mwaka huu. Waundaji wake wakisema iligharimu sehemu ndogo tu ya ile ya Marekani na sasa Rais Donald Trump anaanza kustuka kwenye tasnia ya teknolojia ya Marekani.

Mtaalamu Chan anasema: "Siyo tu kuwa mfano wa Kichina ulikuwa karibu sawa na mfano bora wa Marekani kwa gharama ndogo, bali pia ulifanywa kwa kukwepa vizuizi vya kuuza AI nje."Tangu 2022, Marekani imewazuia wateja wa China kununua Nvidia H100 ‘ kichakata taarifa za kielektroniki kinachotumia akili unde,’ zilizotumika zaidi kwa mafunzo ya AI. Badala yake, Nvidia inazalisha toleo dogo lililolengwa kwa wateja wa China.

Kwa Chan, uzinduzi wa chatbot wa China unaoshindana na ule wa Marekani ulikuwa ni jambo la "kizalendo".

"Kwa Wachina, ilikuwa changamoto dhidi ya utawala wa Marekani," anasema.

Mfano ni Huawei, ambayo mwaka 2019 iliongezwa kwenye ‘Entity List’ au ‘orodha ya bidhaa zilizowekewa vikwazo na Marekani’ kwa tuhuma za ujasusi, wizi wa mali za kiakili au bunifu na uangalizi wa data.

Matokeo yakawa,  simu za Huawei haziwezi kutumia Android ya Google, lakini baada ya kushambuliwa, Huawei ilitumia miaka kadhaa kuendeleza mfumo wake na chips za SoC. “Sidhani wangefanya hivyo kwa kiwango hiki bila vizuizi vya Marekani," Chan anasema.

FAIDA CHINA

Marekani iliongoza teknolojia kwa sababu ya nguvu ya sekta binafsi, motisha ya uchumi kwa uvumbuzi na nishati kubwa. China inafaidika kwa uwekezaji wa serikali ikiwa na sera ya viwanda inayowezesha sekta muhimu. Inafaidika na kwa muda mrefu na mpango wa uwekezaji unaoendana na soko, kwa mpango wa muda mrefu, hata kama haileti faida mara moja.

Ushindani mkali ndani ya nchi ni faida nyingine kwa China ambapo serikali za mitaa zinasaidia biashara zao na kuandaa "mashindano " ya ndani.

China inaweza pia kujaribu teknolojia mpya kwa idadi kubwa ya watu, ikichangia utafiti na maendeleo, kwa mfano, sekta ya dawa, watoa dawa wanaweza kujumuisha wagonjwa haraka, kutumia kanzidata ya kitaifa na kuharakisha majaribio ya dawa.

Leo teknolojia imejumuishwa kwa urahisi katika maisha ya kila siku, kwa mfano Akili Unde inahusika katika kusambaza bidhaa na huduma, malipo bila pesa taslimu na biashara mbalimbali.Hata hivyo, Chan anaonya kwamba bila ushirikiano wa nchi nyingi, China inaweza kupata changamoto.

BBC