Katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, zaidi ya watu milioni 940 bado hawana upatikanaji wa uhakika wa umeme, huku zaidi ya milioni 700 wakitegemea nishati hatarishi kama kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Nchini Tanzania, zaidi ya nusu ya wananchi—takribani watu milioni 36—wanaishi bila umeme. Jamii nyingi vijijini hulazimika kutumia mafuta ya taa, kuni na mkaa kwa ajili ya mwanga na kupikia, hali inayosababisha changamoto nyingi kiafya na kijamii.
Wanawake ndiyo wanaoathirika zaidi. Wengi hutumia muda mwingi kukusanya kuni na kuvuta moshi wenye sumu wakati wa kupika, jambo linaloathiri afya zao na kuwanyima muda wa kujishughulisha na kazi za kiuchumi. Wengi wao pia hukosa chanzo cha kipato cha kudumu.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, Puma Energy Foundation imeungana na Solar Sister, shirika linalowawezesha wanawake kuanzisha biashara za kuuza taa na bidhaa nyingine za nishati safi katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tangu kuanzishwa mwaka 2010, Solar Sister imeunda mtandao wa zaidi ya wajasiriamali wanawake 12,000 waliowafikia watu zaidi ya milioni 5.5 katika ukanda huo. Wajasiriamali hawa hupewa mafunzo ya masoko, uhasibu, mipango ya biashara, ushauri, na upatikanaji wa mikopo midogo.
Nchini Tanzania pekee, mpango huu umechangia kufikia zaidi ya watu milioni 2.3 tangu ulipoanzishwa mwaka 2013, huku ukibadilisha maisha ya maelfu ya wanawake vijijini.
Awamu ya kwanza ya ushirikiano kati ya Puma Energy Foundation na Solar Sister, iliyoanza mwaka 2023, ililenga katika Mpango wa Kukuza Biashara.
Kupitia mpango huu, wanawake 579 nchini Tanzania walipata mafunzo ya ujuzi wa kidijitali, mbinu za biashara na upatikanaji wa teknolojia kama simu janja. Hii imewawezesha kuongeza mauzo, kipato na kufikia kaya nyingi zisizo na umeme kwa kutumia nishati safi.
Awamu ya pili ya ushirikiano, iliyoanza mwaka 2025, inalenga kuajiri na kuwafundisha wanawake 500 zaidi katika mikoa mitatu mipya. Pia, wanawake 200 wanapewa mafunzo ya biashara za kidijitali na wanatarajiwa kuuza bidhaa 16,000 za sola, zikiwemo majiko safi 2,000.
“Lengo si kuuza bidhaa za nishati pekee,” alisema Cesear Mloka, Mkurugenzi Mkaazi wa Solar Sister Tanzania.
“Ni kuwawezesha wanawake kujiamini, kupata uhuru wa kifedha na heshima katika familia na jamii zao.”
Neema Ally, mkazi wa Songwe, alikuwa akifanya kazi ya kulima mashamba ya watu wengine kwa kipato kidogo. Ndoto yake ya kumiliki shamba lake ilionekana mbali hadi alipojiunga na Solar Sister.
Kupitia mafunzo na biashara ya sola, Neema aliweza kukodisha ekari tano za ardhi, kulima mahindi, na sasa anaajiri wengine kijijini kwake huku akigharamia elimu ya watoto wake.
Theresia John Robert, kutoka Kaskazini mwa Tanzania, alikuwa akipata riziki kwa kuponda mawe kwa mikono. Mwaka 2017 alijiunga na Solar Sister na kuanza kuuza taa za sola na majiko safi.
Mwanzoni alikuwa na hofu ya kuzungumza na wateja, lakini baadaye alijijengea ujasiri, akasafiri kwa baiskeli kufikia vijiji vya mbali. Sasa amejenga nyumba yake, kitu ambacho hapo awali alidhani hakiwezekani.
Hadithi zao zinaonyesha namna upatikanaji wa nishati safi unavyoweza kuibadilisha jamii — kutoka kwenye umaskini hadi kwenye ustawi na ujasiri wa kiuchumi.
Kupitia ushirikiano ulioboreshwa na Puma Energy Foundation, Solar Sister inalenga kuwafikia watu 85,000 nchini Tanzania kwa bidhaa za nishati jadidifu zenye kiwango cha chini cha kaboni. Hatua hii itapunguza hewa chafuzi, kuboresha afya za kaya na kuimarisha uthabiti wa tabianchi.
Lakini faida kubwa zaidi ipo kwa wanawake: kuwawezesha kiuchumi, kuwapa sauti na nafasi ya uongozi katika jamii zao.
“Tunajitahidi kuboresha maisha na kuleta mabadiliko yenye tija katika jamii,” alisema Laura Fruehwald, Meneja wa Programu wa Puma Energy Foundation.
“Kupitia ushirikiano huu, nishati si tu chombo cha matumizi ya kila siku, bali kichocheo cha uwezeshaji na maendeleo endelevu.”
Nchini Tanzania, kampuni ya Puma Energy inaendelea kusaidia juhudi hizi kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma za nishati safi ya kupikia zilizo bora na nafuu. Hii ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya kupikia kwa nishati safi, inayolenga kupunguza hatari za kiafya na athari za kimazingira.
Kwa kuunganisha nguvu ya wanawake wajasiriamali na dhamira ya kutoa suluhisho la nishati safi, ushirikiano kati ya Puma Energy Foundation na Solar Sister unaunda njia jumuishi ya maendeleo endelevu — yanayojikita katika uwezeshaji, ustawi na maisha bora kwa Watanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED